Miongoni mwa maafa yaliyowasibu watu na jamii ni dhana mbaya, jambo ambalo linakata mapenzi kati ya watu, na mwenye dhana mbaya huwaangalia watu kwa jicho ovu, na bila shaka dhana mbaya ni kinyume na sheria ya kiislamu.
Ili mafungamano baina yetu na watu yabaki kuwani imara ni kuwakabili watu hali ya kuwa nyoyo zetu zimesalimika pia kuwa safi na nyuso kuwa na bashasha na kuwadhania watu kwa dhana nzuri pindi tunaposalimiana nao. Tunapozingatia mafungamano ya Waislamu yamesambaratika kutokana na dhana mbaya. Unaposikia maongozi ya Waislamu tunasikia wakisema fulani amekusudia hivi, na fulani ametaka jamabo hili. Yote yanapelekea kupatikana kwa chuki na mwisho ni kuvunjika au kusambaratika kwa mafungamano. Dhana mbaya inapeleka kufuatilia aibu za watu na kuchunguzana kwa ajili hiyo utasikia kwa mwenye dhana mbaya akisema ‘Nitajaribu kuhakikisha’ basi atachunguza na kusengenya na kumtaja mwenzake kwa uovu. Kuenea kwa dhana mbaya kunakosekana uaminifu kati ya watu na kukatana jambo ambalo kwamba linapelekea kutofaulu katika mambo yetu.
Anasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال الله تعالى) : وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ) [الأنفال: 46]
{{Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkaharibikiwa na kupotea nguvu}}.
Dhana mbaya haileti kheri na ni njia ya kuenea kwa uadui na kupatikana kwa madhambi hayo duniani ama kesho akhera ni majuto. Tazama watu waovu walivyo wakejeli Waislamu na kuwadhania maovu pindi Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Aliposema:
قال تعالى (وَقَالُوا مَا لَنَا لَا نَرَى رِجَالًا كُنَّا نَعُدُّهُمْ مِنَ الْأَشْرَارِ 62 أَتَّخَذْنَاهُمْ سِخْرِيًّا أَمْ زَاغَتْ عَنْهُمُ الْأَبْصَارُ) [ص62: 63]
{{Kisha wale wabaya watasema: Imekuwaje, Mbona hatuwaoni wale watu tulikuwa tukiwahesabu katika waovu kwa kumfuata Muhammad. Je, tuliwafanyia mzaha (huko duniani, na hali yakuwa ni watu wakubwa Akhera au wamo Motoni humu pamoja na sisi) ila macho yetu haya waoni tu ?}}.
Anasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى) : فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آَمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ 34عَلَى الْأَرَائِكِ يَنْظُرُونَ35 هَلْ ثُوِّبَ الْكُفَّارُ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ) [المطففين34: 36]
{{Basi leo walioamini watawacheka waliokufuru. Watakuwa Juu ya viti vya fahari, wakitazama (neema zao). Je, makafiri wamepewa malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda?}}.
Anasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
(يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ) [الحجرات: 12] قال تعالي :
{{Enyi mlioamini, Jiepusheni sana na dhana mbaya. Kwani dhana mbaya ni dhambi}}.
Inajulisha Aya katika kuhifadhi heshima ya Muislamu kwa kutangulia na katazo la dhana. Ni uzuri ulioje kwa mujtama ulio salimika na dhana mbaya. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Jiepusheni na dhana hakika ya dhana ni maongezi ya uongo wala msichunguzane wala msichukiane kuweni ndugu katika waja wa Mwenyezi Mungu].
Wamesema baadhi ya wanavyuoni dhana ambayo inafaa kuepukwa ni ile ambayo kwamba haijulikani njia yake kuwa ni ya sawa na sababu iliyokuwa ya wazi, mfano anayedhaniwa akiwa ni mtu mwema na akapewa amana kuwadhania kuwa amekhini ni haramu. Kinyume na ambae anajulikana anayefanya maovu wazi wazi kwa ajili hiyo wamesema wanavyuoni dhana mbaya kwa mtu mwema haifai na hapana tatizo kudhania uovu mtu muovu.
Imepokewa hadithi Said ibn Musaib akisema: “Amewaandikia baadhi ya maswahaba kutowacha kufanya wema kwa jambo la ndugu yake maadamu hujashindwa wala asidhani neno baya limetoka kwa ndugu yako ikiwa inawezekana kuchukulia kwa uzuri na huo ndio mfano wa watu wema pindi wanaposhindwa kuelewa baadhi ya maneno, kwa kuwahukumu makosa watu wengine bila ya kuzingatia nia na hali ya yule mtu”. Ibn Qayyim amesema: “Neno moja husemwa na watu wawili mmoja wao anakusudia haki na mwingine wao anakusudia batili kwa ajili hiyo hahukumiwi mtu kuwa kafiri kwa aliyesema “ Ewe mola wangu wewe ni mja wangu na mimi ni mola wako” hakukusudia kujifanya Mwenyezi Mungu. Amesema Sheikhul Islam Ibn Taymiyya pindi anaponukuu maneno ya wenye kumkhalifu akisema “Maneno haya yana upana, na haki huchukuliwa kwa uzuri na batili huwa na mambo mengi”
Mwanadamu hana haki kwa ndugu yake isipokuwa kwa mambo yaliyo wazi. Amepokea Abdulrazaq kutoka kwa ‘Umar Ibn Khattab akisema: “ Watu walikuwa wakipokea wahyi wakati wa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na wahyi ukakatika, lakini tunachukua sasa kwa yale yaliyodhihiri kutokana na vitendo vyenu kwa atakae dhihiri kheri tutamuamini na tutamkaribisha haitujalishi sisi usiri wake na Mwenyezi Mungu ndiye atakaye muhesabu kutokana na usiri wake na atakae dhihiri shari lake kwetu hatutomuamini wala hatutomsadiki hata akisema kuwa usiri wake ni mwema”. Kwa Muislamu ahesabu kuwa kila neno analozungumza au hukumu anayotamka na akumbuke Neno lake Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى (وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ) [الإسراء: 36]
{{Wala usifuate usiyo na ilimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa}}.
Waja wa Mwenyezi Mungu sababu za dhana mbaya ni kuinukia mtu katika mazingira maovu na atakayefuata matamanio yake ataingia katika dhana mbaya; kupenda kitu humfanya mtu kuwa kipofu na kiziwi, mwanadamu akifuata matamanio yake kwa kumpenda mtu mwingine makosa yake huwa ni mema na akimchukia mtu mwingine mema yake huwa ni maovu. Baadhi ya watu wanajiinua utu wao na kujiona saa zote kuwa wao au yeye siku zote yuko katika haki na watu wengine wako katika batili na kujitakasa nafsi yake kwa kudharau watu wengine jambo ambalo linaleta dhana mbaya kwa watu wengine.
Dhana mbaya ni sababu ya kupatikana tuhuma kwa watu na kuwagura bila ya sababu ya kisheria na kuwadhulumu kama alivyosema msemaji: “Naona uadui wala sioni sababu zake yote ni kutokana na mshikamano uliokatika, dhana ilivyokuwa na madhambi, na kusengenya kulikokuwa kuovu.
Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى (وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُبِينًا ) [الأحزاب: 58]
{{Na wale wanaowaudhi wanaume Waislamu na wanawake Waislamu pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri}}.
Suluhisho la dhana mbaya
Kuwadhania watu dhana nzuri, fikiri kwa kina kabla hujatoa hukumu na kutuhumu kwani kukosa kwa kumdhania mtu mwema ni bora kuliko kwa kumdhania mtu uovu. Amesema ‘Umar : ‘Dhania kheri kwa neno litakalo kwa ndugu yako baada ya kuwa na dhana, ikiwa panapatikana ndani yake kheri’.
Kutoa udhuru kwa watu na kutofuatilia aibu za watu na kuwajibika ni katika adabu za kiislamu katika kutoa hukumu kwa watu na kumuachia Mwenyezi Mungu mambo yaliyojificha.
Mwisho
Ndugu katika Imani, tumeona hatari mbaya ya Muislamu kumdhania Muislamu mwenzake vibaya, na athari yake katika jamii ya kislamu. Jamii ya kislamu ni jamii iliyo hifadhiwa na sheria za Allah (Subhaanahu wa Taala). Muislamu akipata khabari yoyote kuhusu Muislamu mwingine ni lazima kwanza apime khabari hiyo kwa mizani ya sheria, ili aweze kujuwa ukweli wa khabari hiyo.
Namuomba Mwenyezi Mungu atuondelee dhana mbaya na atuwezeshe kuwadhania watu dhana mzuri, na kuwapa udhuru watu.