KUJILAZIMISHA NA SUNNA YA MTUME (S.A.W)


3994
wasifu
Siku ya Ijumaa, siku bora kabisa iliyotokewa na jua. Katikas siku hii Mwenyezimngu Alimuumba Adam, Kiyama kitasimama na ni siku ya Idi kwa Waislamu. Kwa hivyo, yameamrishwa baadhi ya mambo, miongoni mwao: hutuba ya Ijymaa,kuoga, kujitia manukato, kwenda Ijumaa kwa kuvaa vazi zuri zaidi nap ambo zuri zaidi, kwenda Ijumaa mapema, kukaa karibu na imamu na kuutayarisha moyo kusikiliza mawaidha na utajo wa Mwenyezi Mngu.

Shukrani za dhati ni za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Bwana wa viumbe vyote. Na rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad. Ama baada ya hayo, Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, Maswali yafuatayo yafaa tujiulize:

Ni nani kati yetu ambaye hapendi apendwe na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)?

Ni nani kati yetu ambaye hampendi Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)?

Ni nani kati yetu ambaye hatarajii kuwa pamoja na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)?

Ni nani kati yetu ambaye hatarajii maombezi ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)?

Jawabu ni kuwa hakuna mtu asiyetaka yote tuliyoyataja. Na njia ya pekee ya kutufikisha kumpenda yeye ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na miongoni mwa alama za mapenzi ya kweli ya kumpenda Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ni kumtii na kufuata Sunna zake. Mola (Subhaanahu wa Taala) amesema:

قال تعالى) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ فَإِنْ تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ) [النساء: 59]

{{Enyi mlioamini, Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume wake na viongozi wenu na mukizozana katika jambo lolote liregesheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake}}.

Pia amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى ): قُلْ أَطِيعُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَإِنْ تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ) [آل عمران: 32]

{{Sema mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume na mukienda kinyume na hivyo basi Mwenyezi Mungu hawapendi wakanushaji}}.

Katika aya nyingine Amesema tena Mola: (Subhaanahu wa Taala):

وقال) : مَنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ وَمَنْ تَوَلَّى فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا) [النساء: 80]

{{Atakaye mtii Mtume basi amemtii Mwenyezi Mungu na atakaye kwenda kinyume basi hatukukufanya wewe kuwa ni mtunzi wao}}. Na ziko Aya nyingi zenye maana kama haya lakini tulizozitaja zinatosha.

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), alituhimiza sana kumtii yeye katika hadithi nyingi sana. Miongoni mwa hadithi hizo; Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema : [ Nawausia uchaji Mwenyezi Mungu na kusikiliza na kutii na hata akiwa kiongozi wenu ni mtumwa. Na atakayeishi katika nyinyi ataona tofauti nyingi, basi shikamaneni na Sunna yangu na Sunna ya makhalifa wema waongofu, ishikeni kwa magego].

Pia Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema tena: [Umma wote utaingia peponi isipokuwa atakayekataa kuingia peponi. Maswahaba wakamuuliza: Ni nani atakayekataa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : Atakaye nitii mimi ataingia peponi na atakayeniasi basi atakuwa amekataa].

Katika maneno ya maswahaba juu ya kushikamana na Sunna. Amesema Ibn Khatwab alipokuwa akilibusu Hajar Aswad (jiwe jeusi): “Hakika mimi najua wewe ni jiwe hunufaishi wala hudhuru, na lau nisingelimuona Mtume akikubusu basi nisingelikubusu.”

Ndugu katika imani! Ningependa kuchukua fursa hii adhimu kuwatajia faida anazopata Muislamu endapo atashikamana na Sunna za Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Na miongoni mwa faida hizo;

Kushikamana na Sunna ni kinga na hifadhi ya Waislamu wasifarikiane kwani ndiyo ambayo huleta mshikamano baina ya waumini na kuwa watu hawafarakani madamu watashikamana kwao na Sunna ya Bwana Mtume rehma na amani zimfikie.

Faida ya pili ya kushikamana na sunna ni kuokoka na kipote kipotofu kitakacho kwenda motoni. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Jua ya kwamba waliokuwa kabla yenu waliopewa kitabu waligawanyika mapote sabini na mbili, na umma huu utagawanyika vipote sabini na tatu, vipote sabini na mbili vitaenda motoni na kimoja pekee ndicho kitakachoenda peponi nacho ni kinachoshikamana na Sunna].

Faida nyengine ya kushikamana na Sunna ni kupata uongofu na kusalimika na upotofu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Enyi watu, hakika mimi nimewaachia kitu mutakaposhikamana nacho hamtapotea milele: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu]. Kwani kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) vinamuongoza aliyeshikamana navyo.

Miongoni mwa faida za kushikamana na sunna ni kwamba mtu atakaposhikamana na Sunna ataingia katika kundi la Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Anahadithia Anas Ibn Malik Mwenyezi Mungu awe radhi naye, ya kwamba walikuja watu watatu katika nyumba za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Wakaulizia ibada ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Wakaelezewa ibada yake basi waliiona kidogo sana. Wa kwanza akasema: Mimi nitaswali usiku kucha milele wala sitolala. Wa pili akasema : Mimi nitafunga siku zote na wala sitokula hata siku moja. Wa tatu akasema: Mimi nitajiepusha na wanawake milele sitaoa. Alipokuja Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akaelezewa kuhusu maswahaba wale akawaambia: [ Nyinyi ndio mliosema hivi na hivi na hivi? Ama mimi naapa kwa Mwenyezi Mungu ya kwamba mimi ni mchaji Mwenyezi Mungu zaidi pamoja na hivyo, mimi naswali usiku nalala nafunga na siku nyingine nala na vile vile naoa wanawake. Basi anayejiepusha na mwenendo wangu si katika mimi]. Na kujiepusha na Sunna ya Mtume inaweza kuwa maasi au ni ukafiri, tunamuomba Mwenyezi Mungu atulinde na ukafiri. Na mtu atakapoacha Sunna kwa kuipuuza na kuipinga na kuikosoa atakuwa ameikosoa Dini na kuikosoa Dini ni katika sampuli za ukafiri.Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na ukafiri.

Na endapo mtu ataacha Sunna kwa uvivu, sio kwa njia ya kuikosoa basi ni kulingamana na Sunna yenyewe, ikiwa ni jambo la wajibu, atapata dhambi kwa kuacha wajibu na akiacha lililopendekezwa atakuwa amepitwa na fadhila kubwa kabisa.

Faida za Kushikamana na Sunna.

Shukrani zote zamstahiki Allah (Subhaanahu wa Taala) Mola wa viumbe wote. Na rehma na amani tunumuombea kipenzi chetu Mtume Muhammad mbora wa viumbe vyote.

Nikiendelea kuzitaja faida za kushikamana na Sunna;

1. Ni kuepukana na njia za shetani. Katika hadithi, swahaba Ibn Mas’uud, Mwenyezi Mungu amuwie radhi, amesema: “Alituchorea Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) msitari mmoja kisha akasema hii ndio njia ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kisha akachora vijisitari kuliani mwa msitari, ule na kushotoni kisha akasema huu msitari mmoja ni njia yangu na vijisitari hivi katika kila kijisitari kuna sheitani awalingania watu kwenye njia ya motoni na upotofu. Kisha akasoma Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Aya hii:

قال تعالى) : وَأَنَّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَنْ سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُمْ بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ) [الأنعام: 153]

.

{{Na hii ndio njia yangu iliyonyooka ifuateni, wala msifuate vijinjia mtapotea na njia yake Mwenyezi Mung}}.

2. Miongoni mwa faida za kushikamana na Sunna ni kuitekeleza sheria na dini ya Mwenyezi Mungu, kwani Sunna humfanya Muislamu kutekeleza sheria bila ya kupunguza wala kuzidisha. Hii ni kuonesha kuwa sunna imekusanya dini yote.

3. Ni katika faida za kushikamana na Sunna kuondosha udhalili na unyonge kwa mtu, kwani udhalili na madhila wanayoyapata Waislamu popote walipo ni kwa sababu ya kuacha kwao Sunna ya Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

4. Miongoni mwa faida za vile vile ni kwamba katika Sunna kumetajwa ugonjwa na dawa pale Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipotaja ugonjwa wa kutofautiana Waislamu kisha akataja dawa yake ambayo ni kushikamana na Sunna yake na Sunna ya makhalifu wema waongofu.

5. Miongoni mwa faida ya kushikamana na sunna ni kupambika mtu na tabia njema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Hakika nimetumilizwa kukamilisha tabia njema]. Amesema Ibn Abdulbar: Hadith hii ameizungumza Madina na ni sahihi na ina maana ya kutengenea na kheri zote dini na dunia - ubora, utu, wema nadhifu- ni katika tabia njema za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Na kwa haya yote ametumilizwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ayatimize.

Mwisho

Nikimalizia kutaja faida za kushikamana na Sunna ni kuokoka na misukosuko na adhabu kali. Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال تعالى) : فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَنْ تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ) [النور: 63]

{{Na watahadhari wanaokwenda kinyume na amri ya Mtume, isije ikawapata wao misukosuko, au wapate adhabu inayoumiza}}. Mwisho kabisa nawausia ndugu zangu kushikamana na Sunna ya Bwana Mtume na huko ndio kutengea nafsi na kutengenea nafsi yako ni kutengenea familia, na kutengenea familia ni kutengenea jamii na kutengenea kwa jamii ni kutengenea kwa ujumla.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Atuongoze katika njia ya sawa na atujaaliye ni wenye kushikamana na Sunna mpaka mwisho wa uhai wetu.





Vitambulisho: