UTANGAZAJI NA ATHARI YAKE KATIKA MAISHA YA WATU


4367
wasifu
Vyombo vya utangazaji leo kwa sampuli zake vituo vyake tofauti tofauti vina athari kubwa katika kusinyanga fikra za mtoto, familia na jamii yote na kuongoza tabia. Hivyo ni kwa vipindi vya utangazaji vinavyovitangaza vyenye kuvutia sana. Basi yafaa kuvitumia matumizi mazuri na kuvifanya ni mimbari ya ulinganizi wa Uislamu na kueneza tabia sahihi za Kiislamu.

Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote na rehma na amani zmfikie Mtume Muhammad. Napenda kuitanguliza mada hii ya vyombo vya utangazaji, kuwatajia umuhimu wake. Na pia nitawabainishia vipi vyombo vya utangazaji vinaweza kuitumikia Dini na matatizo yanayo vikabili vyombo hivyo.

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Ametupa neema ya ulimi ili tumshukuru kwa neema hiyo kwa kuitumia vilivyo kwa mujibu wa mafunzo mema ya kiislamu. Ametuamrisha Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kuutumia ulimi vizuri tunapozungumza.

Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى): يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا) [الأحزاب: 70]

{{Enyi mulioamini, Mcheni Mwenyezi Mungu na mseme maneno ya sawa}}. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) asema: [ Aliyemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, basi aseme maneno mazuri au anyamaze].

Na Ametilia nguvu mshairi akisema: ‘Zungumza vizuri uwezavyo kwani maneno yako ni yako na kunyamaza ni vizuri na ikiwa hutapata maneno mazuri ya kuzungumza basi kunyamaza bila ya kufanya vizuri ni vizuri’. Asema mshairi mwengine: ‘Kuzungumza ni vizuri na kunyamaza ni usalama basi unapozungumza usiwe na maneno mengi kwani sijajuta kwa kunyamaza hata mara moja lakini nimejuta juu ya maneno yangu mara nyingi’.

Kwa mujibu wa Aya na hadithi na mashairi tuliyoyataja inaonesha wazi kuwa Muislamu hafai kabisa kuutumia ulimi wake kinyume na maagizo ya Allah (Subhaanahu wa Taala), huku tukijua ya kwamba kila siku watu wanawasilina kupitia njia tofauti tofauti kama kutumia simu, barua, na vyombo vingine vya mawasiliano, bali wengine kupitia vyombo vya utangazaji. Na kwa kweli watu wamevielekea mno vyombo hivyo ili kupata habari mbali mbali.

Kwa kweli vyombo vya utangazaji vina faida zake na hasara zake. Kwa hivyo hatusemi kwamba haifai kutumia vyombo hivyo, lakini isiyofaa ni kuvitumia katika njia mbaya isiyokubalika kiislamu. Kwani makafiri wakiwemo Waamerika na Wamagharibi wame vitumia vyombo hivi katika kuwapotosha wanaadamu na njia ya sawa, vikiwemo vyombo vya kusikiliza kama redio na vyombo vya kuonesha kama runinga na vya kusoma kama magazeti, majarida na vyenginevvyo.

Kwa kweli vyombo vya utangazaji vimechukua nafasi kubwa kabisa katika kuwaathiri na kuwapotosha watu kimaadili. Sasa wajibu wetu ni mambo gani ya upotofu yanayoenezwa na makafiri katika vyombo vya utangazaji?. Bila shaka wajibu wetu ni kuwatahadharisha watu na uovu unaoenezwa na vyombo hivyo, kwa kuwalingania katika Uislamu na kuacha upotofu. Napenda kuchukua fursa hii kuwauliza maswali yafuatayo:-

Ulinganizi ni nini ndugu zangu katika imani?

Ni upi umuhimu na ubora wa ulinganizi?

Ni lipi lengo na hukumu ya ulinganizi?

Ni ipi misingi ya ulinganizi ?

Ni zipi nguzo za ulinganizi?

Ni zipi njia na aina za ulinganizi?

Umuhimu wa Ulinganizi

Ulinganizi ni kuwaita watu na kuwafundisha uislamu na kuutekeleza kimatendo kwa ajili ya kuwatakia kheri katika maisha yao hapa duniani na kesho akhera.

Umuhimu wa kulingania watu ni kwamba mlinganizi ana daraja kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu anawaita watu kuwacha ibada zote mbaya na kushikamana na ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala): “ Na hakuna mwenye maneno mazuri kuliko yule anayewalingania watu kwa Mwenyezi Mungu na akafanya vitendo vizuri na akasema Mimi ni katika Waislamu”.

Umuhimu wa ulinganizi ni kwamba anapata anayelingania ujira mkubwa. Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema. [Anayelingania katika uongofu atapata ujira sawa na atakayeufuata uongofu huo na hatapunguziwa katika ujira wake kitu chcchote].

Umuhimu wa kulingania vile vile ni kutii na kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) aliposema: [Nifikishieni hata kama ni Aya moja]. Kulingania hupatikana ndani yake ukamilifu wa kumfuata Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) katika ulinganizi wake wa busara. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Aasema:

قال تعالى) : قُلْ هَذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّهِ عَلَى بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ) [يوسف: 108]

{{Sema hii ndio njia yangu nalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa elimu na busara mimi na wanaonifuata na ametakasika Mwenyezi Mungu na sikuwa ni miongoni mwa washirikina}}.

Wametofautiana wanavyuoni katika hukumu ya ulinganizi, je ni lazima kwa kila mtu au wakifanya baadhi huwatosheleza wengine?. Wanavyuoni wengine wamesema kwamba ni lazima kwa kila Muislamu na wengine wamesema kwamba wakifanya baadhi ya Waislamu huwatosheleza waliobakia. Lakini ilivyo ni kwamba ulinganizi ni lazima kwa kila Muislamu kulingana na uwezo wake. Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ

[آل عمران: 110] ( {Mumekuwa umma bora mliochaguliwa kwa watu munaolingania katika kheri munaamrisha mema na munakataza mabaya}}. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Atakayeona jambo baya katika nyinyi basi aliondoshe kwa mkono wake na ikwa hawezi basi aliondoshe kwa ulimi wake (kwa kusema) na ikiwa hawezi basi achukie kwa moyo wake].

Nachukua tena fursa hii kuitaja misingi inayotegemewa katika kulingania, nayo ni:

Qur’an Tukufu,

Hadithi

Sira ya Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na

Historia ya makhalifa wema waongofu. Misingi tuliyoitaja ndiyo ambayo anayelingania huitumia kuwaita watu katika kheri.

Nguzo za Ulinganizi

Nisikilizeni kwa makini niwatajie nguzo ambazo ni lazima zipatikane ndio upatikane ulinganizi na nguzo hizo ni kama zifuatazo:

Mlinganizi

Anayelinganiwa

Kinacholinganiwa

Njia na aina za ulinganizi.

Yatakiwa mlinganizi asifike na apambike na sifa njema alizokuwa nazo Mtume rehma amani zimfikie sifa hizo ni ukweli, uaminifu, kumtakasia Mwenyezi Mungu ulinganizi, ushujaa, upole, maneno mazuri, subira, uadilifu, na sifa nyingine nzuri.

Wanaolinganiwa ni aina tofauti za watu. Kuna Waislamu, wanafiki, makafiri, viongozi, raia, wakubwa na wadogo. Na kila mmoja katika hawa kuna njia na namna yake ya kumlingania.

Kinacholinganiwa ni Uislamu na hii kazi ya Mitume wote. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا أَنِ اُعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ) {{Hakika[النحل: 36] tuliwatumiliza katika kila umma Mtume kuwalingania watu kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu mujiepushe na sheitani}}.

Njia za ulinganizi ni nyingi. Miongoni mwa njia hizo kuwasiliana na mtu moja kwa moja, kutoa khutba, kuandika vitabu, kufundisha madrasa au vyuo vikuu, kuandika makala gazetini, kutumia vyombo vya utangazaji kufikisha ujumbe kama redio, runinga na vyinginevyo. Kwa hivyo inatakiwa tuwe makini na ufisadi unaopatikana katika vyombo vya habari inatakiwa tuwatahadharishe Waislamu popote waliopo na uovu unaoenezwa na vyombo hivi.

Miongoni mwa aina na sampuli za ulinganizi ni kuwa mfano mzuri wa katika jamii, kujadiliana kwa lengo la kuelimishana, kutumia hikma, pia kutumia mawaidha mazuri, kutumia mifano kwa kutoa visa, na kutumia vitisho na kutia moyo katika mawaidha. Na inatakiwa mlinganizi achague aina ya ulinganizi ambao anaona itakuwa wepesi kukubaliwa ulinganizi wake.

Kwa kweli kusisitiza na kufanya mambo kwa uhakika bila ya kubahatisha na kufuatilia mambo kwa makini ni jambo la kupongezwa sana. Bila ya kusahau kwamba inatakiwa tuwe wakweli na waaminifu katika kukusanya habari na kuwaelezea watu, ili kuhakikisha kuwa na habari ya ukweli. Amesema Mola Wetu (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى : (وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ) [الإسراء: 36]

{{Na usiingilie jambo usilokuwa na ujuzi nalo. Hakika macho, masikio na moyo, vyote hivyo utaulizwa kuhusiana navyo}}.

Pia Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى) : وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا) [الأنعام: 152]

{{Na mutakapozungumza fanyeni uadilifu}}.

Pia Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

وقوله تعالى : (وَقُلْ لِعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ) [الإسراء: 53]

{{Na sema kuwaambia waja wangu waseme maneno yaliyokuwa mazuri}}.

Misingi ya vyombo vya Utangazaji

Uislamu umeweka misingi kuvifanya vyombo vya utangazaji kuwa imara.

Msingi wa kwanza na muhimu kabisa katika maisha ya watu ni kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema Mwenyezi (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى: (فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ) [محمد: 19]

{{Jua kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye}}. Mwingine ni kuhisi majukumu wa kuwalingania watu katika njia ya kheri, kuwa mkweli katika maneno na matendo, pia kuwa muadilifu na kuzingatia adabu za mjadala wakati anapojadiliana na kupeana mawaidha mazuri. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى): ادْعُ إِلَى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُمْ)[النحل: 125] {{Walinganie watu katika njia ya Mola wako kwa hikima na mawaidha mazuri}}.

Matatizo yanayovikumba Vyombo vya Utangazaji

Shukrani zote za dhati ni za Allah (Subhaanahu wa Taala) Mola wa viumbe vyote, huku nikimtakia rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad.

Enyi Waumini! Ni vyema tujue ya kwamba matatizo ambayo yanavikabili vyombo vya utangazaji kiasi kwamba ilipelekea kukosekana habari za uadilifu na kupatikana habari potofu na za ufisadi ambazo hupotosha watu. Na miongoni mwa matatizo hayo ni:-

Kutoeneza vyombo hivyo habari za ukweli mpaka ikapelekea kutokubalika chombo hicho na kudharauliwa na watu na pengine kuzusha fujo baina ya watu na wasimamizi wa chombo hicho.

Kutosaidiwa kimali vyombo vya utangazaji ili kutangaza na kueneza habari kwa nzuri na nyepesi na pia kuzidi kuelimisha watu katika njia nzuri.

Katika matatizo yanayovikumba vyombo vya utangazaji na utangazaji ni ujinga na kufuauta matamanio ya nafsi, kwa kutoa habari bila ya ujuzi na bila kuhakikisha habari ile sawa sawa iwe inamhusu mtu au kikundi. Hii inaweza kuleta fujo pale atakapotoa habari bila ya elimu wala ushahidi.

Katika mifano ya matukio tuliyoyataja ni pale makafiri walipo toa makala ya kumtusi na kumkejeli Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam). Pia kueneza habari za uongo kuhusu Waislamu kuwa ni magaidi, kiasi kwamba inaleta tashwishi na chuki baina ya Waislamu na makafiri.

Katika matatizo ni kutodhaminiwa vyema magazeti na majarida ili kueneza faida katika jamii.

Michezo ya kuigiza katika vyombo vya utangazaji ina mafunzo kuhusu mambo yanayojiri maishani mwa watu. Mchungaji na mchezaji michezo hii lengo lao kubwa ni kuwafikishia ujumbe watu aidha kwa kuwahimiza kufanya jambo fulani au kujiepusha na jambo uvu fulani. Hii ni miongoni mwa faida zinazokusudiwa katika michezo hii. Kwa upande mwengine, kuna madhara ya michezo hii kama mtu kusema uongo, kujifananisha na mwanamke au mwanamume, yeye muigizaji kwenda kinyume na mafunzo anayoyatoa. Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قوله تعالى) : وَمَا أُرِيدُ أَنْ أُخَالِفَكُمْ إِلَى مَا أَنْهَاكُمْ عَنْهُ إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ مَا اسْتَطَعْتُ([هود: 88]

{{Sitaki kuwakhalifu katika yale ninayowakataza sitaki isipokuwa kutengeneza niwezavyo}}.

Yanayoilazimu serikali na watu kwa jumla ni kusimama kidete kutoa nasaha kuwapatia wahusika wa vyombo hivi wamche Mwenyezi Mungu katika suala zima la uenezaji habari. Dini ni kupeana nasaha kwa kuamrishana mema na kukatazana mabaya ili vyombo hivi viwe vitafaidisha umma na vitatoa habari za kweli. Kwa hivyo inatakiwa Waislamu wakubwa kwa wadogo washikamane na ibada hii ya kupeana nasaha ili tufaulu duniani na kesho akhera.Tuna imani ya kwamba endapo wahusika wa vyombo vya utangazaji watashikamana na maadili mema ya kiislamu, watu watafaidika sana.

Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala):

قال تعالى): الَّذِينَ إِنْ مَكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآَتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنْكَرِ) ] الحج: 41]

{{Wale ambao tukiwamakinisha katika hii ardhi wanasimamisha Swala na kutoa zaka na wakaamrishana mema na kukatazana mabaya}}.

Mwisho

Tumetaja japo kwa ufupi nukta zinazofungamana na vyombo vya utangazaji. Vile vile tumetaja umuhimu wa vyombo vya utangazaji katika jamii na vipi vinaweza kutumikia katika kutumikia Dini yetu ya Kiislamu pia tukagusia matatizo yanayokumba vyombo vya utangazaji.

Mwisho tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie ni miongoni mwa wenye kusikia yaliyo mazuri na tukawa ni wenye kuyafuata, tunamuomba Atuoneshe haki tuwe ni wenye kuifuata na atuoneshe batili tuwe ni wenye kuiepuka.





Vitambulisho:




Amani ya Ulimwengu.