FADHLA ZA KUSOMA QUR’ANI


7700
wasifu
Qur'ani tukufu ni maneno ya Mwenyezi Mungu na ni kitabu Chake kitukufu. Si kama maneno yoyote wala kitabu chochote, ni Teremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima Mwenye kuhimidiwa. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kushinda Ameweka adabu ambazo yatakikana zitungwe wakati wa kuisoma, kwa kuitukuza na kuiheshimu, Akamuamuru Mwenye kuisoma awe na tohara na awe mnyenyekuvu na mwenye kukizingatia anachokisoma na adabu nyinginezo ambazo yapaza kuzitunga wakati wa kusoma Qur'ani.

Ewe Muislamu ulipoumbwa na ukaletwa hapa Duniani uliwekewa katiba na mfumo wa kuishi na njia ya kupita mwanzo mpaka mwisho, nzuri na mbaya, yote hayo utayapata kwenye Qur’an ukifundishwa na Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Kusoma Qur’an na Adabu zake

Baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumtakia rehema Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na kutakia radhi Maswahaba na waliokuja baada hao mpaka qiyama.

Ama baadu: mazungumzo yetu ni kuhusu kitabu ambacho ndio msingi wa kufaulu kwenu, chenye kuwatoa kwenye kitua, ndani yake kuna khabari ya waliokuja kabla yenu na watakaokuja baada yenu na hakimu kati yenu, chenye kupambanua baina ya haki na batili. Mwenye kukiacha ameumia, mwenye kutaka uongofu kwa hicho ataongoka, na mwenye kutaka kuongoza na kitabu kingine amepotea; ni kamba ya Allah ya kuaminika isiyokatika; ni utajo wa Mwenyezi Mungu ni njia iloyonyoka, mwenye kuifuata hapotei na mwenye kuifuata hachanganyikiwi. Hawashibi nayo wanavyuoni na maajabu yake hayapungui. Atakaye ukweli ataupata humo na mwenye kuhukumu nacho atahukumu kwa usawa. Matakwa ya Allah ni tuisome Qur’an ili atuongoza na atuingize peponi.

Enyi waumini, Someni Qur’an na muwasomeshe watoto wenu au wenzenu, muwe mumebebwa na mazingira yake, frikra zenu na mawazo yawe katika mazingira ya Qur’an, muwahifadhisha watoto wenu kwa udogoni, kwani mkifanya hivyo, inaifanya igande vizuri zaidi ndani ya nyoyo zao, kwani kuhifadhi udogoni ni kama kutia naqshi kwenye jiwe.

Ewe waja wa Mwenyezi Mungu, Muongopeni Mola na muwe na hamu na Kitabu hiki. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله عز وجل: (إنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنْفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَنْ تَبُورَ لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُمْ مِنْ فَضْلِهِ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ) [فاطر: 30]

{{Hakika wanaosoma hiki Kitabu cha Allah na wakasimamisha swala na wakatoa kwa mali yao tulizowapa kwa siri na dhahiri, wanatarajia biashara isiofilisika, na hakika Allah atawalipa awaongeze, kwani yeye mweyekusamehe saana na ni mwenye kushukuriwa}}. Na mke wa Mtume ‘Aisha akazidi kutufafanulia akisema: ‘Kusoma kwa Qur’an kunatafautiana, kuna anayesoma hodari. Hivyo, thawabu zake ni nyingi kiasi cha kutangamana na Malaika na anayesoma akigongagonga atapata malipo mara mbili. Vilevile Abi Umama akamwambia amemsikia Mtume akisema: [Someni Qur’an, itakufaa siku ya Qiyama kuwaombea shufaa. Haya yote ni fadhila za Qur’an na fadhila za kusoma Qur’an]. Na Mtume wetu (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimuusia Abu Said akimwambia : [Nakuusia umche Mwenyezi Mungu, kwani hilo ndio kichwa cha kila kitu, na utoke kwenda Jihad kwani hilo ndio daraja kuu la Uislamu na umtaje Mwenyezi Mungu kwa wingi, na usome Qur’an ukifanya hivyo roho yako itakuwa mahali pazuri mbinguni na utakuwa na utajo upo ardhini].

Adabu za kusoma Qur’an

Kusoma kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Taala)

Waja watalipwa kulingana na nia zao. Mtume anatutolea khabari kuwa watu watalipwa vibaya japokuwa tunawaona wakifanya mema, nao ni sampuli tatu:-

Mtu anajishughulisha na Qur’an kuisoma vizuri, kuikusanya n.k

Mtu aliyeuliwa jihad fi sabilillahi.

Mtu tajiri anaye toa sana.

Kumbe wote hawa watatu, wanafanya riya, Allah atamwambia msomaji Qur’an: Si nilikufundisha Qur’an? Atajibu: Ndio ewe Mola; baadaye ulifanya nini? atajibu nilikua nikiisoma usiku na mchana, Mwenyezi Mungu atasema: ‘Umesema urongo, na Malaika watazidi kumkaripia ‘muongo we, na watasema Ewe Mola: huyu bwana, alikuwa akisoma kwa ajili ya watu, na tukaachia watu wamlipe kule kule duniani. Mungu atawaamrisha Malaika wamtie motoni (Mwenyezi Mungu atulinde na hayo)

Kusoma hali akiwa na utwahara

Hapana shaka kuyasoma maneno ya Allah ukiwa msafi, ndio bora kama vile kupiga mswaki, kutawadha n.k. Kwa sababu Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Hakika midomo yenu, ndiyo njia za kusoma Qur’an, isafisheni kwa miswaki]. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akasema tena: [Ikiwa mja anaswali, Malaika humjia, na wakamsimamia nyuma yake wakimsikiliza Qur’an na wanaendelea hivyo mpaka anyamaze]. Na je ikiwa mja kinywa chake chanuka? Malaika watakaa kando.

Kusoma kisawasawa

Mola wetu anatuamrisha kuisoma Qur’an na Mtume wetu anatushinikiza hivyo, na maswahaba wakisoma Aya Aya, mmoja wao ni Anas bin Malik Anatuambia Mtume akiwafundisha hata kuvuta Bismillahi na kadhalika. ‘Abdallah bin Masuud amesema, “Kusoma haraka haraka ni mbaya bali ni usome pole pole, ipate kugonga ndani ya moyo, na usimame katika Aya za maajabu, igonge moyo”. Albara amesema: ‘Nimemsikia Mtume akisoma Wattini Wazzaytuni kwenye Swala ya Ishaa. Sijawahi kusikia sauti nzuri kama hiyo’. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Tengenezeni sauti zenu mnaposoma Qur’an]. Na hizo hadithi ni swahihi. Ni vizuri asome kwa sauti ya kuimbia ya kughani, imepokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Si katika sisi yule mtu atasoma Qur’aan na haghani]. Na kughani kwenyewe ni mume kwa sauti ya kiume na mke ajikaze, sio sauti kuwavutia wengine, na asome asimame kwenye mwisho wa kila Aya kama anavyotueleza mke wa Mtume Ummu Salama.

K usoma kwa kwa sauti ya chini

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alitufundisha, tusisome kwa sauti ya juu, mpaka tukawaudhi wengine. Kwa mfano, wengine wanaswali na majirani wamelala, soma kwa kiasi. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anatuambia katika maana ya hadithi: “Nyote mtaitwa na mola wenu, msiudhiane wala msipandishiane sauti nyingi na kama mtu anasinzia aache kusoma alale, asije akasoma makosa makosa asijijue, na asiache sura zile fadhila zaidi kama suratul-Ikhlas, ambayo ni theluthi ya Qur’an. Na katika riwaya kadhaa Mtume amekuwa akisema: [Suratul-Ikhlas, ni theluthul ya Qur’an. na alikuwa akisoma Suratul Sajdah na Suratul Insaan katika Sala ya Alfajiri, na Tabaraka na Surat Al-Falaq na An-Nisa kabla ya kulala. Na vile vile akisoma Surat Al-Falaq na An-Nisa na Ayatul-Kursiyu baada ya kila swala].

Kukatazwa kusoma Qur’an katika rukuu na Sijida

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) mwenyewe ametukataza hilo kwenye hadithi swahihi akisema: [Enyi watu, hakukubakia kwenye bishara za mitume isipokua ndoto za watu wema, nami nimekatazwa kusoma Qur’an kwenye rukuu na sijida. Mtukuzeni Allah na mjitah idi kwa dua]. Na sababu yake ametaja Sheikhul-Islam, kukaa rukuu na sijida ni pahali pa kujidhalilisha Muislam kwa Mola wake.

Kulia wakati wa kusoma Qur’an

Mola Anasema kulingana na maana ya Aya Akiwasifu waumini ya kuwa; wanaposomewa Qur’an wanapomoka kusujudu huku wanalia na hio linawanazidisha kumcha Mwenyezi Mungu. Maswahaba wengi walikua wakilia kwa sababu ya ucha Mungu na kumfuata Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Mmoja wao ni Ibnu Mas’uud aliyesema: ‘ Siku moja Mtume aliniambia nimsomee, nikamjibu kwani Qur’an, inakuteremkia wewe iweje mimi nikusomee?. Mtume akasema: [Napenda nimsikie mtu akisoma. Nikasoma suratul Nisaa mpaka nikafika Aya fulani, nikaona macho ya Mtume yakitoka machozi].

Mmoja katika maswahaba amesema: ‘Nilimjia Mtume naye akiwa anaswali na ana kitambaa akijifutia nacho machozi. Na habari mashuhuri kwa Abu Bakr anaposoma Qur’an katika kuwasalisha alikua akilia. ‘Umar ibnu Khattwab alipokuwa akisoma Aya, alisikia sauti za kilio na yeye akalia akadondokwa na machozi. Mke wa Mtume ‘Aisha amewahi kupita sehemu mbalimbali watu wasoma na ukali. ‘Abdullah Ibnu ‘Abbas alikuwa akisoma Qur’an na akirudia rudia na wasikilizaji wakilia.

Kilio wakati wa kusoma Qur’an ni dalili ya kumcha Mwenyezi Mungu ikiwa ni kilio cha kweli, kwani kilio kiko namna nyingi:- kilio cha rahma na sikitiko, kilio cha kumuogopa Allah, kilio cha mapenzi na shangu, kilio cha furaha na kilio cha huzuni. Kilio kinachotakikana ni cha kumuogopa Mwenyezi Mungu na sio cha kinafiki na riya cha kujifanya unamuogopa Allah. Na kilio cha kumuogopa Mungu, yule msikilizaji naye huhisi kumuogopa Mwenyezi Mungu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Hakika sauti nzuri ya Qur’an ni ukisikia wamuona mwenzio anamuogopa Mwenyezi Mungu].

Ama kujiliza na kujikamua kulia ni sampuli mbili:-

Namna imesifiwa nzuri

Namna imesifiwa vibaya.

Kusifiwa vizuri, kama alivyojiliza ‘Umar alipomuona Mtume na Abubakar wanalia, alipowauliza sababu, wakachelewa kumjibu, na ‘Umar akakianza chake. Watu wema waliotangulia wanasema: lieni kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu au lizaneni.

Ama kilio kinacholaumiwa ni mtu kujifanya mwema mbele ya watu kwa kulia hiki ni kilio cha unafiki. Kwa yote hayo ni Muumini alie anaposoma Qur’an, khabari zikitokana na mama ‘Aisha, amemsikia mmoja kati ya masahaba watukufu akisema yeye kama ni kulia basi ni moja katika aina tatu:-

Akisoma Qur’an na akisikia inasomwa.

Akisikia khutba ya Mtume.

Akiona jeneza.

Kuizingatia Qur’aan

Ukisoma Qur’an na ukizingatia, ndio jambo muhimu zaidi ambalo linazaa matunda Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anasema:

قال الله تعالى) : كِتَابٌ أَنْزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِيَدَّبَّرُوا آَيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ) [ص: 29]

{{Tumeteremsha kitabu kilicho barikiwa, basi kisomeni na mkizingatie enyi mulio na akili}}. Basi tukisome na tukifikirie na tukifahamu vilivyo. Na ikiwa hatuzingatii Mwenyezi Mungu Atatuuliza ilikuaje wasikizingatie ama nyoyo zao zimefungwa, nyuma ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) baada ya Fatiha akaanza Baqarah akarukuu baada ya kumaliza Aya mbili akaanza rakaa nyengine baada ya fatiha akasoma suratul Al-‘Imran na yote hayo, akipita tasbihi, anasabihi, na kadhalika mpaka tukamaliza swala na maswahaba wengi hivi ndivyo wakifahamu na kuizingatia, mmoja ni AbdulRaman anasema, wenzetu wakisoma Qur’aan kwa Mtume baadae wakaendea wenzao, basi wale wenzao wakichukuwa Aya kumi kumi wakienda nazo, baada ya kufahamu na kuzingatia wakija wakijiongezea nyingine

Kusujudu kwa sababu ya kusoma Qur’an

Msomaji akipitia sehemu ya sijda, ni muhimu asujudu. Na wamekhitalifiana wanavyuoni kuhusu jambo hili, Abu Hanifa amesema ni wajibu kusujudu, ama kauli yenye nguvu ni kauli ya ‘Umar Ibnu Khatwab, kwamba kusujudu ni sunna na hivyo ndio kauli ya wanavyuoni wengi. Msomaji awe katika hali ya adabu, inafaa asome akiwa amekaa, amesimama, au akitembea na kadhalika. Kama Allah (Subhaanahu wa Taala) anavyosema:

قال تعالى: (الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَى جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ) [آل عمران: 191]

{{Waja wema wanamtaja Mwenyezi Mungu ikiwa wamesimama au wamekaa au wamelala}}. Lakini vizuri zaidi ni mtu akae kisawasasa kikao cha heshima, kama Mtume alivyokua akikaa na akielekea kibla, akisoma baada ya swalatul Fajri mpaka jua kuchomoza, na asikae sana, isipite siku tatu pasina kusoma Qur’an,

Kutahadharisha Kusahau Qur’an

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, watu wameshughulika na dunia wakasahau kusoma Qur’an, na watoto wameshughulika na masomo ya kilimwengu mpaka hawana wakati wa kutosha na walimu hawashughulikiwi ikapelekea wasifanye kazi yao vizuri. Yote hayo, yamefanya Qur’an kuwa kitu kigeni, dhaifu na hata wasomao Dini wanapata shahada nzuri nzuri, hawasomi Qur’aan kisawasawa imepelekea kuipa mgongo Qur’an. Tumekua wajinga na hata katika mambo ya kidini tunaongozwa na wajinga hii ndio hasara, hatuipi kipaombele Qur’an. Hali hii itafanya Qur’an itushitaki kesho akhera ikisema: “ Ewe Mola hawa waja wako duniani walinitupa na wakanidharau, walikuwa hawanisomi, hawanifikirii na hawanizingatii, Wala hawanitumii katika maamrisho wala makatazo, bali wao wakishughulikia machezo, nyimbo na maneno ya upuzi.

Hatuna budi tupate Walimu Wazuri

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu hatuna budi mpaka tupate walimu wazuri, wa kutusomeshea watoto, sio kila mtu au mtoto apate msahafu ajisomee mwenyewe mpaka Mwalimu amsikilize kwani maandishi peke yake hayatoshi, tupate utatuzi wa kuwaweka walimu wa kisawa na utatuzi wa matatizo ya wanafunzi, na mipangilio ya masomo yao, bali ziko madrasa nyingi kubwa kwa ndogo, vichochoroni na upenuni, kumbi na vyumba, vyote havina matokeo mazuri, tunachekwa na dini nyinginezo, walimu na wanafunzi na majengo, yapo katika hali ya kudharauliwa, sababu hatuna mwelekeo, lakini lau tungekuwa na wasimamizi wa mijini, mashambani tungepata matokeo mema.

Tuhifadhi Kitabu Kitukufu

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, Tujifundishe na tukihifadhi kitabu chake, tukisomeni kwa kumuogopa Allah. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Mwenye kusoma herufi moja ana thawabu kumi, na utahesabiwa harufu moja moja]. Amesema ibnu-ll-Qayyim: ‘ Hebu zingatia, Allah ni mfalme wa wafalme, Atubembeleza tujipatie thawabu nyingi, Atutie moyo tupate thawabu hizo kwa urahisi, na ametunasihi saana, hii neema ya uhai isitupotee, vile vile ametuahidi raha kubwa kwa kumtii, na Ametuonya adhabu kali kwa kumuasi, na waja wema, inawapeleka kwenye wema ni kumtaja Allah kwa wingi kuwa ni Nuru, ni dawa, ni uongofu ni upambanuzi na ni hoja.

Mwisho

Mwenyezi Mungu alituumba kwa lengo la kiibada, kisha akatutumia Mtume akatufundisha vile atakavyo Yeye Mola, lakini Mungu huyo hatumuoni wala hatumsikii sauti, na tunaona dalili zake, alama zake na miujiza yake, kama mbingu na ardhi usiku na mchana na maneno yake matukufu. Mwenye kuyasoma atapata thawabu nyingi kwa kila herufi moja thawabu kumi na faida tofauti tofauti utazipata utakapoisoma Qur’an.

Nyoyo zetu na akili zetu zimejaa mashughuli ya kilimwengu hata hatuna nafasi ya kusoma Qur’an. Kwa hivyo ni kuangalia akhera yetu tupate taqwa, na tufuate utaratibu wa kuisoma. Tuisome tuijuwe maana huenda Qur-an ikarudi kwenye vifua vyetu na mienendo yetu.

Ewe Mwenyezi Mungu, Tujaalie waja wema, tuisome Qur’an kama maswahaba, tuisome na kuifahamu, tuisome kwa nidhamu, adabu na kuiheshimu.





Vitambulisho:




UKWELI WA UTUME NA UJUMBE WAKE