KUTUBIA KUTOKAMANA NA MAASIA


3158
wasifu
Likikusanyika ongo na uchafu kwenye nguo na uchache wa kuosha, kutakuwa na nini? Basi nyoyo ni kama hivyo. Dhambi zinapandana, dhambi juu ya dhambi zinakusanyika, pamoja na uchache wa kuomba msamaha na kutubia, Moyo huo utakuwa vipi? Muumini hakosi kuwa na maasia, na si sharti awe amehifadhika nayo. Lililo sharti kwake ni mwingi wa kutubia na kurejea kwa Mola wake. Na moyo unaotenda maasia bila kutubia ni kama nguo inayochafuka na isioshwe.Basi mwenye kutaka kutakasa moyo wake ajilazimisha na kutubia na kuomba msamaha na kurudi kwa Mola Mwenye kurehemu Mwingi wa kusamehe.

Kutubia kwa Mwenyezi Mungu ni jambo ambalo hatochoka nalo Muislamu, vipi na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikua akitubia kwa Mwenyezi Mungu kwa siku mara mia.

Ndugu zangu Waislamu wadhifa wa mwanadamu ni kufanya ibada ya Mwenyezi Mungu, ameumbwa kwa ajili ya hiyo ibada akifanya jema amejifanyia nafsi yake na ametekeleza wajibu wake, akifanya maasia basi ni upungufu katika kazi yake, na madhara inamrejea mwenyewe.

Je mnajua ndugu zangu Waislamu? Kwamba maasi ni uchafu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Mwenye kufanya uchafu huo basi ajistiri na stara ya Mwenyezi Mungu hata kama hatuoni uchafu huo wala hatusikii harufu ya uchafu huo katika moyo].

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى : (كَلَّا بَلْ رَانَ عَلَى قُلُوبِهِمْ مَا كَانُوا يَكْسِبُونَ) [المطففين: 14]

{{Sivyo hivyo, Bali yanatia kutu juu ya nyoyo zao maovu waliyokuwa wakiyachuma}}.

Na Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Mwanadamu akifanya dhambi huwa inaingia nukta nyeusi katika moyo wake, akitubia husafishwa dhambi hilo, na akizidisha huzidi weusi]. Madhambi ambayo yanakusanyika katika moyo bila ya toba hupandana na kuziba moyo. Ndugu zangu Waislamu, nguo ikizidi kuwa chafu bila ya kusafisha matokeo yake inakuaje? Moyo mfano wake ni huo.

Ndugu zanguni Waislamu tunafanya madhambi usiku na mchana bila ya kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha tunasubiri nini kutokana na moyo hoyo?

Ndugu zangu Waislamu, sote tunafanya madhambi, lakini kinacho tupambanua kati yetu kuna wanao tubia baada ya kufanya madhambi, na kuna wanao ghafilika kwa kutubia.

Umuhimu wa Toba katika Qur’an

Ndugu zangu Waislamu, mlango wa toba uko wazi, na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) anatuitia tutubie Akisema neno lake tukufu:

قال الله تعالى: (قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَى أَنْفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِنْ رَحْمَةِ اللَّهِ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ) [الزمر: 53]

{{Sema, Enyi waja wangu mliodhulumu nafsi zenu, Msikate tamaa na rehma ya Mwenyezi Mungu; bila shaka Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote; hakika yeye ni mwingi wa kurehemu}}.

Moja wapo ya majina ya Mwenyezi Mungu ni msamehevu, mwenye kukubali toba, Mwenyezi Mungu anakielezea kisa cha Musa alipomuua mtu bila ya kukusudia akisema:

قال الله تعالى): قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي فَاغْفِرْ لِي فَغَفَرَ لَهُ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ) [القصص: 16]

{{Akasema: Mola wangu, Bila shaka nimedhulumu nafsi yangu, basi nisamehe. Naye Mwenyezi Mungu akamsamehe. Kwa yakini yeye ni mwingi wa kusamehe na Mwingi wa rehema}}.

Mwenyezi Mungu Ametuhimiza na kusisitiza waja wake kurudi kwake kwa kuomba msamaha na maghfira.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقوله تعالى): يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَصُوحًا عَسَى رَبُّكُمْ أَنْ يُكَفِّرَ عَنْكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ) [التحريم: 8] {{Enyi mlioamini, tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli. Huenda Mola wenu akakufutieni maovu yenu}}.

Umuhimu wa Toba katika Sunna za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)

Amepokea Abi Musa ‘Abdallah bin Kais Asha’ari hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Mwenyezi Mungu hunyosha mikono yake ili atubiye aliyekosea wakati wa usiku, na hunyosha mkono wakati wa mchana ili atubiye aliyekosea wakati wa usiku].

Inapaswa kutubia kwa makosa yote, na ndio kufaulu, na kuchelewa kutubia ni uovu. Amepokea Abu Huraira hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [Mimi natubia kwa Mola wangu zaidi ya mara sabini]. Na amesema tena Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Enyi watu tubieni kwa Mwenyezi Mungu na muombe msamaha, mimi natubia kwa siku moja mara mia]. Mwenyezi Mungu ameamrisha waja wake watubie taubatu nasuha, Amesema Mwenyezi Mungu: “ Enyi mlioamini, tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli. Huenda Mola wenu akakufutieni maovu yenu”.

Masharti ya Tawbatu Nasuha:

Kujivua na dhambi.

Kujuta kwa kosa alilolifanya.

Kuazimia kutorudia tena kwa kosa lile.

Wamesema wanazuoni akirudia kosa la kwanza baada ya kutubia hamlazimu kutubia toba ya nasuha kwa mara ya pili. Na miongoni mwa masharti ya toba ni kurudisha haki ya mtu.

Hali ya Wenye Kutubia

Wenye kutubia leo wanaendelea kufanya makosa, na wakidai kutubia na wakitarajia mazuri mbele ya Mwenyezi Mungu na kutoogopa adhabu yake. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله) : أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّهِ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ) [الأعراف: 99]

{{Je, wameaminisha kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi adhabu ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye khasara}}.

Amesema Hassan Basri: “Muumini anafanya matendo mazuri na yeye anaogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu lakini mtu muovu anafanya maasi na anayo matarajio”

Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anawahimiza watu kuswali rakaa mbili anapotubia. Amesikiwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [ Mtu yoyote akifanya maasi na akatawadha kuswali rakaa mbili, isipokuwa Mwenyezi Mungu humsamehe mja huyo].

Na amesema tena Mtume wa Mwenyezi Mungu: [ Mtu yoyote anayetawadha na akakamilisha udhu wake na akasema nashuhudia kwamba hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wake, isipokuwa hufunguliwa milango ya pepo minane aingia atakao].

Toba haifai wakati mtu anapotolewa roho au jua linapotokea upande wa magharibi, anasema Mwenyezi Mungu:

Amepokea Abu Huraira hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [ Haisimami kiyama mpaka jua litoke upande wa magharibi]. Na amesema tena Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Anayetubia kabla ya jua kutoka upande wa magharibi, basi Mwenyezi Mungu hukubali toba yake].

Na amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Mwenyezi Mungu aliyetukuka hukubali toba ya mja kabla ya kukata roho.

Na amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّى إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآَنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ( [النساء: 18] {{Hawana toba yake ambao Hufanya maovu mpaka mauti yamewahudhuria mmoja wao akasema: Hakika mimi sasa na tubu}}. Hakubaliwi toba yake wakati wa kukata roho ikiwa hakuomba msamaha kabla ya hapo.

Faida ya Toba:-

Kupata msaada wa milele katika uhai wa dunia na kesho akhera, amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ) [النحل: 97]

{{Wafanyaji mema, wanaume na wanawake, hali yakuwa ni Waislamu, tutawahuisha maisha mema, na tutawapa ujira wao mkubwa Akhera. Kwasababu, ya yale mema walikuwa wakiyatenda}}.

Qur’an imetaja kuwa amali njema ni iliyokamilika mambo matatu nayo ni:-

Kuafikiana kwa yale alichokuja nacho Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (وَمَا آَتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانْتَهُوا( [الحشر: 7]

{{Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho}}.

Iwe kwa ajili yake Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ) [البينة: 5]

{{Wala hawakuamrishwa ila kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia dini, wawache dini za upotofu}}.

Iwe imejengwa na misingi ya akida, Amesema Mwenyezi Mungu:

قال تعالى) : مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنْثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ)

[النحل: 97] {{Wafanyaji mema, wanaume na wanawake, hali ya kuwa ni wenye imani}}. Kinyume chake, lau kama si muumini haitokubaliwa amali yake.

Kupata uongofu na amani kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى) : الَّذِينَ آَمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ أُولَئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُمْ مُهْتَدُونَ) [الأنعام: 82]

{{Hapana shaka kuwa wale walioamini na hawakuchanganya imani yao na ushirikina kuwa hao ndio watakao pata amani, nao ndio waliongoka}}.

Ubadilishaji wa maovu kwa amali njema, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قوله تعالى) : إِلَّا مَنْ تَابَ وَآَمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا) [الفرقان: 70] {{Ila Yule atayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri; basi ndio Mwenyezi Mungu atawabadilisha maovu yao kuwa mema}}.

Kufaulu kupata radhi zake Mwenyezi Mungu na kuokoka na moto. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قوله تعالى (وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَى مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ 135 أُولَئِكَ جَزَاؤُهُمْ مَغْفِرَةٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ) [آل عمران: 136]

{{Na ambao wanapofanya uchafu au kudhulumu nafsi zao, hukumbuka Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha kwa dhambi zao. Na nani anaye samehe dhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu? Na hawaendelei na maovu waliyoyafanya, hali wanajua. Hao ndio ambao malipo yao yatakuwa msamaha kwa Mola wao na Bustani zinazopita mito mbele yake, ambamo watakaa milele. Na ni wema ulioje ujira wa watendao mema}}. Maana yake, baada yakufanya madhambi wanaudi nyuma na kumkubuka Allah na kuaomba msamaha kwa madhambi waliyoyafanya.

Amepokea Abu Huraira hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akisema: [Kuna mtu amefanya madhambi, akasema Mola wangu nimefanya madhambi, basi nisamehe, akasema Mwenyezi Mungu mja wangu amefanya madhambi na akajua ana Mola ambae atakae msamehe makosa yake, basi nimemsamehe. Kisha akafanya dhambi tena na akaomba msamaha na Mwenyezi Mungu akamsamehe, kisha akafanya dhambi kwa mara ya tatu na kuomba msamaha akasema Mwenyezi Mungu mja wangu amejua ana Mola atakae msamehe, shuhudieni kuwa nimemsamehe na afanye atakavyo].

Mwisho

Ewe Mwenyezi Mungu, sisi ni waja wa kufanya madhambi, sisi ni waja wenye makosa mengi, sisi tumefanya madhambi yetu kwa siri, sisi ni waja wagonjwa kwa makosa tuliyofanya. Tumekuja tunataka toba yako. Sisi ni waja wako maskini tumenyoosha mikono yetu basi tusamehe madhambi yetu. Tunataraji kutoka kwako Mola wetu msamaha na maghfira.





Vitambulisho:




Maneno ya Mwenyezi Mungu.