Ameharibu Mimba Karibu Na Miezi Mitatu. Je, Damu Inakuwa Ya Aina Gani? Nifaas Au Istihaadhah?


452

SWALI: Assalam alaykum Nilikuwa na mimba baina ya miezi miwili au mitatu, nikaharibu mimba. Nilivyopata mafunzo kuwa inakuwa ni damu ya Istihaadhah na hivyo napaswa kusali na kufunga. Lakini damu hiyo ni nzito na imetoka mapande mapande. Je hukmu yake ni sawa tu na Istihaadhah? Nitashukuru kupata majibu.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Suala hili lina rai mbili miongoni mwa Maulamaa wakubwa. Kwa mujibu wa rai ya hili kundi la mwanzo la Maulamaa, wanaonelea kuwa maumbile ya mtoto yanaanza kujengeka kuanzia siku themanini na moja taqriban hadi miezi mitatu kwa mujibu wa Maulamaa wengine, na hivyo, ikiwa mwanamke ameharibu mimba kabla ya kipindi hicho cha kuanzia siku themanini na moja au miezi mitatu, basi damu itakayomtoka itakuwa ni damu ya Istihaadhah (damu ya ugonjwa) ambayo haimzuii kuswali na kufunga Swawm, ila tu afanye Wudhuu kila kipindi cha Swalah. Na ikiwa imepita siku themanini na moja hadi miezi mitatu, basi huhesabika ni damu ya Nifaas. Na hoja ya Maulamaa wa rai ya mwanzo ni kwamba maumbile ya mtoto tumboni huanza baada ya taqriban siku themanini na moja ya uja uzito kutokana na dalili katika Qur-aan na Hadiyth kama ifuatavyo: Allaah (Subhaanah wa Ta’ala) Anasema: “Enyi watu! Mkiwa mko katika shaka ya kufufuliwa, basi hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na udongo (baba yenu Nabii Aadam) kisha (tukawa Tunakuumbeni nyinyi) kutokana na manii (tone la maji ya uzazi), kisha (yanageuka kuwa) pande la damu linaloning’inia, kisha (linageuka kuwa) kinofu cha nyama na kinachoumbika na kisichoumbika (kama hali ya mimba inapoharibika) ili Tukubainishieni (Qudra Yetu ya Kufanya Tunalotaka). Na Tunakikalisha fukoni la uterasi Tukitakacho mpaka muda maalumu uliowekwa…” Al-Hajj 22:5 Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “…Hakika kila mmoja hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho...” Al-Bukhaariy na Muslim Hivyo basi, inadhihirisha kwamba kizazi tumboni kinapitia hatua kadhaa; siku arubaini huwa ni nutwfah (mchanganyiko wa manii ya mwanamume na mwanamke). Kisha siku arubaini kinakuwa ni ‘alaqah (kipande cha damu) Kisha siku arubaini nyengine huwa ni mudhwgah (pande la nyama) Hizo ni jumla ya siku mia na ishirini (miezi minne). Na maumbile ya mtoto tumboni kama kichwa, tumbo, mikono, miguu huanza kuumbika katika hatua ya mudhwghah, na sio kabla ya hapo. Hivyo basi mwanamke anapoharibu mimba kabla ya siku themanini na moja taqriban, huwa bado hakijaumbika kitu na damu hiyo haiwi ni damu ya Nifaas bali ni ya Istihaadhah, na aswali na kufunga kama kawaida. na kilichoharibika hakitofanyiwa wajibu wote anaofanyiwa maiti na kitafungwa tu kwenye kitambaa na kufukiwa. Kwa kawaida mwanamke anapokuwa mja mzito huwa hapati damu ya hedhi kama alivyosema Imaam Ahmad kwani kusimama hedhi ndiko kunadhihirisha uja uzito. Ingawa baadhi ya wanawake (wachache) huendelea kupata hedhi hata wakati wa mimba lakini huwa ni wakati wake wa hedhi kwa maana humjia kila mwezi kwa wakati wake maalumu kama vile alivyokuwa hakushika mimba. Na kwa hali hiyo, ya hao wanawake wachache wanaopata hedhi wakati wa mimba, basi wao hupaswa kujizuia na yale yaliyoruhusiwa kama kuswali, kufunga na mengineyo. Ama kundi la pili la Maulamaa, wao wanaonelea kuwa, ikiwa ni kabla ya miezi minne kabla ya kupuliziwa kiumbe roho, wao wanaonelea kuwa mimba ikiharibika kabla ya hapo, basi hiyo itakuwa ni damu ya istihaadhah na kuwa kilichoharibika hakitooshwa wala kukafiniwa wala kuswaliwa na kuzikwa kama maiti wa kawaida, bali kitafungwa na kufukiwa katika shimo vizuri. Na kundi hili dalili yao ni Hadiyth iliyotangulia na tunairudia kuitaja: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “…Hakika kila mmoja hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho...” Al-Bukhaariy na Muslim Wao kwa mujibu wa dalili hiyo, wanaonelea kuwa kiumbe maadam hakijapuliziwa roho, basi kinakuwa hakijakamilika na hivyo hakihesabiwi kuwa ni kiumbe kamili na hivyo, haitohesabiwa damu ile itakayomtoka mwanamke aliyeharibu mimba, kuwa ni damu ya nifaas. Hivyo itakuwa ni damu ya Istihaadhah. Katika rai za Maulamaa wa makundi mawili hapo juu, rai inayoonekana ni ya salama ni ile ya kwanza. Kadhalika kwa wale wanawake wachache ambao hupata hedhi wakati wa mimba kama inavyosemekana, basi wajue kuwa itakuwa ni damu ya hedhi tu kwa sharti ikiwa ile damu ya Istihaadhah imesimama kisha hiyo itakayoanza nyingine itahesabika ni ya hedhi ikiwa huyo mwanamke zimemkuta siku zake na akahahikikisha sifa za damu hiyo ni sifa za damu ya hedhi. Damu ya hedhi itahesabika ikiwa itakuwa na mambo mawili yafuatayo: 1. Ikiwa damu ina sifa za damu ya hedhi ambazo rangi yake kuwa nyekundu ilokoza au kahawia, damu kuwa nzito, na damu kuwa na harufu ya kukirihisha. 2. Mimba imeharibika wakati au tarehe za matarajio ya hedhi. Hivyo, kama tulivyotaja hapo juu, ni kwamba mwanamke aiangalie vyema damu yake vizuri baada ya kuharibu mimba wakati anapotaraji siku zake za hedhi, na baada ya damu ya Istihaadhah kukatika, katika kipindi alichoharibu mimba na baada yake, kuhakikisha kama hiyo damu ni ya hedhi ili ajiepushe na yale yaliyokatazwa kwa mwenye hedhi. Ama ikiwa muda alioharibu mimba si muda wa siku zake za hedhi na ana uhakika hapati hedhi wakati huo, basi ajue hiyo ni Istihaadhah na aendelee kufanya 'Ibaadah zake huku akiwa anajisafisha wakati wa Swalah kabla ya kuchukua Wudhuu na kuvaa kitu cha kuzuia damu isitoke. Na wale wanawake wengine wanaokuwa hawajapata siku zao katika tarehe wanazotaraji wakadhani wana mimba, ni bora wahakikishe hospitalini na kupimwa ikiwa kweli wana mimba kuliko kubaki kuweka dhana kuwa ni mimba kwa sababu tu hakupata siku zake kwa muda aliotaraji. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Muujiza wa Milele