Alinuia Kutoa Zakaah Ya Dhahabu Kumpa Ndugu Yake Lakini Ametoa Kwengine


291

SWALI: Natumai wote hamjambo,nilikuwa na swali langu,enshallah mutaweza kunijibu,mie ni mwanamke nilienda kupima dhahabu zaku kwa ajili ya kutoa zaka,nikatajiwa kiasi fulani cha kutoa,nikanuia nusu nitoe kwa dada yangu mkubwa na nusu nitoe kwa dada yangu mdogo,lakini nikatoa kwa mkubwa,halafu ikatokea kilio sehemu na wao hawana uwezo,pesa zilizobaki nikatoa kwenye kusaidia msibani,sasa zakaah yangu yafaa,au yabidi nitoe nyingine kama nilivyonuia kumpa na dada yangu mdogo?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Fahamu dada yetu kuwa Zakaah inapatiwa watu maalumu waliowekwa na Allaah Aliyetukuka kama ilivyokuja katika Qur-aan: ((إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ)) ((Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allaah na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Allaah. Na Allaah ni Mwenye kujua Mwenye hikima)) [At-Tawbah: 60] Je, dada zako wako katika mojawapo wa hizo sampuli nane za watu waliotajwa katika Aayah tuliyoitaja hapo juu? Ikiwa wapo basi kuwapa unapata ujira mara mbili kama alivyosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ndefu ambayo mwisho wake inasema hivi: ((لَهُمَا أَجْرَانِ أَجْرُ الْقَرَابَةِ وَأَجْرُ الصَّدَقَةِ)) البخاري و مسلم ((Watapata wao wawili ujira mara mbili; ujira wa ujamaa (kuunga ukoo) na ujira wa sadaka)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Tukija katika swali lako ni kuwa mwanzo Allaah Aliyetukuka Atakulipa kwa nia yako njema ya kutaka kumpatia dada yako Zakaah ili imsaidie katika maisha yake. Huna makosa yoyote kwa kuacha kumpa dada yako kwa kumsaidia mtu mwengine uliyeona kuwa anahitaji zaidi. Lakini swali ambalo tungependa kukuuliza ni kuwa je, huyu uliyempatia yu katika aina mojawapo ya wale wanaofaa kupewa Zakaah? Je, ulipotoa ilikuwa ni kumsaidia katika ule msiba au ulitia nia ya kutoa kama Zakaah? Pia tufahamu kuwa Zakaah zinatolewa kwa lengo maalumu, nalo ni kumuezesha mtu anayepewa kuweza kujikimu kimaisha na baada ya muda aweze kutoa pia. Sasa pindi unapotoa katika msiba huwa lengo hilo halifikiwi kabisa na mara nyingi misiba yetu yanatoka katika mipaka ya kidini. Tufahamu kusaidia huko hakufai katika Dini kwani Allaah Aliyetukuka Anasema: ((وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ)) ((Na saidianeni katika wema na ucha Mungu wala musisaidiane katika madhambi na uadui)) (5: 2). Na ikiwa ulisaidia msiba kwa kufanywa mambo ya kulisha watu na kuwalaza kwa matanga na kuwagharamia kwa chakula. Vinywaji na mengineyo, basi utakuwa umepoteza mali zako bure na hakuna faida yoyote unayopata na isitoshe unaweza kupata madhambi kwa kushamirisha bid'aah. Soma hapa upate kujua zaidi masuala ya misiba inavyotakiwa ifanywe na yasiyofaa ndani yake: Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bid-ah Ni Dhambi? Kumsomea Khitmah Maiti, Kumchinjia Na Kumuombea Duaa Kwa Pamoja Kuweka Matanga Ni Sunnah? Kisomo Cha Arubaini Baada Ya Maiti Kufa Ni Sunnah Au Bid'ah? Mambo Yanayofaa Kumfanyia Mzazi Aliyefariki Khitmah Kutokufaa Na Madhara Yake Nasaha yetu kwako ni kuwa lau utakuwa una uwezo ingekuwa bora kwako kutoa sehemu iliyobaki ya Zakaah na ukajaalia kile ulichotoa katika msiba kuwa ni sadaka kwako. Na Allaah Aliyetukuka Atakujazi kwa yote uliyoyafanya. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Tarekh ya mitume:utangulizi mkuu