MADAWA YA KULEVYA NA ATHARI YAKE KATIKA KUMUANGAMIZA BAROBARO


4075
wasifu
madawa ya kulevya limekuwa ni janga kubwa kwa jamii yetu,leo vijana wengi wakisalamu wamekosa mustaqbali wao kwa kutumi uraibu huu mbaya,unao angamiza vijana,na kuangamiza jamii kwa jumla,ni wajibu kwa kila muislamu kupambana na madawa kama haya ilikuifadhi jamii yetu na kila ovu linalo patikana na madawa kama haya.

Allah amemkirimu mwanaadamu kwa kumpa akili na fahamu na akamuelekeza kwa kufikiri na kuzingatia, akili ikawa ndio neema kubwa ya Allah kwa huyu mwanadamu, akili ndio inayotufahamisha baina ya mwanadamu, wanyama na visivyokuwa na roho. Enyi waja wa Allâh! Allâh Mtukufu amewakirimu wanadamu juu ya viumbe vyake vingi, akasema (Subhaanahu wa Taala):

فقال سبحانه : (وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آَدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُمْ مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى كَثِيرٍ مِمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا ) [الإسراء: 70]

{{Hakika Tumewatukuza wanaadamu, na Tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na Tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na Tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa Tuliowaumba}}. Allâh amewakirimu wanaadamu kwa mambo mengi aliyowapambanua na viumbe vingine vikiwemo, visivyo na roho, wanyama, mimea na majini, alimkirimu kwa akili na fahamu na akamuelekeza kwa mazingatio na kutafakari, kwa hivyo akili ikawa ndio neema kubwa zaidi kutoka kwa Allâh, kwayo, mwanadamu huweza kupambanua baina ya kheri na shari madhara na manufaa, kwayo huweza akafurahia maisha yake, kuendesha mambo yake na kustarehe, kwayo ndio umati zote ziweze kupanda na maisha kuendelea.

Akili ni johari yenye thamani, wenye akili huwa wakiihifadhi na kuihami kwa kuukubali ubora wake na kuhofu wasije wakaipoteza.

Mwanadamu anapoikosa akili yake basi hakuna atakayemtofautisha baina yake na wanyama, anayeikosa akili yake huwa hana manufaa bali huwa ni mzigo kwa familia na jamii yake. Akili hii ya thamani hupatikana kwa wanadamu kwa watu wasiyoiangalia kuitunza na kuihami. Bali katika watu, yuko anayeikanyaga akili chini ya nyayo zake akifuata matamanio yake na macho yake yakawa hayaoni, hata jambo hilo likawa wazi kabisa.

Mtu anapokunywa pombe au kutumia madawa ya kulevya au akanusa ulevi, basi hapo huanza kukosa akili akajiinua kutoka katika ulimwengu wa ubinadamu na akavaa nguo ya maovu na mauaji. Hapo mlevi huanza kupooza na akamsahau Mola wake, akaidhulumu nafsi yake, akaondokana na haya aliyokuwa nayo, watoto wake akawafanya mayatima na mkewe akawa mjane kwa sababu ya kukosa akili.

Hapo akawa amelitupa jambo la dharura maishani mwake katika yale mambo matano ambayo sheria za mbinguni zimeafikiana kwamba ni wajibu mtu kuyahifadhi mambo hayo, nayo ni akili, ni wajibu mtu kuhifadhi akili na kuichunga, anayeikosa akili yake kwa kulewa, atakuwa ameikosa akili na jamii yake, na ataitumbukiza jamii yake na waumini wenziwe katika maporomoko ya udhalilifu na maangamizi, hapo amani ikakosekana na jamii ikatishia amani.

Watumiaji wa madawa ya kulevya hukosa kuyasimamia majukumu waliyonayo na kusimamia akili zao. Mamia ya Waislamu wamepotea kwa sababu ya madawa ya kulevya na ulevi. Roho zao zimeenda kwa Mola wao huku wakiwalalamikia wale mafasiki na waovu waliojiingiza wao wenyewe na kuwaingiza wengine katika maangamivu.

Haya madawa ya kulevya yamewapeleka watu waliokuwa na familia katika jela miaka mingi yakiwa ndio malipo ya yale makosa waliyoyateuwa familia zao zikabakia bila ya msimamizi, wake zao wakawa kama wajane, watoto wao kama mayatima, wakapoteza ubarobaro na maisha mazuri waliyokuwa nayo, mustakbali wao wakaupoteza kwa mitaimbo ya maadui zao jela zikawa zimejaa pomoni namna walivyokuwa wengi.

Wenye akili dhaifu huyapokea wanayoletewa na maadui na kuenezwa na madalali waovu.

Bila shaka ni misiba iliyowapata Waislamu, nao wameghafilika na mambo wanayopelekewa, maadui wamejua njia ya kuingia kwa Waislamu.

Allâh (Subhaanahu wa Taala) Amesema kweli wakati Alipotuambia:

قال سبحانه) وَلَا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّى يَرُدُّوكُمْ عَنْ دِينِكُمْ إِنِ اسْتَطَاعُوا) [البقرة: 217]

{{Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika Dini yenu kama wakiweza}}. Ajabu kubwa ni kwa yule anayenunua ufisadi kwa mali yake!

Kwa nini mtumiaji wa madawa ya kulevya hawezi kupata mawaidha kwa wale waliopata mikasa katika familia zao, ikawaangamiza kabisa, na ni vipi ajitoe katika kundi la watu wenye akili na heshima zao ajipeleke katika kikundi cha wendawazimu wasio na akili?. Al-Hassan Al-Basry Amesema: “Lau kama akili ingalikuwa inauzwa bila shaka ingekuwa ni ghali mno.”

Basi iweje tena mtu aiharibu akili yake yeye mwenyewe? Kwa hakika huu ni msiba uliowashukia watoto wa Kiislamu. Tunamuomba Allâh atuongoze. Kwa ajili hiyo, kutumia kila kinachoondoa akili au kuilewesha kwa kinywaji au chakula au kinginecho, inakuwa ni haramu.

Katika Qur’an Allâh (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قوله تعالى (يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنْصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ) [المائدة: 90] {{Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu}}.

Kwa mujibu wa Aya hii, pombe ni najisi, kwa sababu, Allâh Amesema: “rijs, ni uchafu” Katika maneno ya Waarabu, rijs ni kila kilicho kichafu kinachochukiwa na watu. Bali Maswahaba watukufu wamefahamu katika Aya hii kwamba pombe si kama imeharamishwa pekee, bali imelinganishwa na shaka ambayo ndio dhambi kubwa zaidi inayotendwa na mwanadamu.

‘Abdullah Bin ‘Abbas amesema: “Ilipoteremka Aya ya kuharamisha pombe, Maswahaba wa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) waliendeana wao kwa wao na wakaambizana kuwa: [Pombe imeharamishwa na imelinganishwa na shirki]. Hadithi hii imepokewa na Tabarany, wapokezi wake ni wapokezi wa Hadithi Sahihi.

Kwa sababu Allâh Amesema kuhusu pombe: ni rijs katika matendo ya shetani. Na akasema kuhusu shirki: “Basi jiepusheni na (rijs) uchafu wa masanamu”

Hadithi za Mtume na Aya za Qur’an zimetilia nguvu uharamu wa pombe na kutahadharisha, na kukemea kuinywa au kuikaribia, pombe ni alama ya upotevu na anuani ya machafu na maovu kama ilivyopokewa, katika Hadithi ya AbdulRahman Bin Wa’lah amesema: Nilimwuliza ‘Abdullahi Bin ‘Abbas kuhusu biashara ya pombe, akaniambia: [Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikuwa ana rafiki kutoka kabila la Thaqif au Daws, akakutana naye Siku ya Fat-hi Makka, akampa zawadi chombo kilichojaa pombe, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamwambia: “Ewe fulani kwani hujui kama Allâh Ameiharamisha?” Yule mtu akamwambia mtumishi wake: “Nenda ukaiuze”. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamwuliza: “Ewe fulani, umemuamrishwa nini?” Akajibu: “Nimemuamrishwa nikaiuze.” Akamwambia: “Aliyeiharamisha kunywewa ndiye Aliyeharamisha kuuzwa”. Akaamrisha, ikamiminwa mchangani]. Muslim.

Katika Hadithi ya Abu Huraira, amesimulia: Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Usiku niliopelekwa Israa, huko Eliya (Baitul-Maqdis) nililetewa vikombe viwili vya pombe na maziwa, nikavitazama, nikachukua maziwa. Jibril akasema: Namshukuru Allâh Aliyekuongoza kuchukua fitra (Uislamu), lau ungalichukua pombe, umati wako wangaliangamia]. (Bukhari).

Katika jumla ya Hadithi zinazoonyesha uharamu wa pombe, ni iliyopokewa kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Yoyote anayekunywa hatakubaliwa Swala yake kwa muda wa siku arubaini, na anayekufa ilihali katika kibofu chake cha mkojo ana sehemu katika pombe ataharamishiwa Pepo. Na iwapo atakufa katika siku arubaini (tangu anywe pombe hiyo), atakuwa amekufa kifo cha kijahiliya]. (Tabarani, ameipokea kwa isnadi yake ni sahihi).

Anayekunywa pombe duniani atanyimwa Akhera kama ilivyopokewa katika Hadith ya ‘Abdullah Bin ‘Umar kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [ Atakayekunywa pombe duniani na asitubie dhambi hiyo, atanyimwa pombe ya Akhera]. (Bukhari na Muslim)

Hadithi nyingine kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) inasema: [Allâh amewalaani watu kumi katika pombe:- mgemaji, anayetaka kugemewa, mnyweshaji, mnywaji, muuzaji, mnunuaji, mbebaji, mwenye kubebewa, mwenye kula thamani yake na mwenye kumnunulia mtu, wote hao wamelaaniwa kwa dua ya Muhammad].

Hikma ya Uislamu imepelekea kuharamisha uchache na wingi wa pombe na vilevi, kwa sababu uchache hupelekea katika wingi, halafu mazoea, kisha ikawa ndio uraibu. Jabir amesimulia kuwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Chochote kinacholewesha kwa wingi, na uchache wake pia ni haramu]. (Abu Dawud na an-Nasa-iy).

Katika mambo ambayo ni wajibu kuyahadharisha ni mti uliolaaniwa, nao ni mti wa bangi na aina nyingine ya miti ya motoni inayolevya inayoangamiza viwiliwili na akili za wanaotumia, ikawafanya wakose mizani na wawe dhaifu wa nguvu na azma, kutumia vichafu hivi huzima nuru ya macho na akili, humfanya mtu mbele ya watu kutokuwa na uadilifu na tabia mbaya. Hucheka na hulia bila sababu, macho humzunguka kama kwamba amefunikwa na mauti.

Maadui wa Uislamu wametengeneza aina nyingi ya madawa ya kulevya, wakatengeneza vidonge vinavyolevya vilivyochanganywa na heroin, haya ni matendo ya shetani, jiepusheni nayo ili mpate kufanikiwa.

Madhara ya kidini ya Madawa ya Kulevya na Ulevi

Enyi waja wa Allâh, madawa ya kulevya na ulevi, vitu hivyo vina madhara kwa upande wa dini. Allâh (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قوله تعالى) إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ فَهَلْ أَنْتُمْ مُنْتَهُونَ) [المائدة: 91] {{Hakika shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na awazuie kumkumbuka Allâh na kuswali. Basi je, mmeacha?}}.

Ulevi huwazuia watu kuswali ambapo Swala ni nguzo ya dini, huzuia kumtaja Allâh na kusuhubiana na Malaika kwa dalii ya Hadithi ya al-Bazzaar kutoka kwa ‘Abdullah Bin ‘Abbas: “Malaika hawamkaribia mlevi’’. Malaika wakiwa mbali naye, bila shaka mashetani watakuwa naye na yule shetani wake atazidi kufurahia. Kwa ajili hiyo mtumiaji yoyote wa madawa ya kulevya utamuona ni mzito kufanya ibada, moyo wake umeepushwa na mambo ya kheri na hupenda mambo ya haramu, kwa sababu moyo wake umejipa uchafu huu, ufuataji wa dini kwake huwa na mapungufu na hali yake daima ni ya kurudi nyuma.

Miongoni mwa Madhara ya kiafya yanayosababishwa na Madawa ya Kulevya

Enyi waja wa Allâh, miongoni mwa madhara ya kiafya yanayosababishwa na madawa ya kulevya, ni kwamba ubongo hukauka, husababisha kuchanganyikiwa, macho kuwa na giza, kisunzi, mapigo ya moyo kuwa dhaifu, mkakamo wa mishipa, kupooza viungo, mwanamke kutopata vizuri ada yake ya mwezi, kama ambavyo mtumiaji wa madawa hayo hupata wasiwasi na hamaniko, yeye huona watu wako dhidi yake, hofu zimemzunguka kila upande, huogopa mwisho mbaya na maradhi mabaya. Ameepukana na kila fadhila, ameshikana na kila jambo duni. Ni makosa mangapi yaliyotendwa kutokana na taathira ya madawa ya kulevya ya kila aina, ni machafu na madhambi mangapi yaliyotendwa kwa kupotea kwa akili za watu? Ni heshima ngapi zimeharibiwa, mali kiasi gani zilizoibiwa, ni ajali ngapi zilizopatikana kwa sababu yake, ni watu wangapi walionyakuliwa ambao hawana kosa, yote hayo yanaingia katika athari ya madawa ya kulevya.

Enyi waja wa Allâh, maadui wa Uislamu hawahifadhi haki ya Muislamu, kila mara hujaribu kuwamaliza Waislamu na vijana wao. Kwa ajili hiyo ndio wanatengeneza madawa ya kulevya yanayoweza kutumiwa kiurahisi na wadogo kabla ya wakubwa, na kwa masikitiko madawa haya yameenea kwa vijana wengi wa Kiislamu, yanayosababisha baadhi yao kuwa katika hospitali teule na wengine kuwa jela maisha.

Mwisho

Wajibu wa akina Baba na Walezi kuhusu jambo hili Hatari

Nanyi enyi kina baba, nyinyi mna wajibu muhimu katika jambo hili, watoto wenu ndio wanaolengwa kwa haya madawa ya kulevya, wajibu wenu ni kuwahifadhi, kujihusisha nao na kumuomba Allâh kwa dua yenye ikhlasi na nia ya kweli Atuhifadhi sote dhidi ya maradhi haya yaangamizayo. Vile vile kusaidiana katika kupiga vita maradhi haya, hiyo ndio kinga madhubuti. Kuzungumzia juu ya maradhi haya hatari ni kwa njia ya kunasihiana, kuelekezana na kuchukua tahadhari. Maadui wa Uislamu walio kando yetu wanafuata kila njia ya kuudhuru Uislamu na wafuasi wake, na kuwamaliza vijana wao, yapasa akina baba kuwalea watoto wao malezi yaliyonyooka na utengevu, na kuacha kila lenye kudhuru na kuharibu, tukifanya hivyo tutakuwa tumeitika mwito wa Muumba wetu Mtukufu.

قال تعالى) يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ) [التحريم: 6]

{{Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Allâh kwa anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa}}.

Allâh Allâh tuwe kama anavyotutaka Allâh, tutekeleze wajibu wa Mola wetu unaotupasa, wala tusisahau kauli ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): “Nyote ni wachunga, na kila mmoja ataulizwa kuhusu alichokichunga”. Tunaambizana wenyewe, ndugu zetu na kila mwenye ghera na nchi yake na haki za Waislamu wasaidiane na maafisa wa usalama – Allâh Awaafikie – katika kuwapa habari za wanaofanya biashara hii, kuwataja walanguzi, kuwatahadharsha wanaotumia na kuwataja wanachezea watu, kufanya hivi ni kufuata Kauli ya Allâh (Subhaanahu wa Taala):

قوله تعالى :(وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَى وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ) [المائدة: 2] {{Saidianeni katika wema na uchamngu Wala msisaidiane katika dhambi na uadui}}. Jambo hili latulazimu sote kushikamana bega kwa bega na tusaidiane, huenda Allâh Mtukufu Akaihami miji yetu, watoto wetu, vijana wetu na vizazi vyetu dhidi ya maradhi haya yaangamizayo. Yeye Allâh Ndiye mwenye kutusikia na kujibu dua. Mswalieni Mtume kwa kufuata amri ya Allâh alipotuamrisha:

قوله تعالى:( إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ) [الأحزاب: 56]

{{Allâh na Malaika Wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu}}.

Mwisho

Madhara ya madawa ya kulevya na athari yake mbaya inaonekana wazi kabisa katika jamii yetu. Yote haya ni kwasababu ya jamii kunyamaza kimya na kuacha kuamrisha mema na kukataza mabaya. Ili tuweze kuondosha maradhi ya madawa haya, ni lazima jamii yote kubeba jukumu la kuamrisha mema na kukataza mabaya.

Tunamuomba Allah Atuhifidhie watoto wetu, familia zetu na jamii yote. Tunamuomba Allah atuwezeshe kutekeleza wajibu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya. Ewe Mola tuafikishe katika kila la kheri hapa duniani na kesho akhera.





Vitambulisho:




Mwanamke ni Malkia