ZAKA NA HUKMU YAKE


5035
wasifu
Maana ya ibada katika sheria ya Kiislamu ni mapana na inaingia ndani yake kila jema la kidini na la kidunia. Hakika ya ibada ni jina linalokusanya maneno na matendo yote Anayoyapenda Mwenyezi Mngu na kuridhika nayo. Muislamu katika dunia hii anajua kikweli kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mngu uja wa kikweli. Anajighulisha kufikia uja huo kama inavyotakiwa ili awe ni mja wa kikweli wa Mola wake. Utukufu wake na ubora wake ni kuwa mja wa Mwenyezi Mngu, akufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake katika kila mamabo ya Dini yake na dunia yake.

Allah (Subhaanahu wa Taala) kwa hikma yake amewakunjulia baadhi ya waja riziki na wengine akawabania, na sio dalili ya kupendwa na Mwenyezi Mungu ukiwa umekunjuliwa riziki wala sio kuchukiwa ikiwa umebaniwa riziki. Kwani siku ya kiyama atakayenufaika ni atakayekuwa na moyo uliosalimika na maovu na ukiwa umeneemeshwa na Mola kwa kupewa mali, basi Allah amekupa mtihani kwa kukulazimisha utoe zaka ili kukuangalia utashukuru kwa kutekeleza amri yake ama utafanya ubakhili wa kutotoa zaka.

Kubainisha namna ya Mwenyezi Mungu Alivyotofautisha Waja wake katika Riziki

Enyi watu mcheni Mungu haki ya kumcha. Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, miongoni mwa hikma za Mungu ni vile alivyo tofautisha tabia za watu na riziki zao. Amewakunjulia watu wengine na amewabania watu wengine na yote hayo ni kwa hikma yake Allah. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala) katika Qur’an Tukufu:

قال الله تعالى : ((فَأَمَّا الْإِنْسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ15 وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ 16) [الفجر: 16]

{{Pindi binaadam anapoonjwa na Mola wake na akamtukuza na akampa neema zake basi husema binaadam, Mola wangu amenitukuza, na pindi anapo muonja Mola wake na kumbania riziki yake basi husema, Mola wangu amenitweza. Sivyo hivyo}} [fajri 15-17].

Yaani sio kila aliyepewa ndio amependwa na wala sio kila aliyenyimwa huwa amechukiwa, bali hapa duniani, Mungu humpa amtakaye na humnyima amtakaye kwa hikma anayo ijua yeye mwenyewe ili kuangalia shukrani ya tajiri na subira ya maskini, kwani mali ni balaa kwa wengine na ni neema kwa wengine. Mwenye kujua ya kuwa kuna haki ya Mwenyezi Mungu katika mali yake, basi kwa mtu huyo mali kwake huwa ni neema, na ukisahau na mali ikawa ni sababu ya kupotea, basi mali itakuwa ni balaa kwako na mali itakuwa ni sababu ya kuadhibiwa kwa mtu huyo. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala) katika Qur’an Tukufu:

قال الله تعالى) : فَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُعَذِّبَهُمْ بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنْفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ ) [التوبة: 55]

{{Yasikushangaze mali na watoto wao, hakika si jingine ila anataka kuwaadhibu kwa mali hayo katika uhai wa duniani na iwatoe roho zao hali ya kuwa ni makafiri}}.

Na Allah anatuambia kuhusu nabii wake Suleiman alipo muelimisha aliyo muelimisha na akaona neema ya Mungu juu yake. Amesema Allah (Subhaanahu wa Taala) katika Qur’an Tukufu:

قال الله تعالى) : هَذَا مِنْ فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ) [النمل: 40] {{Hii ni fadhila ya Mola wangu ili apate kunifanyia mtihani kama nitashukuru ama nitakufuru}}. kinyume na aliyeghurika na akasema:

وقال: (إِنَّمَا أُوتِيتُهُ عَلَى عِلْمٍ عِنْدِي(. [القصص: 78]

{{Hakika si jingine, nimepewa kwa ajili ya elimu niliyonayo}}

Uwajibu wa Zaka na kuwa ni Nguzo katika Uislamu.

Ewe Muislamu Allah amewajibisha matajiri haki katika mali zao kuwapa maskini {Na wale katika mali zao kuna haki inayojulikana kwa wenye kuomba na wale walionyimwa}

Ili matajiri wawakunjulie ndugu zao maskini, na Allah Akafanya zaka ni nguzo ya tatu katika nguzo za Uislamu, kama alivyotuambia Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano, kushuhudia ya kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) ni Mtume wake, na kusimamisha swala, na kutoa zaka, na kufunga mwezi wa Ramadhani na kwenda kuhiji]. Amepokea hadithi hii Bukhari kutoka kwa Ibnu ‘Umar. Na katika swahihi mbili kutoka kwa Ibnu ‘Abbas radhi za Mungu ziwe juu yao amepokea neno la Mtume kumwambia Mu’adhi : [Wajulishe ya kuwa Allah (Subhaanahu wa Taala) Amewafaradhia Sadaka juu yao na inachukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kurudiswa kwa maskini wao]. Na dalili nyingi zimeeleza kuhusu zaka na umuhimu wake.

Ni nini Hikima ya Kufaradhishwa Zaka?.

Katika kufaradhishwa kwa zaka kuna hikma nyingi ambazo Allah (Subhaanahu wa Taala) Ameweka ndani yake. Kwanza ni kuusafisha moyo kutokana na ubakhili na kusafisha mali kutokana na uchafu kisha kutia baraka katika mali. Na kutoa zaka ni kuvunja nguvu za shetani kwani ukitoa zaka hutia nguvu imani kwa sababu huwa umeshinda hawaa yako na matamanio yako na wasiwasi wa shetani. Kwa sababu Allah (Subhaanahu wa Taala) Atwambia:

قال الله تعالى) : الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُمْ بِالْفَحْشَاءِ وَاللَّهُ يَعِدُكُمْ مَغْفِرَةً مِنْهُ وَفَضْلًا وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ) [البقرة: 268]

{{Shetani anawaagiza ufukara na anawaamrisha maovu na Mwenyezi Mungu anawaagiza msamaha kutoka kwake na fadhila na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa ilimu}}.

Na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anatuambia: [Na Sadaka haipunguzi mali].

Ewe ndugu yangu Muislamu, toa zaka kwa kupenda na kuamini ya kuwa ni wajibu wako na kumtii Mola wako, usipofanya hivo siku ya qiyama ni siku ambayo hayakufai mali wala watoto ila mwenye kuja kwa Mungu (Subhaanahu wa Taala) hali ya kuwa na moyo uliyosalimika.

Ewe ndugu yangu Muislamu toa zaka na huku watia nia kwani nia ndiyo yenye kuzingatiwa katika amali zote na ukitoa zaka kwa nia ya hiyo zaka, basi pokea bishara ya kheri na baraka kutoka kwa Mungu na malipo makubwa siku ya kupambana na Mola wako.

Sampuli ya Vitu ambavyo yapasa kutolewa Zaka.

Kitu cha kwanza unacho wajibika kutoa ni kinachotoka Ardhini, mbegu na matunda, Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال الله تعالى : (وَآَتُوا حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ) الأنعام: 141]

{{Toeni haki yake siku ya kuvuna}}. Na sharti zake ni kufikia vikapu vitano kwa sasa ni 900kg. Na ikiwa imenoshezwa kwa gharama itakuwa kiwango cha kutoa ni nusu ya fungu la kumi. Ama ikiwa haikuwa na gharama itakuwa ni fungu la kumi. Ama mboga na vinginevyo ambavyo havikai muda mrefu havina wajibu wa kutolewa zaka.

Zaka za Wanyama na Hukumu yake.

Wanyama wanaopaswa kutolewa zaka ni Ngamia, N’gombe na Mbuzi. Wanyama hawa wakiwa wanalisha wenyewe katika mimea ya Ardhini na uchache wa kiwango cha Ngamia kinachopaswa kutolewa zaka ni Ngamia watano na kiwango cha N’gombe ni thelathini na cha Mbuzi ni arubaini. Ama wanyama wanao lishwa kwa kununuliwa chakula hawatolewi zaka ila kuwa mwenyewe ataka kuwafanyia biashara atatoa zaka za biashara.

Zaka ya Mali ya Biashara na Hukumu yake.

Mali ya biashara ni kila kitu ambacho Muislamu amekiandaa kuuza au kununua kutokana na bidhaa tofauti tofauti; kama chakula au mavazi au kipando au chochote chingine kikifika mwisho wa mwaka tutatoa robo ya fungu la kumi ni sawa umepata faida ama hasara. Mfano thamani ya kitu iwe ni shilingi laki moja, lakini baada ya kupitiwa na mwaka ikawa ni laki tano basi zaka zake ni hisabu ya hizo elfu mia tano, na ikiwa kimepunguwa kima cha mali yako elfu mia moja, mali yatahisabiwa vile yalivyo pungua.

Zaka za Naqdain (Dhahabu na Fedha)

Dhahabu na fedha ni wajibu kuzitolea zaka, Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

قال تعالى: (وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنْفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ34 يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنْفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنْتُمْ تَكْنِزُونَ) [التوبة34: 35]

{{Na wale ambao wanaziweka dhahabu na fedha kwenye hazina kisha wasizitolee zaka kwa ajili ya njia ya Mwenyezi Mungu basi wape bishara ya adhabu kali siku ambayo zitachomwa hizo dhahabu na fedha katika moto wa jahannam kisha wapigwe nazo pasi katika nyuso zao na mbavu zao, kisha waambiwe, hizi ndizo mlizozihifadhi kwa nafsi zenu, basi onjeni mlivyokuwa mkivihifadhi}}. Kwa hivyo, dhahbu na fedha hutolewa zaka na hizi pesa pia hutolewa zaka kwani hutumika badala ya dhahabu na fedha na huchukua hukumu ya dhahabu na fedha na hutolewa robo ya fungu la kumi.

Zaka ya Hisa za Kampuni

Na hisa za kampuni mbali mbali huwa zinagawanyika mara mbili:-

Ni hisa ambazo zinabadilishiana, Muislamu akiwa na hisa hizo huwa anataka faida na huzificha wakati mwengine, hisa hizo zinalazimu kutolewa zaka kama vile dhahabu na fedha.

Ni hisa ambazo huwekwa kama akiba, haziuzwi wala kununuliwa isipokuwa mwenyewe huwa anatumia faida yake, basi ile faida akikaa nayo mpaka ukapita mwaka basi itamlazimu kuitolea zaka.

Je, Majumba na Viwanja vya kukodisha vina Zaka?

Zaka za majumba na viwanja vya kukodisha inategemea yale makubaliano ya kukodishiana, ikiwa malipo watachukuwa mwisho wa mwaka basi itakuwa ni wajibu kutoa zaka, lakini kama watapokea malipo ya nyumba kila baada ya miezi sita, basi itakuwa si wajibu kutoa zaka ikiwa malipo hayo watayatumia, lakini ikiwa watakusanya na ikafika mwisho wa mwaka na hujayatumia, utawajibika utoe zaka.

Ama nyumba unayoikaa na gari unalolitumia kwa kulipanda wewe mwenyewe vitu hivi havitolewi zaka.

Wenye kufaa kupewa Zaka.

Ewe ndugu muislamu, Allah (Subhaanahu wa Taala) hakumuachia Mtume yeyote wala Malaika kueleza wanaofaa kupewa zaka, Ewe muislamu, muogope Mwenyezi Mungu katika kutoa zaka zako na ujuwe ya kuwa umepewa amana kwa hivyo fikisha amana kwa wahusika {hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha kutekeleza amana kwa wenyewe} maana ya Aya.

Na kuna sampuli ya watu wanaostahiki kupewa zaka nao ni:-

Maskini na fukara ambao hawana kitu au wanacho lakini hakiwatoshi, basi ni wajibu tuwape zaka za kuwatosha mwaka mzima na anaye hitaji kuoa katika wao, kwani hayo ndio mahitaji muhimu sana. Ama mtu akiwa ana uwezo inafaa umnasihi na umtahadharishe kwani Mume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alijiliwa na watu wawili wakamuomba sadaka, Mtume akawaangalia vizuri akawaona ni watu barabara, kisha Mtume akasema [Mukitaka nitawapa na tajiri hana haki katika zaka wala mwenye nguvu anayefanya kazi]. Maana ya hadithi, imepokea hadithi hii na Ahmad na Abu Daud na Annasai kutoka kwa ‘Ubaydullah ibn Adiyyi.

Na sampuli nyingine ni mwenye madeni ni sawa ikiwa deni ni la nafsi yake kisha akashindwa kulipa lakini isiwe ndio kawaida yake ya kukopesha kisha kushindwa kulipa. Na yafaa kumpaa zaka mtu aliyeingia madeni kwa sababu ya kusaidia umma.

Na wengine wenye kufaa kupewa zaka ni wenye kupigana jihadi na waliokatikiwa na safari.

Kutahadharisha Wasiostahiki Zaka wasiombe.

Ewe Mja wa Allah, Ewe Muislamu ukiwa ni tajiri tahadhari na kuchukua zaka, ukichukua ni haramu unayokula, na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wassalam) Amesema katika maana ya hadithi: [Mwenye kuomba watu kwa ajili ya kufanya wingi (mali yake) hakika si lingine ila anaomba kaa la moto, basi ni apunguze au afanye wingi]. Na katika musnad ya Imam ahmad ibn Hambali amepokea kutoka kwa Abu Hurayra.

Ndugu yangu Muislamu, ni watu wangapi wanaoomba zaka na hali ya kuwa hawana haki ya kupewa. Kwa hivyo ndugu yangu Muislamu, tahadhari kuchukua zaka ikiwa huna haki nayo.

Na wewe mwenzangu mwenye kutoa zaka, uangalie sana ni nani wanao stahiki kupewa zaka. Kuna watu ambao (wamejihifadhi ambao hawaombi watu kwa kuwahimiza, na wasiowajua wanaowadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujihifadhi). Jaribu kupeleleza kwani unaweza ukamuona mtu ni tajiri mbele za watu, kumbe ni maskini na anayejua hali yake ni Allah peke yake.

Na miongoni mwa mambo muhimu ni kuwa Allah ameifanya zaka ni sababu ya jamii kuzoeana na kushirikiana na kushikamana na kuhurumiana Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [Warehemuni walioko Ardhini, atawarehemu aliyeko mbinguni]. Imepokewa ma Ahmad na Abu Dawuud na At-Tirmidhi.

Na lau matajiri wangalitoa zaka za mali yao, maskini wangalitosheka na wangehifadhi nyuso zao na wangehifadhika na uhalifu na wangekuwa mbali na mambo yasiokuwa na kheri.

Basi fanyeni pupa kwa kutoa zaka za mali yenu na kwa wanaostahiki na ni uzuri kuhusisha jamaa zako, kwani ukifanya hivyo utapata mambo mawili, thawabu ya kutoa zaka na thawabu ya kuunga kizazi na utafute majirani zako. Vile vile yafaa tusaidiane kutafuta mafukara wanaostahiki kupewa zaka.

Tumuombe Allah atukubalie mema yetu, Yeye ndiye muweza wa kila kitu na mjue ya kuwa hakika maneno mazuri zaidi ni kitabu cha Mwenyezi Mungu na uongofu bora ni uongofu wa Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wassalam)

Mwisho

Nawausia ndugu zangu Waislamu waliowajibika kutoa zaka wazifikishe zaka hizo kwa wenye kustahiki na inapobidi kuficha zaka zenu wakati mnapotoa mfanye hivyo. Kwani baadhi ya mafukara hawataki kujulikana hali zao, na jaribu kuhusisha zaka zako kwa jamaa zako waliokuwa mafukara, kwani huwa ni sadaka na kuunga kizazi, tumuombe Mwenyezi Mungu atuafikie kila la kheri kwani yeye ndiye muweza wa kila jambo.





Vitambulisho: