IDUL-ADH’HA


3657
wasifu
Idul- Ad’ha ni Idi ya kuchinja, ni Idi ya ukarimu, kuwahurumia Maskini, ni Idi ambao mamilioni ya Waislamu wanakusanyika kutekeleza matendo ya dini muhimu zaidi nayo ni Hija. Na katika Idi ya Ad’ha unaonekana ukarimu wa wa wakrimu, kwani kunafanyika hapo kuchinja ili kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (SW) na kuwapa mafukara na maskini.

Idul Adhaha (Iddi ya kuchinja) ni mojawapo ya idd mbili katika Uislamu na inakuwa tarehe kumi Dhulhijaa baada ya kusimama Arafa sehemu ambayo wamesimama mahujaj katika kutekeleza Hijja, na kwisha Iddi hiyo tarehe 13 Dhulhija. Iddi hiyo ni kukumbuka kisa cha Nabii Ibrahim alipotaka kumchinja mwanawe Ismail kwa ajili hiyo wanasimama Waislamu kuchinja wanyama.

Hekima ya Swala ya Iddi

Imeshurutishwa swala ya Iddi ili kuzishukuru neema za Mwenyezi Mungu na kushibisha matamanio ya binadamu.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى : (فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا فِطْرَةَ اللَّهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّهِ)

{{Basi elekeze uso wako katika Dini iliyo sawa sawa, ndilo umbile Mwenyezi Mungu Alilowaumbia watu (yaani Dini hii ya kislamu inawafikiana barabara na umbo la binadamu) hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vya Mwenyezi Mungu}}.

Iddi ni Mkusanyiko wa Mambo Manne;

Kukusanyika kwa watu.

Kukusanyika kwa sehemu.

Kukusanyika kwa wakati.

Kukusanyika kwa ibada maalum.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى : (وَلِكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنْسَكًا لِيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَى مَا رَزَقَهُمْ مِنْ بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ فَإِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ ) [الحج: 34] {{Na kila umma tumewafanyia mahali pa kuchinja, mihanga ya Ibada ili kulitaja jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile alivyowaruzuku katika wanyama hao wenye miguu mine. Basi Mungu wenu ni Mungu mmoja tu; Jinyenyekesheni kwake. Na wape khabari njema wale wanyenyekevu}}.

Imepokewa na Anas kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipokwenda Madina aliwakuta watu wa Madina wana siku mbili wanacheza, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akawaambia Mwenyezi Mungu amekubadilishieni siku mbili hizi kwa iddul Adha (kuchinja) na Iddul-fitr (baada ya Ramadhani). Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قوله تعالى : (فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ) [الكوثر: 2]

{{Basi Sali kwa ajili ya Mola wako na uchinje kwa ajili ya mola wako}}.

Hukumu ya Kuchinja katika Siku ya Iddi Pamoja na Sharti Zake na Namna ya Kuchinja.

Amesema Ibnu ‘Umar “Kuchinja ni sunnah”. Amesema Imam Sha’abi: “Haruhusiwi mtu kuacha kuchinja isipokuwa kwa mwenye kuhiji na kusafiri”. Imepokewa na Ibnu Majah kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ameamrisha kugawanya nyama ya Udhiya mara tatu akisema kuleni, toeni sadaka na muhifadhi.

Kushurutishwa Kupiga Takbira pamoja na Hukumu Zake na Namna yake

Imepokewa na Ibnu Abbas amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) hakuna siku kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, wala siku zinazopendekezwa kwake amali kama siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhulhija, zidisheni Tasbihi na Takbiri na Tahlil (Lailaha ila Allah).

Kutembelea Jamii na kutumia Wakati kwa Michezo na Furaha

Amesema ‘Aisha kuwa wahabesha ( watu wa Ethiopia) wanachezea siku ya Iddi, akaniita Mtume wa Mwenyezi Mungu na nikawa nawaangalia kupitia mabega ya Mtume, akaja Abubakar. Mtume akamwambia Abubakar amuwache kwani kila jamii wana Iddi yao. Ni makosa wanawake kudhihrisha mapambo yao na kujirembesha. Kunazidi kujirembesha kwa wanawake katika siku ya Iddi na hivyo ni kinyume ya sheria.

Katazo la kupigana na kuoneshana Silaha katika Siku ya Iddi

Imepokewa na Abu Huraira Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema atakayebeba silaha si katika sisi ( kwa Waislamu). Amesema Hasan Al-Basri: kumekatazwa kubeba silaha katika siku ya Idd isipokuwa kwa atakayetishiwa na adui.

Kukutana Siku ya Iddi na Ijumaa

Imepokewa na Abu Huraira Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema “Imekutana kwenu nyinyi Idd mbili atakayetaka hatoswali ijumaa, lakini mimi nitaswali Idd na Ijumaa (haimanishi kupomoka swala ya adhuhiri).

Kuombea Dua za Kheri Siku ya Iddi

Amesema Adham kijakazi wa Umar ibn Abdul Aziz “Tulikuwa tukimwambia ‘Umar Ibn ‘Abdul ‘Aziz siku za Idd mbili: Mwenyezi Mungu Atukubalie sisi amali zetu na alikuwa akitujibu”

Mwisho

Ndugu Waislamu, siku ya Iddi ni siku muhimu katika maisha ya Muislamu kwa kufanya mambo ya kheri na kujikurubisha kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Siku hii si siku ya kufanya machafu na kumkasirisha Allah (Subhaanahu wa Taala). Kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na Masahaba wake. Ni jukumu la kila Mzazi kuwafundisha familia yake hukumu ya siku hii muhimu katika Dini ya kislamu, ili jamii ya kiislamu iweze kujiepusha na mambo ya upuzi katika siku hii.

Tumuombe Mwenyezi Mungu Atupe baraka na kutusamehe madhambi yetu na kutupa mazuri hapa duniani na kesho akhera.





Vitambulisho:




Muhammad …Mtume wa Mwisho.