UMUHIMU WA DUA


6699
wasifu
Viumbe wanamhitajia Mola wao Awapatie mambo ya kuwanufaisha na Awaondolee mambo ya kuwadhuru ili wapate kutengenekewa na dini yao na dunia. Na mja hakosi kupata mitihani na maonjo yanayomfanya daima amhitajie Mola wake. Kwa hivyo Mwenyezi Mngu Amemuwekea dua na ameiwekea hiyo dua adabu na masharti na nyakati za kukubaliwa ambapo dua huwa iko karibu zaidi na kujibiwa.

Enyi Waja wa Allah, viumbe vyote vinamuhitaji Mola wao katika kupata manufaa yao au kuzuia madhara yasiwafikie, kwa lengo la maisha yao hapa Duniani na kesho siku ya mwisho. Na kila mja anapojikurubisha kwa Allah, basi Allah anamuinua daraja na kumfanya mtukufu mbele ya viumbe vyake. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anawapa mitihani viumbe vyake kwa misukosuko mbalimbali ili waweze kurudi kwa Mola wao na kuomba msaada kwake katika kupambana na mitihani hiyo.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) anapenda kuombwa msaada na waja wake na anapenda waja wake kurudi kwake pindi wanapofikwa na shida na misukosuko ya ulimwengu. Kufanya hivyo, ndio msingi wa ibada. Na makusudio makubwa ya sharia kuamrisha na kunyeyekea kwa Allah na kutaraji pamoja na kumtegemea Yeye peke yake kwa mambo yote. Imepokewa na Abi Dharri katika hadithi Qudsi: [Amesema Mwenyezi Mungu: Enyi waja wangu nyinyi wote ni wapotevu ila Yule niliye muongoza, basi niombeni uongofu wangu].

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amepanga kila kitu, na Akaweka sababu ya kila kitu. Ameweka sababu za kufaulu Mwanadamu na sababu za kufeli Mwanadamu. Ameumba sababu zote na athari ya hizo sababu, na hakuna kitu kitakua bila ya kutaka Allah (Subhaanahu wa Taala). Na lau angetaka Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kuumba kitu bila sababu angefanya. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى (فَعَّالٌ لِمَا يُرِيدُ ) [البروج: 16]

{{Mwingi wa kutenda Alipendalo}}. Na Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

وقال تعالى): (أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ تَبَارَكَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ) [الأعراف: 54] {{Fahamuni, kuumba ni kwake tu Mwenyezi Mungu, na amri zote ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote}}.

Hukumu ya Kuamrishwa kuomba Dua

Dua ni ibada bora mbele ya Mwenyezi Mungu. Ameamrisha kwa lengo la la kupata kheri na kuzuia shari. Dua ni sababu kubwa ya kupata kheri na Baraka za Mwenyezi Mungu. Na ni sababu kubwa ya kukinga madhara na shari zote. Na hakika Mwenyezi Mungu ameamrisha waja wake kumuomba Dua katika Aya nyingi. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال الله تعالى): وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ )[غافر: 60]

{{Na Mola wenu anasema; Niombeni nitakujibuni. Kwa hakika wale wajivunao kufanya ibada yangu, bila shaka wataingia Jahannam wadhalilike}}.

Uhakika wa kuomba Dua

Kutukuza mapenzi ya mja kwa mola wake katika kuomba msaada wakutatuliwa matatizo ya ulimwenguni na matatizo ya Akhera.

Kuhakikisha ukweli wa kumuabudu Mola wa walimwengu wote. Kufanya hivyo, ni kufungamanisha moyo wa mja na Mola wake na kumtakasia ibada zote Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), na kutotegemea mtu au kitu kingine pamoja na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Kuwa na yakini kamili yakuwa Allah ndie Mweza wa kila kitu, hakuna kitu kinacho mshinda, Mjuzi wa kila kitu, hakuna kitu kilicho fichika mbele ya Allah (Subhaanahu wa Taala).

Kudhihirisha mja unyonge wake mbele ya Muumba wake. Na kumhitaji Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika mambo yake yote. Na huu ndio Ukweli wa kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

Fadhila za Dua:

Dua ni Ibada. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Dua ni Ibada] (Abu-Daaud). Dua ni ubongo wa ibada, kwa sababu Dua imekusanya ibada zote; kunyenyekea, kutegemea, kutarajia, kuogopa, kuomba msaada, n.k.

Dua ni Ibada tukufu kushinda ibada zote. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Hakuna ibada tukufu mbele ya Allah kushinda Dua] (Atirmidhi).

Kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake na hifadhi yake. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika hadithi Qudsi: [Mola Asema: Mimi niko pamoja na mja wangu pindi anapoelekea kwangu kwa maombi yake] (Bukhari na Muslim).

Nyakati za kukubaliwa Dua.

Wakati wa kusujudu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake wakati akiwa katika sijida. Kwa hivyo, ombeni Dua wa wingi] (Muslim).

Baada ya Adhana. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Dua hairejeshwi baina ya Adhana na Iqaama] ( At-Tirmidhi).

Thuluthi ya mwisho wa usiku. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Mola wetu anateremka kila usiku mpaka katika uwingu wa dunia wakati wa thuluthu ya mwisho wa usiku. Na Anasema: Nani mwenye kuniomba nimkubalie dua yake] ( Bukhari).

Siku ya Ijumaa. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Katika siku ya Ijumaa kuna Saa, atakaye omba Dua. Mwenyezi Mungu hukubali dua yake] (Bukhari na Muslim).

Ndugu Waislamu, kukubaliwa Dua na Allah ni lazima yapatikane masharti yake. Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Ametufundisha masharti ya kimsingi ya kukubaliwa Dua.

Masharti ya kukubaliwa Dua:-

Kumtakasia Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na kumpwekesha Allah katika kuomba Dua. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala) :

قال الله تعالى): فَادْعُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ) [غافر: 14 {{Basi muombeni Mwenyezi Mungu yeye tu ibada yenu, ingawa makafiri watachukia}}.

Kujiepusha na haramu; Kula, kunywa na kuvaa mavazi ya haramu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Enyi watu, hakika Mwenyezi Mungu ni mzuri, na hakubali ila kitu kizuri. Kisha akataja mfano wa mtu anayesafiri safari ndefu hali akiwa amechoka, nywele zake zimejaa vumbi, anainuwa mikono yake kuelekeza mbinguni huku akisema: Ewe Mola wangu, Ewe Mola wangu, na hali kwamba chakula chake ni cha haramu, Kinywaji chake cha haramu na mavazi yake ni ya haramu. Vipi Allah ataikubali Dua yake].

Kuhudhurisha moyo wakati wa kuomba Dua, na kuwa na matarajio ya ukweli kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Muombeni Allah hali mkiwa na hakika ya kukubaliwa Dua yenu. Na mjuwe Allah hakubali Dua ya moyo ulioghafilika] (At-Tirmidhy).

Adabu za Kuomba Dua:

Usafi wa mwili. Kwa sababu Dua ni Ibada, na Ibada haikubaliki bila ya usafi

Kuinua mikono juu wakati wa kuomba Dua. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) : “Hakika Mola wenu ana sifa ya haya na ukarimu. Anaona haya kumrejesha mja wake anapoinua mikono yake kumuomba Dua”

Kuomba Dua zilizothibiti katika Qur’an na Sunna ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).

Mwisho

Ndugu Waislamu, kwa hakika Dua ni silaha ya Muislamu. Muislamu anaweza kutumia silaha hii kwa ajili ya kupambana na adui yoyote, sawa katika binadamu au katika majini. Vilevile, Dua ni kinga ya Muislamu, ikiwa Muislamu ataitumia kinga hio kujilinda nayo. Ndugu Waislamu, tusisahau masharti ya kukubaliwa dua zetu, ni muhimu sana. Bila ya kukamilisha masharti hayo dau zetu hazikubaliwi na Allah (Subhaanahu wa Taala). Tunamuomba Allah Atukubalie dua zetu, na Atuepushe na haramu. Atupe uwezo wakutafuta halali. Na Atujaalie mwisho mwema, tukutane naye hali Akiwa radhi na sisi.





Vitambulisho:




Muhammad Abdul Kareem