KUHIMIZA CHUMO LA HALALI NA KUEPUKA HARAMU


4040
wasifu

Kutafuta halali na kuhakikisha kuipata ni jambo la wajibu na lazima. Nyayo za mja Siku ya Kiyama hazitaondoke pale ziliopo mpaka aulizwe kuhusu mali yake vile alivyoyachuma na vile alivyoyatumia. Ni haki ya kila Muislamu mwanamume na mwanamke ajibidiishe kuchuma mali mazuri na kufanya kazi isiyo na dosari ili ale halali na ayatumie katika halali na ajiepushe na kula haramu na kila chenye wasiwasi kuwa ni cha haramu, kwani kila mwili uliojengeka kutokana na haramu , basi Moto unamfaa zaidi

Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, hakika Allah ametuneemesha neema nyingi zisizo na idadi kama; neema ya afya, macho, masikio na n.k. Na neema kubwa kushinda neema zote ni neema ya Uislamu. Neema hii Allah (Subhaanahu wa Taala) anachagua katika waja wake wale ambao watapata hidaya yake na kuwa Waislamu. Ndugu katika imani, ni nani katika sisi ambaye hataki kuishi maisha mazuri hapa duniani na kesho akhera. Nani katika sisi ambaye hataki kuwa na afya njema yeye na familia yake?. Yote hayo yanapatikana katika kuchuma halali.

Ndugu Muislamu, ukitaka afya njema na maisha mazuri hapa duniani na kesho akhera, jitahidi kutafuta riziki ya halali, ndio ufunguo wa kila kheri. Hakika Mwenyezi Mungu Ametuhalalishia vitu vingi vizuri, na Akatuharimishia vitu vichache viovu. Kila kitu ambacho kina manufaa kwa mwanadamu Allah kahalalisha na kila kitu ambacho kina madhara kwa mwanadamu, Allah kaharimisha. Ndugu Waislamu, hiyo ndio rehema ya Allah kwa waja wake baada ya kutuongoza katika Uislamu kisha aliwafundisha kila kitu ambacho mwanadamu anahitaji katika maisha yake, na akawatahadharisha na kila kitu ambacho kinadhuru maisha ya mwanadamu.

Fadhila za Kuchuma Mali ya Halali

Ndugu Waislamu, Dini ya Kiislamu imeamrisha kuchuma halali na kuishi maisha mazuri. Imeamrisha watu kufanya kazi ya halali kwa bidii, kwa lengo la kujisaidia katika maisha. Na imekataza watu kuwa wavivu na kuomba omba njiani. Qur’an na Hadithi zimeweka wazi umuhimu wa kutafuta riziki na fadhila za kuchuma halali. Miongoni mwa fadhila za kuchuma halali:-

Kuchuma halali na kula chakula cha halali ni njia ya Mitume. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا( [المؤمنون: 51] {{Enyi Mitume Kuleni vyakula vizuri na fanyeni mema. Hakika mimi ni Mjuzi wa yote mnayoyatenda}}. Na amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hajakula mtu chakula kizuri kuliko chakula alicho kichuma kwa mikono yake, na Mtume Dawud alikuwa akila chakula kilicho chumwa na mikono yake].

Kutafuta chakula cha halali imeshikamanishwa na kwenda jihadi. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى (وَآَخَرُونَ يَضْرِبُونَ فِي الْأَرْضِ يَبْتَغُونَ مِنْ فَضْلِ اللَّهِ وَآَخَرُونَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ( [المزمل: 20] {{Na wengine watasafiri katka ardhi wakitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu, na wengine watapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu}}.

Kuamrishwa kutafuta riziki ya halali baada ya kutekeleza ibada tukufu ya Swala. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانْتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِنْ فَضْلِ اللَّهِ) [الجمعة: 10]

{{Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika ardhi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu}}.

Kuchuma halali na kula chakula cha halali ni sababu ya Allah (Subhaanahu wa Taala) kukubali dua zetu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Enyi watu, hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri, na hakubali ila kitu kizuri. Kisha akataja mfano wa mtu anaye safiri safari ndefu hali akiwa amechoka, nywele zake zimejaa vumbi, anainuwa mikono yake kuelekeza mbinguni huku akisema: Ewe Mola wangu, Ewe Mola wangu, na hali kwamba chakula chake ni cha haramu, Kinywaji chake cha haramu na mavazi yake ni ya haramu. Vipi Allah ataikubali Dua yake ].

Athari ya kuchuma Chakula cha haramu

Ndugu katika imani, Hakika kuchuma haramu na chakula cha haramu kina athari mbaya kwa mwenye kuchuma na kadhalika kwa jamii nzima. Miongoni mwa athari hizo ni:-

Kukosekana baraka na kuzidi ukame katika ardhi

Kuzidi magonjwa

Kuenea machafu katika ardhi

Dhulma na udhalimu kuzidi katika ardhi. Mfano wa watu kula mali kwa njia ya dhulma kama; kula Riba, kunyang’anya, kudanganya, kula Rushwa, na n.k.

Kupungua nafasi za kazi na kuzidi uhaba wa kazi

Dua kutokubaliwa

Ndugu Waislamu, mtu hawezi kuendelea katika maisha yake akiwa anachuma haramu. Vilivile, jamii haiwezi kuendelea ikiwa watu wake wanakula haramu. Leo watu hawachagui baina ya halali na haramu. Mtu hajali kula haramu na kulisha watu wake haramu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Itawafikia watu wakati, mtu hatojali kula haramu]. Enyi Waislamu, tujihadharini sana na kula haramu. Na tujuwe wazi ya kuwa Allah (Subhaanahu wa Taala) Atatuliza siku ya akhera kila tulicho kichuma hapa duniani. Je ulichuma kwa njia gani? Njia ya halali au ya haramu?. Tuandae jibu la kumjibu mola wetu siku hiyo nzito.

Mifano ya Watu Wema katika kujiepusha na Haramu:

Swahaba Abubakar Siddiq aliletewa kitu na mfanyakazi wake. Abubakar akala, baada ya kula, yule mfanya kazi akamuliza Abubakar: Je wajua nimekipata wapi? Akasema Abubakar sijui. Akamuambia hicho kitu nilimdaganya mtu siku za jahalia (zama za ujinga) nilimfanyia uganga. Kisha akanipa hicho kitu ulicho kula kama zawadi. Abubakar akaingiza mkono wake mdomoni na akajitapisha na akatapika vyote vilivyokuwa tumboni.

Swahaba ‘Umar Bin Khattab alikunywa maziwa, kisha akamuuliza yule aliyemletea maziwa: Je umepata wapi maziwa haya? Akamuambia nimechukuwa maziwa hayo kutoka kwa ngamia wa Sadaka katika Baitul maal. ‘Umar akaingiza mkono wake mdomoni na akajichapisha maziwa aliyokunywa.

Mmoja katika wanawake wema alimuusia mumewe kwa kumuambia: Ewe mume wangu mche Mwenyezi Mungu, hakika sisi tunaweza kuvumilia njaa, lakini hatuwezi kuvumilia ukali wa moto wa jahannam.

Ndugu Muislamu, hivi ndivyo walivyo kuwa watu wema wakishi, na ndio siri kubwa ya kufaulu kwao nayo ni kwa ajili ya kujiepusha na haramu. Kwa hivyo, ni jukumu letu sisi Waislamu kujiepusha na haramu na kujifananisha na watu wema. Kufanya hivyo ndio kufaulu kukubwa hapa ulimwenguni na kesho akhera.

Ndugu katika imani, nawausieni na kujiusia nafsi kumcha Mwenyezi Mungu, na kufanya bidii kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake. Hakika jambo muhimu la Muislamu kujiepusha nalo ni kufuata matamanio ya kilimwengu, na kuwa hamu yake yote ni kupata ulimwengu, na akasahau akhera. Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anatufundisha ya kuwa dunia ni shamba la akhera. Muislamu akifanya bidii hapa duniani na kulima mazao mazuri, basi kesho atavuna mavuno mazuri.

Mambo yanayo sababisha kuchuma haramu

Kupenda ulimwengu na kuathirika na maisha ya ulimwengu na kusahau akhera. Amesema ‘Abdillahi Ibnu ‘Umar: ‘ Ishi katika dunia kama mgeni au mpita njia’

Kufuata matamino na hawaa ya nafsi. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hatakuwa muumini mmoja wenu mpaka matamanio yake yafuatane sawa na niliyokuja nayo].

Kupenda kukusanya mali nyingi, mpaka mtu kumsahau muumba wake na kufanya mali ndio muumba wake. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Ameangamia mwenye kuabudu Dinari na Dirham].

Mwisho

Ndugu Muislamu, Ukitaka kheri na baraka katika maisha yako basi chuma mali ya halali, Mwenyezi Mungu Atakubariki katika mali yako na watoto wako na mambo yako yote. Hakika wale wanao chuma haramu na kula haramu wamo katika khatari kubwa hapa ulimwenguni kwa kuishi maisha ya dhiki na mwisho mbaya wakiondoka duniani. Vilevile, siku ya kiama watapata khasara kubwa nayo ni kukasirikiwa na Mola wao (Subhaanahu wa Taala). Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri na hakubali isipokuwa mazuri]. Ikiwa mtu anakula haramu na kuchuma maali ya haramu, kwa hakika huyo atakuwa mbali na rehma ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Ndugu Waislamu, Tujiepusheni na chakula cha haramu, mali ya haramu kama kula maali ya Riba, kudhulumu watu katika biashara, kula mali ya mayatima na n.k. Tunamuomba Allah Atuepushe na mali ya haramu, Atuwezeshe kutafuta riziki ya halali, tutosheke na kichache cha halali, na Atuhifadhi sisi na watu wetu na kila njia ya haramu.





Vitambulisho:




Ali Hajjaj Souissi