UHIMIZAJI JUU YA SUBIRA


3393
wasifu
subira ni kutu muhimu sana na muislamu atakikana awe na subira katika mambo yake yote,subira katika twaa na subira katika kuacha maasia,na kusubiri juu ya mitihani itakayo mpata,na malipo ya mwenye kusuri ni pepo ya allah s.w

Ikiwa subira ni chungu mwisho wake ni tamu. Subira ndio silaha ya Muislamu ya kupambana na mitihani ya ulimwengu. Bila ya subira Muislamu hawezi kufaulu katika kufanya ibada na mambo ya akhera. Ombeni msaada kwa kusubiri na kuswali. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) yuko pamoja na wanaosubiri. Subira huvuta kheri. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika Qur’an tukufu:

قال تعالى: (يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ) [آل عمران: 200]

{{Enyi mulioamini subirini na shindaneni na kueni macho na mcheni Mwenyezi Mungu ili mupate kufanikiwa}].

Jueni waja wa Mungu kuwa subira ni ukarimu usiokwisha, na ulinzi usioshindwa, na ngome isiyovunjika, subira na nusra ni ndugu wawili na asie vaa vazi la subira basi hushindwa na nafasi na sheitwani.

Subira ni ndugu yake muumini wala hana Imani kwa asie kuwa na subira, na akiwa nayo basi Imani yake ni ndogo na mtu asiekuwa na subira ni kama anavyosema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَعْبُدُ اللَّهَ عَلَى حَرْفٍ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انْقَلَبَ عَلَى وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآَخِرَةَ ذَلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ) [الحج: 11]

{{Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutukia kwayo, na ikimfikia misukosuko hugeuza uso wake, amekhasiri duniani na akhera hii ndiyo khasara iliyo wazi}}. Subira ni tabia za waumini waliokamilika, hawezi kuwa nayo mtu ila baada ya kujaaliwa na Mwenyezi Mungu. Amesema Imam Ahmad; Mwenyezi Mungu ametaja subira katika Qur’an mara tisini (90) katika sehemu tofauti.

Faida ya kusubiri

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) atawapa malipo yao bila ya hesabu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُمْ بِغَيْرِ حِسَابٍ) [الزمر: 10]

{{Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hesabu}}.

Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao katika kuwaongoza na kuwanusuru. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ) [الأنفال: 46] {{Subirini hakika Mwenyezi Mungu yupo pamoja na wenye kusubiri}}.

Mwenyezi Mungu kuifanya subira ni sehemu katika uongozi. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا وَكَانُوا بِآَيَاتِنَا يُوقِنُونَ ) [السجدة: 24]

{{Na tukafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoza watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini}}.

Subira ni bora kwa aliyekuwa nayo. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُمْ بِهِ وَلَئِنْ صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِلصَّابِرِينَ) [النحل: 126]

{{Na ikiwa mutasubiri, basi hakika hiyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri}}.

Subira na Taqwa ni kinga ya vitimbi vya maadui. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَإِنْ تُصِبْكُمْ سَيِّئَةٌ يَفْرَحُوا بِهَا وَإِنْ تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ) [آل عمران: 120]

{{Nyinyi mkisubiri na mkamcha Mwenyezi Mungu, hila zao hazitakudhuruni kitu}}.

Subira inaleta manufaa. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى ) : يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ) [آل عمران: 200]

{{Enyi mulioamini subirini, na shindaneni kusubiri na kuweni macho na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa}}.

Kuwabashiria Mwenyezi Mungu wenye subira kwa kheri tatu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ 155الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ 156أُولَئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ )[البقرة: 157]

{{Wabashirieni subira wale ambao ukiwasibu msiba husema hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake yeye hakika tutarejea, hao juu zao zitakua baraka zitokazo kwa mola wao mlezi na rehema nao ndio wenye kuongoka}}.

Subira hutia mtu peponi na humuokoa kutokana na moto. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال عز وجلّ) : إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ ) [المؤمنون: 111]

{{Hakika Mimi leo nimewalipa (Pepo) kwa sababu ya kusubiri kwao, bila shaka hao ndio wenye kufaulu}}.

Uhakika wa subira

Subira katika lugha ya kiarabu ina maana kuzuia, na maana inayokusudiwa ni kufunga nafsi kutokana na huzuni, kuzuia ulimi kwa kushtaki, viungo kwa kupiga makofi na kupasua mifuko. Na akasema Nun Misri: “Ni kujiepusha na makosa na kutulia pindi unapopatwa na balaa na kudhihirisha utajiri pindi unapofikwa na umaskini”.

Aina za mashtaka:

Mashtaka yasiyopingana na subira, kama alivyosema Mtume Yaakub. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال عز وجلّ) : قَالَ إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّه) [يوسف: 86]

{{Hakika mimi namshtakia Mwenyezi Mungu sikitiko langu na huzuni yangu}}.

Na akasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال عز وجلّ) : فَصَبْرٌ جَمِيلٌ) [يوسف: 18]

{{Subira ni njema}}.

Mashtaka ya saa zote na ya kusimulia

Vigawanyo vya subira:

Subira katika maamrisho ya Mwenyezi Mungu

Subira katika makatazo ya Mwenyezi Mungu

Subira kutokana na kudra zake Mwenyezi Mungu.

Na kama alivyosema Sheikh AbdulKadir Jeilani: hapana budi kwa mja kufanya jambo, na kukatazika kwa jambo na kusubiri kwa Qadar.

Mambo haya matatu Luqman amemuusia mwanawe akisema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ) [لقمان: 17]

{{Ewe mwanangu shika sala, na amrisha mema, na kataza maovu, na subiri kwa yanayokupata}}. Muumini hatamani matatizo na anasubiri pindi anapopatwa na balaa. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) siku miongoni mwa siku alipokutana na adui akimnyemelea mpaka kupinduka jua akamsimamisha akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Enyi watu musitamani kukutana na adui na muombe Mwenyezi Mungu afya na mukikutana nao subirini na jueni kuwa pepo iko chini ya upanga].

Na Abubakar Sidiq amesema “Napenda kuwa na afya nishukuru ni bora kuliko kupatwa na mitihani nisubiri, na muumin anajua lolote linalompata ni kheri. Kama alivyopokea hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Ajabu ya muumin ni kuwa mambo yake yote ni kheri, akipata furaha hushukuru na akipata msiba husubiri na yote ni kheri].

Maisha yote ni mitihani. Anasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى) : وَنَبْلُوكُمْ بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ) [الأنبياء: 35]

{{Na tunakujaribu kwa mitihani wa shari na kheri na kwetu sisi mtarudi}}. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) anawaonya waja wake wakati wowote ili apate kujua alie na subira na wakweli.

Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله) : أَمْ حَسِبْتُمْ أَنْ تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنْكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ) [آل عمران: 142]

{{Je mnadai mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu waliopigana jihadi na hawajapambanua walio na subira}}.

Na akasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقوله تعالى : (وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّى نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنْكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ) [محمد: 31] {{Na bila shaka tutawajaribu mpaka tuwadhihirishe wapiganao jihad katika nyinyi na wanao subiri, nasi tutazifanya mitihani khabari zenu}].

Na akasema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقوله تعالى) : إِنْ يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِثْلُهُ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ وَلِيَعْلَمَ اللَّهُ الَّذِينَ آَمَنُوا وَيَتَّخِذَ مِنْكُمْ شُهَدَاءَ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ 140 وَلِيُمَحِّصَ اللَّهُ الَّذِينَ آَمَنُوا وَيَمْحَقَ الْكَافِرِينَ) [آل عمران: 141] {{Kama yamekupateni majeraha basi na hao watu wengine yamewapata majeraha mfano wa haya na si kwa namna hii tunawaletea watu kwa zama ili Mwenyezi Mungu awapambanue walioamini na awachague miongoni mwenu mashahidi na Mwenyezi Mungu hawapendi madhalimu}}.

Na akasema mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

و قال تعالى) : إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَاللَّهُ عِنْدَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ) [التغابن: 15]

{{Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa}}.

Inadhihiri pindi Mtume alipokuwa Makkah kama alivyopokea hadith na Khabbab bin Arat akisema: [ Tumemshitakia Mtume ((SWALLA LLAHU ‘ALAYHI WASALLAM)) tukisema: je utuombee nusra kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) huchukuliwa mtu kabla yenu akizikwa na hupasuliwa mara mbili kwa msumeno kuanzia kichwani na hukatwa nyama, mifupa yake kwa msumeno wa chuma,na huridhika na adhabu hiyo ili ahifadhike na dini yake, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akapiga mfano akisema aende mtu kutoka Sana’a mpaka Hadhramut hamuogopi isipokuwa Mwenyezi Mungu, na mbwa mwitu yuko pamoja na mbuzi lakini munafanya haraka yaani mutapata adhabu ya washirikina basi subirini kama walivyosubiri kabla yenu].

Fadhila za Subira katika Hadith za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)

Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Muislamu yoyote akifikiwa na msiba basi na aseme kwako wewe Mwenyezi Mungu ndio marudio, Mwenyezi Mungu nilipe kutokana na msiba huo na unipe kheri baada yake].

Alipokufa Baba Salama akasema Mama Salama nani mbora kama Baba Salama? Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamuoa Mama Salama ambaye ni bora kuliko yoyote.

Imepokewa na Aisha akisema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : [ Muumin yoyote akipatikana na msiba isipokuwa Mwenyezi Mungu humtosheleza hata kama amedungwa na mwiba].

Imepokewa na Abi Musa amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Akiwa mgonjwa mwanadamu au akisafiri, Mwenyezi Mungu humuandikia kama alivyokuwa mzima au akiwa mwenye kukaa].

Maneno ya baadhi ya Salaf juu ya Subira:

Amesema Sufyan kuhusu Neno lake Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قوله تعالى) : وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا وَكَانُوا بِآَيَاتِنَا يُوقِنُونَ) [السجدة: 24]

{{Na tukafanya miongoni mwao waongozi wanao ongoza watu kwa amri yetu, walipo subiri na wakawa na yakini}}. Walipochukua Kichwa cha kila jambo (Subira) tukawafanya viongozi.

Walipotaka kumkata mguu Urwa bin Zubeir wakamwaambia: tukunyweshe kinywaji usisikie maumivu akasema Urwa: Mwenyezi Mungu amenipa mitihani ili aone subira yangu. Je nipinge amri yake? (kunywa kinywaji)

Amesema ‘Umar Ibn ‘Abdulaziz: Mwenyezi Mungu ampe neema mja na akampokonya neema hiyo na akasubiri basi subira hiyo inakuwa ni bora kuliko alichopokonywa.

Abubakar alipokuwa mgonjwa aliambiwa je hatukuitii tabibu? Akasema ashaniona tabibu, akaambiwa amekwambia nini? Akasema Abubakar ameniambia kuwa yeye ni mtendaji kwa anachotaka.

Ndugu yangu Muislamu: subiri udhia wa jirani yako na umfanyie wema, ima atatengana na wewe kwa kugura au kwa mauti. Ndugu yangu Muislamu subiri kwa jamii yako ukipata udhia kwao na utoshelezeke. Subiri kwa mke wako kutokana na makosa na upungufu. Huwezi kupata mwanamke aliye kamilika sifa zake, lazima usubiri na uridhike kwa tabia yake. Hapana budi kwa mwanamke kumsubiria mume wake kwani ndio sababu ya kudumu mapenzi.

Lazima uwasubirie wafanyikazi kwani hakuna mtu anayefanya wajibu wake kwa ukamilifu, na tabia za watu zinatafautiana basi hapana budi kuwa na subira na kutazama mambo kwa mwisho wake. Asiyekuwa na subira hupoteza kheri zote.

Namuomba Mwenyezi Mungu pamoja nanyi uwafikie na usaidizi katika kheri zote. Yeye ni muweza wa kila kitu. Namuomba Mwenyezi Mungu atusamehe na Waislamu, basi muombeni Mwenyezi Mungu msamaha na mtubie kwani yeye ni msamehevu na mwingi wa rehema.

Mwisho

Ndugu Muislamu mafanikio ya mwanadamu hapa Duniani na kesho siku ya Mwisho yanafungamana na Subira. Allah (Subhaanahu wa Taala) atamlipa Mwanadamu Kwa kiasi ya subira yake katika maisha yake hapa duniani.

Namuomba Mwenyezi Mungu mwafaka na usaidizi katika kila kheri, yeye ni muweza juu ya kila kitu, namuomba Mwenyezi Mungu msamaha kwa kila dhambi tuliofanya basi mtakeni Mwenyezi Mungu na muregee kwake, yeye ndiye mwingi wa kusamehe.





Vitambulisho:




kuhitajia binandamu Dini