KUMTAJA MWENYEZI MUNGU (S.W)


5457
wasifu
Utajo wa Mwenyezi Mungu kwa kiwiliwili ni kama maji kwa samaki. Samaki huwa vipi akiwa nje ya maji? Dini Ya mila iliyolingana sawa umemuhimiza Muislamu afungamane na Mola wake, ili dhamiri yake iwe hai, nafsi yake isafishike, moyo wake utwahirike na ajipatie kutoka Kwake msaada na taufiki. Kwa hivyo yamekuja kwenye Teremsho la Qur'ani liliothibitishwa na Sunna ya Mtume iliyotakata yenye kuvutia kumtaja Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, kwa wingi katika kila hali, na kuwekea kila wakati na hali ya Utajo (wa Mwenyezi Mungu) wake.

Baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu wa Taala) na kumtakia rehema bwana Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Mola Mtakatifu kwa rehema yake Amewawekea waja wake kila njia za kusahilisha kufikia kwake. Mojawapo wa njia hizo ni dhikri. Dini ya Kislamu imewahimiza wafuasi wake kufanya bidii Kumtaja Mweyezi Mungu kwa kila hali. Kwasababu, Dhikri ni mawasiliano baina ya mja na Mola wake popote alipo, na ni silaha ya Muislamu wakati wakupambana na madui. Na vile vile, Dhikri ni kinga ya kumuhifadhi Muislamu na madui wote.

Kumtaja Allah ni Uhai wa Moyo na kusafishika kwake

Nawausia enyi watu na kujiusia nafsi yangu kumcha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kwa siri na kwa dhahiri, mumche, mumuabudu, mumsujudie na mfanye kheri kwa hakika mutafaulu.

Hakika nyoyo za binadamu wote ni kama viumbe vingine vyote, hayawani, mimea, na visivyokuwa na roho. Hayawani anahitajia vyakula, mimea inahitajia maji na hata chuma. Sheikhul-Islam Ibnu Taimiyya - Mungu Amrehemu- amesema: ‘Utajo wa Mungu kwa moyo ni kama maji kwa samaki, je huaje akitolewa majini?’

Uhusiano wa mja na mola wake ukiwa ni wakati wa asubuhi au jioni tu, basi mja huyo anafanya ghushi, lakini uhisiano wa maana wa mtu kuwa nao na mola wake ni kushikamana na maamrisho na kuepukana na makatazo. Na dhikri iwe ni yenye kumsaidia katika shida zake.

Fadhila za Dhikri na namna Uislamu ulivyohimiza

Dini ya kiislamu imehimiza sana uhusiano wa Muislamu na mola wake uwe imara. Na kuna dalili nyingi kuhusu jambo hilo. Miongoni mwa dalili hizo ni pale Allah (Subhaanahu wa Taala) aliposema katika mana ya Aya:

قال عز وجل) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اذْكُرُوا اللَّهَ ذِكْرًا كَثِيرًا 41وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا42) [الأحزاب: 42] {{Enyi mlioamini mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi na mumtakase asubuhi na jioni}}.

Na pale Aliposema katika maana ya Aya:

وقال سبحانه : (وَالذَّاكِرِينَ اللَّهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّهُ لَهُمْ مَغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ) [الأحزاب: 35]

{{Wenye kumtaja Mwenyezi Mungu sana waume na wake, Allah Amewaandalia msamaha na malipo makubwa}}.

Na aliposema katika maana ya Aya:

وقال تعالى : (فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ) [البقرة: 152] (وَلَذِكْرُ اللَّهِ أَكْبَرُ) [العنكبوت: 45] {{Nikumbukeni (kwa twaa na ibada), Nami nitawakumbuka (kwa rehema na msamaha)}. Na amesema katika maana ya Aya: {{Na hakika utajo wa Mwenyezi Mungu (dhikri Allah) ni mkubwa}}.

Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alitilia mkazo jambo hili kwa kusema katika maana ya hadithi: [Maneno mawili yanayopendekeza kwa Mola, mepesi katika ulimi, mazito katika mizani, nayo ni subhanaallah wabihamdihi, subhanaallahul adhiim]. Imepokewa na Bukhari na Muslim.

Na akasema katika maana ya hadithi: [Je siwapi habari za amali zenu bora na iliyotakasika zaidi mbele ya mfalme wenu na yenye kuinua daraja zenu zaidi na ni bora kwenu nyinyi kuliko dhahabu na pesa na bora kwenu nyinyi kuliko kupambana na adui na mkakata shingo na wakawakata. Wakasema: ni lipi hilo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: ni kumtaja Allah (Subhaanahu wa Taala)]. Imepokewa na Ahmad.

Na akasema katika maana ya hadithi: [Mwenye kusema, subhanallah wabihamdihi, hupandiwa mti wa mtende katika pepo]. Imepokewa na Haakim na Tirmidhi aliyehukumu kuwa ni hadithi hasan swahiih.

Enyi waja wa Allah kumtaja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) huondosha shida na balaa na hupamba ndimi za mwenye kumtaja kama yanavyo pambwa macho ya mwenye kuangalia kwa nuru. Ndimi zilizoghafilika ni kama jicho pofu, sikio ziwi na mkono ulio poza. Hasan al Basri amesema: ‘tafuteni utamu katika mambo matatu, katika swala na dhikri na kusoma Qur’an mkipata ni sawa na msipo pata basi mjue mlango umefungwa.

Kazi ya Dhikri katika kumsaidia Muumini kupambana na Shetani

Pindi binadamu anapofanya madhambi huwa si jambo jengine ila ni kughafilika na kumtaja Allah (Subhaanahu wa Taala), ndio mola akatuambia katika maana ya Aya:

قال تعالى) : وَمَنْ يَعْشُ عَنْ ذِكْرِ الرَّحْمَنِ نُقَيِّضْ لَهُ شَيْطَانًا فَهُوَ لَهُ قَرِينٌ) [الزخرف: 36]

{{Mwenye kughafilika na utajo wa Mwenyezi Mungu, tunamfanya shetani kuwa ndiye rafiki yake}}.

Na Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema katika maana ya Aya:

وقال تعالى) : (وَمَنْ أَعْرَضَ عَنْ ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنْكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَى) [طه: 124]

{{Na Mwenye kuupa mgongo utajo wangu hakika mtu huyo atakuwa na maisha ya dhiki na tutamfufua hali ya kuwa ni kipofu}}. Na Ibnul-Qayyim - Allah Amrehemu - alipokea kutoka kwa baadhi ya watu wema waliotangulia walisema: ‘Ukimakinika utajo wa Allah katika moyo wa binadamu, shetwani akimkaribia husongwa kama anavyosongwa binadamu na sheitwani, basi sheitani huyo aliosongwa hukusanyikiwa na mashetani wenzake na huku wakimuuliza “Ana nini huyu? Huwa kunajibiwa: “ Hakika shetani huyu amerogwa na binadamu.

Enyi Waislamu hii ndio kazi ya dhikri ambayo ni silaha ya Muumin ya kuweza kupambana na adui mkubwa wa binadamu.

Dhikri ni usaidizi wa Muumini katika mambo yake yote

Enyi waja wa Allah, kitu kitukufu zaidi chenye kupita akilini mwa binadamu, na twahara zaidi chenye kutamkwa na midomo ni dhikri ya Allah (Subhaanahu wa Taala). Na binaadamu wote kwa jumla huwa wana babaiko na maisha yao na hakuna jambo lolote lenye kuondosha babaiko ila dhikri ya Allah, ndio akatuamuru Allah na ndiye Mkweli kama ilivyo katika Aya ambayo mana yake:

قال تعالى : ((الَّذِينَ آَمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُمْ بِذِكْرِ اللَّهِ أَلَا بِذِكْرِ اللَّهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ) [الرعد: 28]

{{Walioamini nyoyo zao hutulia kwa utajo wa Mwenyezi Mungu, jueni na mtanabahi kwamba utajo wa Mwenyezi Mungu hutuliza nyoyo}}. licha ya hivyo hata kazi zako za kawaida, nyumbani, ofisini, sokoni huwa nyepesi kwa kumtaja Allah kwa dalili ya maneno ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipolalamikiwa na Sahaba Ali na binti yake Fatma kuhusu uzito anaopata Fatma katika kazi za nyumbani na huku wakitaraji bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) atawawekea mfanyakazi nyumbani, lakini Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akawaambia katika maana ya hadithi yake: [Je, niwaonyesheni jambo bora zaidi kuliko kuweka mfanyakazi nyumbani? mkifika kitandani mseme: “Subhanallah mara thalathini na tatu, Alhamdulillah mara thalathini na tatu, na Allahu Akbar mara thalathini na tatu hizi ni mia kwenye ulimi lakini ni elfu katika mizani].

Shida inayo wapata Watu Wenye kughafilika na Dhikri

Enyi waja wa Allah, tukipeleleza vyema tutaona kuwa wengi wanaokumbwa na shida za kila aina, magonjwa, kurogwa, na kukosa raha ya maisha utapata yote haya husababishwa na kuwa mbali na dhikri. Na huenda tukajiuliza kwanini watu hawaingii katika hifadhi ya Mola wao naye atawakinga kutokana na balaa zote? Kwani binadamu hajui kuwa kulala, kuamka na harakati zote ziko na dhikri, hata kulala na mkewe? ndio siri ya Allah (Subhaanahu wa Taala) kusema katika maana ya Aya:

قال تعالى) : وَاذْكُرُوا اللَّهَ كَثِيرًا لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ) [الجمعة: 10]

{{Na mumtaje Mwenyezi Mungu sana hakika mtafaulu}}.

Na binadamu yoyote namna atakavyo kuwa na nguvu, basi yeye ni dhaifu mbele ya mitihani ya Mungu, na huwa anamuhitaji Mola wake kama anavyohitaji maji na hewa.

Kumtaja Mwenyezi Mungu kwa Mazingatio

Ukiwa unamtaja Mungu kwa ulimi na unazingatia kwa moyo basi ni dalili ya mtu kuwa na imani. Neno la Allahu Akbar ndio kichwa cha kila nguzo na ndio jambo la kwanza alilokalifishwa nalo Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) pale alipoamrishwa kuwaonya watu, Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى : (يَاأَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ1 قُمْ فَأَنْذِرْ2 وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ3) [[المدثر1: 3].

{{Ewe uliyejifunika, inuka ukhofishe, na Mola wako umtukuze}]. Hakika (Allahu Akbar) ndio neno la kwanza ambalo huhuisha ardhi iliyokufa, na sauti yake inashinda ngurumo ya bahari iliyochafuka. Kwa hivyo, inapasa sauti yake isikilizwe katika sikio la kila mwenye kufikiria kufanya maovu.

Enyi Waislamu, mkumbukeni Allah kwa wingi hakika mtafaulu mkifanya hivyo. Ewe mwenye kughafilika, ukiona moyo wako hauko ujue kwamba kwa kumtaja Allah utahuika na utaimarika.

Kwa nini kuwe kumtaja Mungu ni Ibada yenye manufaa zaidi kuliko Ibada nyingine pamoja na wepesi wake iwapo Moyo wako haukughafilika?

Utakapouliza swali hilo, jawabu ni kwamba ibada zote zimewekewa kiwango na wakati isipokuwa dhikri haina kiwango wala wakati. Allah (Subhaanahu wa Taala) anatuambia:

قال تعالى) : وَاذْكُرْ رَبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآَصَالِ وَلَا تَكُنْ مِنَ الْغَافِلِينَ )[الأعراف: 205].

{{Mkumbuke mola katika nafsi yako kwa kunyenyekea pasina kudhihirisha neno, asubuhi na jioni, wala usiwe miongoni mwa wenye kughafilika}}.

Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ametujulisha silaha ya kujikinga na moto nayo ni [Al-Baaqiyaatu Swalihaatu (Visalio vyema) Subhanallah, Walhamdulillah, Wala Ilaaha Illa llah Allah Akbar]. Na kwa sababu ya kuwa mara nyingi moyo huamrisha maovu inatakikana kwa binadamu awe mara zote anamfikiria Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Tahadhari na Vikao vya Watu Walioghafilika

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ametahadharisha watu kuondoka katika kikao bila ya kumtaja Allah (Subhaanahu wa Taala) katika kikao hicho kwa neno lake: [Hakuna watu wowote watakaoinuka katika kikao wakawa hawakumtaja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika kikao hicho ila ni kama waliokalia mzoga wa punda, na watakuwa wamepata hasara]. Kwa ajili hiyo Mtume amevipinga vikao vya watu walioghafilika, na amekataza vikao vyote ambavyo havimtaji Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na vile vikao ambavyo vinawasahaulisha watu kumtaja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na vinavyowafanya watu kutumia muda mrefu katika mambo ya kipuuzi, hivi vyote ni vikao vya uvundo havina faida. Na ili mtu akikaa asipate hasara katika vikao vya aina hii, ni aseme anapoondoka katika vikao hivi, kwa kulingana na mafundisho ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) aliposema: “Yoyote atakaye kaa kwenye kikao, maneno ya kipuuuzi yakawa mengi, basi naye akasema kabla hajainuka katika kikao hicho, [Subhaanak Allahumma Wabihamdika Ash-hadu An-lailaaha illa Anta, Astagh-firuka wa Atubu ilaika], ila Mwenyezi Mungu humfutia makosa yaliyotokea katika kikao hicho”. Na Allah (Subhaanahu wa Taala) anatuambia :

قال تعالى ): يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا لَا تُلْهِكُمْ أَمْوَالُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ فَأُولَئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ) [المنافقون: 9]{{Enyi mlioamini yasiwapumbaze mali yenu na watoto wenu yakawafanya msikumkumbuke Mwenyezi Mungu, na mwenye kufanya hivyo atakuwa ni miongoni mwa waliopata hasara}}.

Mwisho

Tumeona namna ya Allah (Subhaanahu wa Taala) na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) wanavyotuhimiza kuleta dhikri na kuonyesha ya kuwa dhikri ndio njia ya kuondosha hamu na ghamu za binadamu, sio kutizama vipindi vya TV na sinema au kukaa vibarazani. Ndugu Waislamu, Tufanyeni bidii kumtaja Allah kama alivyo tufundisha Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).





Vitambulisho:




Hamkanushi isipokuwa ni Mpingaji