UFAHAMU WA IBADA KATIKA UISLAMU


4383
wasifu
Maana ya ibada katika sheria ya Kiislamu ni mapana na inaingia ndani yake kila jema la kidini na la kidunia. Hakika ya ibada ni jina linalokusanya maneno na matendo yote Anayoyapenda Mwenyezi Mungu na kuridhika nayo. Muislamu katika dunia hii anajua kikweli kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu mja wa kikweli. Anajishulisha kufikia uja huo kama inavyotakiwa ili awe ni mja wa kikweli wa Mola wake. Utukufu wake na ubora wake ni kuwa mja wa Mwenyezi Mngu, wakufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake katika kila mamabo ya Dini yake na dunia yake.

Kumuabudu Mwenyezi Mungu ndio hikma kubwa ya kuumbwa kwa binaadamu. Na ibada ni kuelekea kwa Mungu katika hali zako zote hata ukiwa unafanya mambo ya kawaida na huku watarajia thawabu utalipwa na Allah.

Hikma ya kuumbwa kwa Binaadamu na Majini.

Enyi waja kuumbwa kwa binaadam sio kwa mchezo, bali ni kwa hikma kubwa ndio Allah akawa anatueleza katika Aya nyingi kuhusu kuumbwa kwa binaadamu akatuambia:

وقال جلّ جلاله: ((وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ38 مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ) [الدخان38: 39] {{Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo}}.

وقال: (وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ) [الذاريات: 56].

{{Sikuumba majini na binaadamu ila ni kwa hikma ya kuniabudu}}. Yote haya ni kueleza hikma ya kuumbwa kwa binaadamu.

Mafhuum ya Ibada

Hakika ya ibada ni kila jambo la kheri katika mambo ya dini na mambo ya dunia na inakusanya maneno na vitendo vyenye kumridhisha Allah. Na utukufu wa Muislamu ni kuwa mnyenyekevu na kwenda mbio kuhakikisha kuwa mja wa Mwenyezi Mungu kisawa sawa kwa kufuata maamrisho na kuepukana na makatazo.

Sampuli za Ibada

Kwa fadhila zake Mwenyezi Mungu ameweka ibada nyingi tofauti tofauti, kuna ibada ya moyo kama ikhlas na ibada za mwili kama vile swala tano na kuna ibada za mali kama kutoa zaka. Kutoa mali hali ya kuwa na imani na radhi kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kuna ibada ambazo zinakusanya baina ya mali na mwili kama hija na jihadi. Kisha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ametutukuza kwa kutuwekea sunna za swala na Sadaka na swaumu na hajj na ‘umra ili zipate kutuinua daraja.

Sharti za kukubaliwa Ibada.

Ibada haikubaliwi ila kwa masharti mawili:-

Amali iwe ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na haina riyaa.

Ifanyike kulingana na alivyoiweka Mwenyezi Mungu na kuelezewa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Kwani dini imekamilika haitaki kuzidishwa wala kupunguzwa kwani Allah anatuambia:

قال تعالى : (الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ) [المائدة: 3]

{{Leo nimewakamilishia dini yenu}}. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ameifikisha kama ilivyo na hakuna mtu mpotevu kuliko mwenye kufuata hawaa yake.

Ukitaka malipo kwa mambo ya kawaida huwa ni ibada yenye kukukurubisha.

Ewe Muislamu vitendo vyako vyote, ukikusudia kupata radhi za Mola utapata.

Kuwatii wazazi wako ni ibada. Alikuja mtu kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akitaka ruhusa kwenda jihadi. Akaulizwa: [Je wazazi wako hai? Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): nenda ukapigane jihadi kwa kuwatii]. Utakuta kuwatendea wema wazazi ni kama kwenda katika uwanja wa jihadi. Kuunga kizazi ni kutekeleza wajibu.

Kama vile alivyosema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى (وَاتَّقُوا اللَّهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ) النساء: 1]

{{Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana na (muwatazame) jamaa}}.

Ndugu Muislamu hata chakula unacholisha watoto wako unapata thawabu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Amemwambia Sa’ad: [Hata unacho kiweka katika kinywa cha mke wako]. Yaani utapata thawabu. Imepokewa na Bukhari na Muslim.

Kuwalea watoto wako pia ni ibada, Allah anatuambia:

قال تعالى) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا قُوا أَنْفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا) [التحريم: 6]

{{Ziokoeni nafsi zenu na ahli zenu kutokana na moto}}. Biashara zako, kuoa kwako kwa ajili ya kujihifadhi ni ibada, kila jambo unalolifanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu unaandikiwa thawabu. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ametuambia: [Hakuna Muislamu yoyote atakayepanda mmea, au atakayelima kisha akala mmea huo binaadamu au ndege ila yule aliyeupanda mti ule mara ya kwanza hupata malipo].

Kuondosha udhia katika barabara ni Sadaka na ni ibada, hata ilimu yoyote anayojifundisha mja huwa anapata thawabu iwapo atataka kunufaisha umma atapata thawabu kwa Mungu kwani amali zote huzingatiwa nia.

Namna ya kuitengeneza Ibada na kuifanya kwa yakini.

Ewe Muislamu, kuwa na msimamo na udumu katika ibada na usichoke kwani Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال تعالى) : وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ) [الحجر: 99]

{{Muabudu Mola wako mpaka yakufikie mauti}}. Isiwe hamu yako ni kumaliza ibada au kumalizika, bali hamu iwe ni kuifanya ibada. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akimwambia Bilali: [Tupumzishe kwa swalah]. Imepokewa na Ahmad. Na alikuwa akisema: [Kutulia jicho langu ni katika swala}. imepokewa na An-Nasai kutoka kwa Anas. Hata kumuingilia mke wako ni ibada, hii ni neema ya Mola kwa waja wake.

Kukatazwa kutia uzito na kuvuka mipaka katika Ibada.

Kwani ukiwa na mikazo utashindwa mwishowe, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). alipofikiwa na khabari ya ‘Abdullah bin ‘Umar ya kuwa usiku anasimama kuswali na mchana anafunga, mkewe akamshitaki. Amesema Mtume (Subhaanahu wa Taala): [Hakika Mola wako ana haki juu yako, na Nafsi yako ina haki juu yako, na hakika ahli yako ana haki juu yako, ewe ‘Abdullahi, funga kila mwezi siku tatu, akakataa akasema naweza zaidi ya hizo, akakazana naye Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) mpaka akamfanya kuwa akifunga siku moja na anafungua siku moja, hivi hivi ndio akamueleza kuswali usiku na kusoma Qur-aani].

Na vile vile, kuongeza mambo katika dini ni mja kujisumbua na wala hafikii lengo, kwani amali ndogo yenye kudumu ni bora kuliko amali nyingi ambayo utaifanya siku na siku nyingine utaacha, na Muislamu kuwa na ibada tofauti tofauti ni bora kwani hufanya uhusiano wake na Mola wake uwe na nguvu. Na Mungu atuafikie kila jambo la kheri.

Kumnyenyekea Mwenyezi Mungu ni Sharafu na Utukufu.

Kwa utukufu wa kunyenyekea kwa Allah ndio Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akawa ni mtukufu zaidi wa viumbe wa Mwenyezi Mungu na akalingania mlinganio mtukufu nao ni kuwa mja wa Mungu mwenye kunyenyekea. Allah amesema:

قال سبحانه وتعالى : (سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى( [الإسراء: 1] {{Utakatifu ni wa Allah ambaye alimpeleka mja wake israai}}.

Na Akasema tena:

وقال تعالى) : تبارك الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا) [الفرقان: 1]

{{Ametukuka ambaye kwamba amemteremshia Qur-aani mja wake ili apate kuwakhofisha walimwengu}}. Na ndio alama kubwa ambayo inatakikana ili apate utukufu wa kuwa mja wa Allah mwenye kunyenyekea. Kwa Mtume mwito mtukufu alioitiwa nao ni kuitwa mja wa Allah.

Ibada ni Uhai wa Roho

Kama unataka kujua ladha ya ibada waangalie wenye kufuata dunia na wakakufuru, Mwenyezi Mungu anawaambiaje katika maana ya Aya:

قال الله تعالى) : (وَالَّذِينَ كَفَرُوا يَتَمَتَّعُونَ وَيَأْكُلُونَ كَمَا تَأْكُلُ الْأَنْعَامُ وَالنَّارُ مَثْوًى لَهُمْ) [محمد: 12] {{Wale walio kufuru wanastarehe na kula kama wanavyokula wanyama na moto ndio marejeo yao}}. Kwa hivyo, kama hujaonja utamu wa imani na ibada basi utakuwa ni kama mnyama katika pori.

Kwa hivyo, wale Waislamu waliohadaika kwa kuwaigiza maadui wa uislamu na wakatutaka na sisi pia tuachane na dini. Hao ni maadui wa dini yetu na aqida yetu na wao kwa hakika wanataka tuangamie kama wao na wanatuhusudu kwa imani zetu. Na tujue ya kuwa hakuna kufaulu ila kwa kushikana na dini hii, ni hakika iliyothibitishwa katika kitabu cha Allah na sunnah za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). na hatuna shaka yoyote isipokuwa tunaogopea baadhi ya vijana wa kiislamu kwa kuhadaika nao.

Ndugu Muislamu, angalia jamii ya kiislamu utaona ndio wenye wagonjwa kidogo na wenye uhalifu kidogo na ndio wenye maisha mazuri zaidi, na ukitaka mfano ni uangalie miji mikubwa ya kenya, Nairobi na Mombasa kuna tofauti, Nairobi uhalifu ni mwingi kuliko Mombasa na Serikali kuu iko Nairobi, makao makuu ni Nairobi na ni kwa nini kuwa hivyo, hii ni sababu Waislamu kule ni kidogo.

Kuna watu wanaofahamu Ibada Kimakosa.

Kuna watu wamefahamu ibada kimakosa wakapotea na wakapoteza watu wengine, na watu hao wako sampuli tatu:-

Sampuli ya kwanza: ni waliofahamu ibada nusu nusu na wakaona ibada ni mtu kuswali, kufunga, kutoa zaka na kwenda kuhiji. Mtu huyo huingia Msikitini na akitoka huamiliana kwa riba na mke wake na watoto wake huzunguka uchi, huamini mengine na hukanusha mengine Mola anatuambia katika mafhuum ya Aya:

قال الله تعالى) : أَفَتُؤْمِنُونَ بِبَعْضِ الْكِتَابِ وَتَكْفُرُونَ بِبَعْضٍ فَمَا جَزَاءُ مَنْ يَفْعَلُ ذَلِكَ مِنْكُمْ إِلَّا خِزْيٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يُرَدُّونَ إِلَى أَشَدِّ الْعَذَابِ وَمَا اللَّهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ) [البقرة: 85] {{Munaamini baadhi ya kitabu na mnakufuru baadhi yake, hayakuwa malipo ya mwenye kufanya hivyo ila ni khizaya kaika uhai wa duniani na siku ya qiyama watarejeshwa katika adhabu kali na Mungu si Mwenye kughafilika kwa mambo wanayoyafanya}}.

Sampuli ya pili: ni ya watu ambao wanaabudu asiyekuwa Mungu na kumtegemea asiyekuwa Mungu na anaitakidi ya kuwa kuna watu Maaqtaada na Maautaada na Maabdaali wanaopelekesha ulmwengu na mambo yake, Anasema Mungu katika mafhuum ya Aya:

قال الله تعالى : (قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّهِ( [آل عمران: 154] {{Sema mambo yote ni ya Mungu}}.

Na wengine wanasema: sisi usiku tunamsherehekea Walii fulani ambaye ukiwa hata baharini atakuitikia. Allah (Subhaanahu wa Taala) Anawaambia katika mafhuum ya Aya:

قال الله تعالى) : أَمَّنْ يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ أَئِلَهٌ مَعَ اللَّهِ( [النمل: 62] {{Ukipatikana na madhara hukuna mwenye kuondosha isipokuwa Yeye}}.

Sampuli ya tatu: ni watu ambao ibada zao wanafanya kwa ajili ya Mungu, lakini ibad zao wanazifanya kwa njia ambayo hajafundisha Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Basi ibada za watu hao wanarejeshewa wenyewe, kwani Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ametuambia ya kuwa katika maana ya hadithi yake: [Mwenye kuzusha katika jambo letu (dini yetu hii) jambo ambalo si katika dini, basi jambo hilo litarudishwa]. Hadithi hii imepokewa na Bukhari kutoka kwa ‘Aisha. Watu kama hawa wanapoteza muda wao bure na wataenda kupata hasara siku ya kiyama.

Kufa ndio mwisho wa mtu kufanya Ibada.

Kwani Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anatuambia katika maana ya Aya:

قال تعالى) : وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ ) [الحجر: 99]

{{Na umuabudu Mola wako mpaka ikujilie wewe yakini (kifo)}}.

Na hii inamaanisha kuwa hukuna muda maalumu ila ni kuondoka katika hii dunia. Na kufa ndio ule uhakika ambao ni mchungu, na watu kimaumbile yao huwa hawataki kufa. Allah (Subhaanahu wa Taala) Anatuambia katika maana ya Aya:

قال تعالى: ( (كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ) [الأنبياء: 35]

{{Kila Nafsi itaonja mauti}}.

Na neno la yakini katika maana ya Aya iliyotangulia linakusudiwa Mauti, kama alivyopokea Bukhari neno lake Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alipokufa ‘Uthman ibn Madh-uuni: [Hakika imemjilia yeye yakini, lakini tunaamtarajia kheri kwa Mungu]. Hapo ndio tunajua kuwa maana ya yakini ni mauti

Na vile vile, kikundi cha Maswahaba na Tabiina wametafsiri ya kuwa “yakini” ni mauti kama vile Ikrima na Qataada. Na pia Aya nyingine Allah akituelezea kuhusu watu wa motoni, Allah atuepushe na moto. Akisema katika maana ya Aya:

قال تعالى): مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ42 قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ43 وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ44 وَكُنَّا نَخُوضُ مَعَ الْخَائِضِينَ 45وَكُنَّا نُكَذِّبُ بِيَوْمِ الدِّينِ 46حَتَّى أَتَانَا الْيَقِينُ47 ) [المدثر42: 47] {{Ni jambo gani lililowatia katika moto wa saqar?, watasema tulikuwa hatuswali na tulikuwa hatulishi maskini na tulikuwa tukizungumza pamoja na wenye kuzungumza na tulikuwa tukikanusha siku ya malipo mpaka ikatujilia sisi yakini}}.

Mwisho

Tumeona katika yaliyotangulia ya kwamba ibada sio ile iliyowekewa wakati na sehemu kama swala na hija, bali hata chakula unachokula au kulisha mkeo na watoto wako huwa ni ibada na wapata thawabu.





Vitambulisho:




Tafsiri-ya-quran-in-swahili-SURAT-AL--AN-A'AM