SIKU YA IJUMA NA HUKMU ZAKE


10913
wasifu
Siku ya Ijumaa, ni siku bora kabisa iliyotokewa na jua. Katika siku hii Mwenyezimngu Alimuumba Adam,na Kiyama kitasimama siku ya ijuma, na ni siku ya Idi kwa Waislamu. Kwa hivyo, yameamrishwa baadhi ya mambo katika siku, miongoni mwao: hutuba ya Ijumaa,kuoga, kujitia manukato, kwenda Ijumaa kwa kuvaa vazi zuri zaidi napambo zuri zaidi, kwenda Ijumaa mapema, kukaa karibu na imamu na kuutayarisha moyo kusikiliza mawaidha na utajo wa Mwenyezi Mungu.

Enyi watu, Mcheni Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na mjuwe ya kuwa hakika Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) huumba atakavyo na huchagua atakavyo. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَيَخْتَارُ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ( {{Na Mola wako huumba atakavyo na huchagua atakavyo, hawana viumbe hiari}}.. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ndie anaye jua hekima kwa kila kitu anacho kichagua miongoni mwa viumbe vyake. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) huchagua Mitume miongoni mwa Malaika na watu. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ameufadhilsha Mji wa Makka kushinda sehemu nyingine. Na akauchagua Mji wa Madina kuwa ni mji aliohamia Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na Masahaba. Kisha akauchagua Baytul Maqdis akajalia ni sehemu ya Mitume wengi ambayo Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ametuelezea habari zao katika Qur’an Tukufu. Na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) amefadhilisha baadhi ya Miezi kuliko mingine na Usiku na Mchana. Akachagua Miezi mine Mitukufu (Dhul-qa’ada, Dhul-hijja, Muharam na Rajab). Na bora wa masiku ni siku ya Ijumaa. Kwa hivyo, mtukuzeni Allah (Subhaanahu wa Taala) na kumsifu na kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Hukumu ya Swala ya Ijumaa

Swala ya Ijumaa ni miongoni mwa swala muhimu za faradhi. Na sharia imetia mkazo zaidi na kusisitiza kutekelezwa swala ya ijumaa kwa jamaa. Na malipo yake ni makubwa zaidi.

Fadhila za siku ya Ijumaa:

Kupata Thawabu na Malipo kwa kila hatua ya kwenda Msikitini sawa na Mtu aliyesimama kuswali na kufunga Mwaka mzima. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Mwenye kuoga na kujisafisha, kisha akaenda Msikitini na mapema na akamkurubia Khatibu na akasikiliza kwa utulivu. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) atamlipa kwa kila hatua malipo sawa na Mtu aliyesimama kuswali na kufunga Mwaka mzima] (Imepokewa na Ahmed).

Kusamehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu za ziada. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Mwenye kutawadha vizuri, kisha akaja Msikitini na akamsikiliza Khatibu na kunyamaza. Anasemehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu]. Imepokewa na Muslim.

Kukubaliwa dua katika siku hii tukufu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna wakati, haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah, ila Mwenyezi Mungi humkubalia Dua yake].

Adabu na Sunna za Siku ya Ijumaa:

Kuoga na kujisafisha na kupaka manukato mazuri pamoja na kuondosha harufu mbaya mwilini.. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Mwenye kuoga siku ya Ijumaa, kisha akaenda Msikitini na mapema. Mfano wake ni kama mtu aliyetowa sadaka ya Ngamia].

Kwenda Msikitini mapema na kumkurubia khatibu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Nedeni mkasali sala ya Ijumaa, na mkae karibu na khatibu].

Kujishughulisha kwa Kumtaja Allah, kusoma Qur’an, kuomba msamaha, kuomba dua kwa wingi na kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Kumsilikiza Khatibu kwa utulivu, bila ya kujishughulisha na mambo mengine. Asema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Mwenye kutawadha vizuri, kisha akaja Msikitini na akamsikiliza Khatibu na kunyamaza. Anasemehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu]. Imepokewa na Muslim.

Mambo yalio katazwa katika swala ya Ijumaa:

Kuja Msikitini kuchelewa na kukata safu kwa kuruka watu, kwa lengo la kutaka kukaa safu ya mbele. Siku moja Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alimuona mtu akikata safu na kuruka watu; Akamuambia kaa chini kwa hakika umewaudhi watu na umefanya maasi makubwa.

Kuwashawishi waja wa Mwenyezi Mungu, kwa kusoma Qur’an kwa sauti kubwa, au kufanya Dhikri kwa sauti ya juu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) aliwakataza Masahaba kusoma kwa sauti ya juu, na akawambia; Asisome mmoja wenu Qura’n kwa sauti ya juu kuliko mwingine.

Kuzungumza wakati wa Khatibu anatoa khutbah ya Ijumaa. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Ukimuambia mwenzako nyamaza na Khatibu akiwa anazungumza, kwa hakika umeharibu swala ya Ijumaa].

Khatari ya kuacha kuswali swala ya Ijumaa

Mtume Muhammad amesisitiza na kutilia mkazo juu la suala la kutekeleza swala ya Ijumaa. Na akawatahadharisha Waislamu wanaoacha kutekeleza swala hii. Adhabu kubwa watakayo pata watu hao hapa duniani ni nyoyo zao kuwa ngumu na kupigwa muhuri wa kughafilika. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Hawataendelea watu kuacha swala ya Ijumaa, mpaka Mwenyezi Mungu apige muhuri nyoyo zao, kisha watakuwa niwenye kuishi katika mughafala].

Ndugu Waislamu, tujihadhari sana na kuacha swala ya Ijumaa, kwasababu adhabu yake ni nzito sana. Moyo ukiwa mgumu, basi mwanadamu anakuwa sawa na myama, hajali lolote wala chochote. Utamuona hamuogopi Mwenyezi Mungu, kwa kufanya maasi usiku na mchana.

Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Taala) athibitishe nyoyo zetu juu ya twaa yake, na atulinde na machafu yote.

Ndugu Waislamu, katika Mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ni kuitukuza siku hii ya Ijumaa, kwani hii ni siku tukufu ilio chaguliwa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na kupatiwa Umma huu wa mwisho.

Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikhusisha baadhi ya vitendo katika siku ya Ijumaa:

Kusoma Surat Sijdah na Surat Insaan katika swala ya Al-Fajiri. Imepokewa na Abu Hureirah – Radhi za Allah ziwe juu yake- {Alikuwa Mtume akisoma katika swala ya Al-Fajri siku ya Ijumaa (Surat Sijdah) katika rakaa ya kwanza. Na katika rakaa ya pili (Surat Insaan)} Muslim.

Kusoma Surat Al-Kahfi. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): {Mwenye kusoma Surat Al-Kahfi siku ya Ijumaa, Mwenyezi Mungu anampa mwangaza baina ya Ijumaa mpaka Ijumaa nyingine}. Al-Bayhaqi na Haakim.

Kuzidisha kwa wingi kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Amesema Ibnu-Qayyim: “Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Bwana wa viumbe vyote, na siku ya Ijumaa ni bwana wa siku zote. Kumswalia Mtume siku hii ina malipo mengi kushinda siku nyingine”.

Kuzidisha kumuomba Allah (Subhaanahu wa Taala) katika siku hii. Kwasababu kuna wakati wa kukubaliwa dua ya Muislamu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna wakati, haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah, ila Mwenyezi Mungu humkubalia Dua yake].

Mwisho

Ndugu katika Imani, kama tulivyo sikia umuhimu wa siku ya Ijumaa, na namna sheria ilivyo tilia mkazo siku hii. Na vilivile malipo na thawaabu nyingi kwa Yule atakae tekeleza ibada kwa masharti yake na nguzo zake. Ni jukumu letu kufanya bidii kwa kufanya ibada mbali mabali kama alivyo tufundisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam), ili tuweze kupata malipo na thawabu nyingi kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Enyi Waislamu, Tushindaneni kufuata Sunna na Mafundisho ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika siku hii kuu.

Mwenyezi Mungu atujaalie miongoni mwa waja wake wema na atupe uwezo wa kufuata Sunna za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Tunamuomba Allah atukubalie ibada zetu na atupe mwisho mwema tukiondoka duniani.





Vitambulisho:




Mtake Msaada Mwenyezi Mungu.