NJIA YA ULINGANIZI WA MITUME


4356
wasifu
’Miongoni mwa sehemu zilizo wazi katika visa vya Mitume na Manabii ni sehemu ya kulingania kwa Mwenyezimngu Aliyetukuka na alie juu. Ulinganizi huu una njia ya wazi isiyo na udanganyifu, miongoni mwa sifa za njia hiyo ni kulingania kwa ujuzi

Kazi kubwa ya Mitume ni ulinganizi. Mitume wote walitumwa kuwalingania viumbe kushikamana na Tawhidi. Tawhidi ndio msingi wa ulinganizi.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا أَنِ اُعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ( ]النحل: 36]

{{Na bila shaka tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba ‘Muabuduni Mwenyezi Mungu na muepukeni Iblisi muovu}}.

Mitume ya Allâh ni watu waliochaguliwa walio bora kwa ulinganizi. Inawezekana kutolea ushahidi neno Lake Allâh (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى (قَالُوا يَا صَالِحُ قَدْ كُنْتَ فِينَا مَرْجُوًّا قَبْلَ هَذَا أَتَنْهَانَا أَنْ نَعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آَبَاؤُنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ ) [هود: 62]

{{Walisema: Ewe Swaleh! Hakika ulikuwa kati yetu ni mwenye kuheshimiwa kabla hujasema haya maneno yako. Je! watukataza kuyaabudu waliokuwa wakiyaabudu wazee wetu. Na hapana shaka sisi tuna shaka kwa unayotuitia na ni wenye kulituhumu jambo lako}}.

Neno Lake Allah (Subhaanahu wa Taala):

وقال تعالى) وَاذْكُرْ عِبَادَنَا إبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ أُولِي الْأَيْدِي وَالْأَبْصَارِ45 إِنَّا أَخْلَصْنَاهُمْ بِخَالِصَةٍ ذِكْرَى الدَّارِ وَإِنَّهُمْ عِنْدَنَا لَمِنَ الْمُصْطَفَيْنَ الْأَخْيَارِ [ص: 47]

{{Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim, Is-haqa na Ya’qubu waliokuwa na nguvu na busara. Sisi Tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera. Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora. Na mkumbuke Ismail, Ilyasaa na Dhulkifli, na wote hao ni katika walio bora}}.

Mitume wote walikuja na ulinganizi mmoja. Wote waliwaambia wafuasi wao kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na makatazo yake.

Mfumo wa Ulinganizi

Kutanguliza Tawhidi kuliko ibada nyingine. ‘Abdullah bin ‘Abbass amesema: Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimwambia Mu’adh Ibn Jabal wakati alipomtuma kwenda Yemen: [Hakika unawaendea watu ambao ni Ahlul-Kitâb. Utakapowaendea, walinganie washuhudie kuwa hakuna mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allâh, na kuwa mimi ni Mtume wa Allâh. Watakapokutii kwa hilo, wajulishe kuwa Allâh Amewafaradhia Swala tano kila mchana na usiku. Watakapokutii kwa hilo, wajulishe kuwa Allâh Amewafaradhia Zaka, inachukuliwa kutoka kwa matajiri wao na wanarudishiwa mafukara wao. Watakapokutii katika hilo, basi tahadhari mali yao yenye thamani. Na uogope dua ya mwenye kudhulumiwa, kwani hakuna pazia baina ya dua hiyo na Allâh]. Al-Bukhary.

Kutumia Lugha inayo fahamika na walinganiwa. Ushahidi ni Neno Lake Allâh (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَمَا أَرْسَلْنَا مِنْ رَسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ فَيُضِلُّ اللَّهُ مَنْ يَشَاءُ وَيَهْدِي مَنْ يَشَاءُ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ )[إبراهيم: 4]

{{Hatukumtuma Mtume ila kwa lugha ya kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi Allâh Humuacha akapotea Amtakaye, na Akamwongoza Amtakaye. Naye ni Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima}}.

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Atakapowajia mkarimu wa watu basi mkirimuni]. Imepokewa na Ibu Majah.

Mwangalie Nabii Nuh aliwaambia watu wake: Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini. Mimi si chochote ila ni Mwonyaji wa dhahiri shahiri. Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha. Basi Hukumu baina yangu na wao kwa Hukumu Yako, na Uniokoe na walio pamoja nami, Waumini.

Kuchagua washirika wazuri katika kusaidiana kulingania watu. Ushahidi ni Neno Lake Allâh (Subhaanahu wa Taala) Alipomfanya Musa waziri wake kuwa ni Harun :

قال تعالى : (وَاجْعَلْ لِي وَزِيرًا مِنْ أَهْلِي 29هَارُونَ أَخِي 30اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي 31 وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي 32 كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا 33 وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا 34 إِنَّكَ كُنْتَ بِنَا بَصِيرًا 35) [طه29: 35]

{{Na Unipe waziri katika watu wangu, Harun, ndugu yangu. Kwake yeye Niongeze nguvu zangu. Na Umshirikishe katika kazi yangu. Ili tukutakase kwa wingi. Na tukukumbuke kwa wingi}}.

Muangalia Nabii Swaleh na watu wake katika Neno Lake Allâh (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِنْ كُنْتُ عَلَى بَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّي وَآَتَانِي مِنْهُ رَحْمَةً فَمَنْ يَنْصُرُنِي مِنَ اللَّهِ إِنْ عَصَيْتُهُ فَمَا تَزِيدُونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ) [هود: 63]

{{Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa kheri kwetu. Je, unatukataza tusiwaabudu waliokuwa wakiwaabudu baba zetu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayotuitia}}.

Mwangalie Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), Aliposema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَإِنْ كَادُوا لَيَفْتِنُونَكَ عَنِ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ لِتَفْتَرِيَ عَلَيْنَا غَيْرَهُ وَإِذًا لَاتَّخَذُوكَ خَلِيلًا 73 وَلَوْلَا أَنْ ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدْتَ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلًا 74 إِذًا لَأَذَقْنَاكَ ضِعْفَ الْحَيَاةِ وَضِعْفَ الْمَمَاتِ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ عَلَيْنَا نَصِيرًا 75)[الإسراء73: 75]

{{Na hakika walikaribia kukushawishi uache Tuliyokufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangelikufanya rafiki. Na lau kuwa Hatukukuweka imara ungelikaribia kuwaelekea kidogo. Hapo basi bila shaka Tungelikuonjesha adhabu maradufu ya uhai, na adhabu maradufu ya kifo. Kisha usingepata mtu wa kukunusuru nasi }}.

Aya na Hadithi zinabainisha wazi mfumo wa Mitume ya Allah katika kulingania wanadamu. Na haya ni mafundisho kwa kila Muislamu atakaye fanya kazi hii ya mitume. Ni lazima afuate mfumo sahihi wa kulingania nayo ni mfumo wa Mitume.

Dalili za Kimaumbile na za Kisharia na za Kiakili

Zinachukuliwa hoja hizo kutoka kwa kisa cha Nabii Ibrahim na babake. Mtume Ibrahim alipomwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika upotofu ulio wazi. Na kadhalika Tulimwonyesha Ibrahim Ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini. Na ulipomuingilia usiku aliona nyota, na akasema: Huyu ni Mola wangu Mlezi. Ilipotua akasema: Siwapendi wanaotua. Alipouona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Ulipotua akasema: Kama Mola wangu Mlezi Hakuniongoza, nitakuwa katika kaumu waliopotea. Na alipoliona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipotua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayofanyia ushirikina. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa Aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina. Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Allâh, na hali Yeye Ameniongoza? Wala siogopi hao mnaowashirikisha Naye, ila Mola wangu Mlezi Akipenda kitu. Mola wangu Mlezi Amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je, hamkumbuki? Na vipi niogope hivyo mnavyovishirikisha, hali nyinyi hamuogopi kuwa nyinyi mumemshirikisha Allâh na kitu ambacho Hakukiteremshia uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua? Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma - hao ndio watakaopata amani na wao ndio walioongoka. Na hizo ndizo hoja Zetu Tulizompa Ibrahim kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua kwa vyeo Tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi.

Na pia hupatikana mfano vile vile katika kisa cha Musa na Firauni. Allâh Mtukufu Alimtuma Musa na Haruni Akawambia: Nendeeni kwa firauni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola wako Mlezi! Basi waache Wana wa Israili watoke nasi, wala usiwaadhibu. Sisi tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na amani itakuwa juu ya aliyefuata uwongofu. Hakika tumefunuliwa kwamba hapana shaka adhabu itamsibu anayekadhibisha na akapuuza. (Firauni) akasema: Basi Mola wenu Mlezi ni nani, ewe Musa? Akasema: Mola wetu Mlezi ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza. Akasema: Nini hali ya karne za kwanza? Akasema: Ilimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi katika Kitabu. Mola wangu Mlezi Hapotei wala Hasahau.

Hikima na Mawaidha Mazuri, Kusimulia visa, Kuhimiza, na Kuonya

Yanayoshuhudia hayo ni neno lake Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) kama alivyosimulia Mâlik bin al-Huwairith kwa kusema: [Tulimwendea Mtume nasi tulikuwa barobaro tuliokaribiana kwa umri. Tukaketi kwake masiku ishirini. Mtume alikuwa ni rahimu mwenye huruma. Akadhani kuwa tumewatamani jamaa zetu. Akatwambia: “Rudini kwa jamaa zenu, mukae nao, muwafundishe na muwaamuru, muswali Swala kadha wakati kadha na muswali kadha wakati kadha. Wakati wa Swala ukifika, mmoja wenu awaadhinie na mkubwa wenu awaswalishe]. Al-Bukhary.

Hudheifa amesema: “Walikuja kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) watu kutoka Najran, wakamwambia Mtume: [Tuletee mtu mwaninifu. Akawaambia: “Nitawatumia mtu mwaminifu wa kweli]. Akawatumia Abu ‘Ubaidah bin al-Jarrah.” Al-Bukhari.

Abu Burdah amesema: Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimtuma Abu Musa na Mu’adh bin Jabal huko Yemen. Akasema: [Na akamtuma kila mmoja katika wao sehemu mbili kisha akawaambia: Fanyeni wepesi wala msifanye uzito, na wabashirieni na wabashirieni watu mazuri wala musiwakimbize watu]. Al-Bukhari.

Yameshuhudiwa hayo kwa haya maneno mashuhuri: “Hikma ni kitu kilichompotea Muumini, basi atakapoipata ni haki yake aichukue.” Yatakikana ijulikane kuwa Hadithi hii imepokewa kuwa ni mursal na pia imepokewa kuwa Zaidi bin Aslam ameirufaisha kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) imetolewa na Tirmidhi.

Mwisho

Ndugu katika imani, kwa hakika ni jukumu la kila Muislamu khaswa wale wanaofanya kazi ya ulinganizi kusoma manhaj na mtume wa Mitume katika kulingania. Ulinganizi ni ibada, na haiwezekani kukubaliwa ibada zetu mpaka tufuate mafundisho ya Mtume katika kutekeleza ibada zetu. Historia ya Mitume ina mafundisho mengi kwa kila mtu atakaye kufanya kazi ya Mitume. Kwa hivyo, tunawahimiza Waislamu kusoma Sera ya Mitume kwa lengo la kujuwa mfumo kamili wa maisha yao. Ili tuweze kuwafuata Mitume katika maisha yetu. Tunamuomba Allah Atuwezeshe kushikamana na mafundisho ya Mitume wake, na Atuwezeshe kufuata mfumo wa Mitume katika ulinganizi.





Vitambulisho:




Suluhisho la Kiakili