Anapata Matone Ya Damu Wakati Ana Mimba Je Anatakiwa Afanye Ghuslu Kila Anaposwali?


311

SWALI: assalam alykum. kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa watu wote wanaoshiriki katika kuiimarisha website hii ambapo wengi wetu tunakuwa tunafaidika na mengi ndani yake, inshallah Mungu atawalipa kila lenye kheir. suala langu ni hili, ikiwa mwanamke amejulikana kwa vipimo kuwa tayari keshashika mimba lakini ikawa bado anaendelea kupata matone ya damu katika kipindi cha miezi ya mwanzo ya mimba yake, jee mwanamke huyu anafaa kuswali na kama ikiwa anafaa inatakiwa akoge kila anapotaka kuswali au vipi...natumai suala langu litajibiwa kwa uzuri zaidi. asaalam alykum

JIBU: بسم الله الرحمن الرحيم الحمد لله والصلاة والسلام على أشرف الأنبياء والمرسلين وعلى آله وصحبه أجمعين و بعد Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa Du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atutakabalie hizo Du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn. Kawaida mwanamke anapokuwa mjamzito, si aghlabu kupata damu. Lakini ikiwa atapata damu basi itakuwa aidha ni damu ya hedhi au nifaas au ni Istihaadha (damu ya hedhi itokayo muda au siku zisizotarajiwa). Inapokuwa ni damu ya Istihaadha, basi mwanamke anatakiwa aendelee kuswali na kufunga (Swawm) kama kawaida yake. Ili kupambanua baina ya damu ya hedhi na damu ya Istihaadha, wataalamu wameona kwamba zipatikane sifa za damu ya hedhi ndio ijulikane kama ni damu ya hedhi, nazo ni; rangi na harufu, na inapokuwa hali ni hii, basi mwanamke ajiepushe na kuswali na kufunga. Ama ikiwa ni damu nyekundu kabisa inayomjia mwanamke wakati asioutarajia au inayofululiza kutoka baada ya siku zake za hedhi, kwa kupita zaidi ya siku kumi na tano, basi hapo itakuwa ni damu ya Istihaadha, na kama tulivyosema itampasa aswali na kufunga kama kawaida. . Kutokana na swali lako kwamba mwanamke huyo anapata matone ya damu miezi ya mwanzo, basi na atazame kama matone hayo yanazo sifa hizo za damu ya hedhi ili apambanue. Na kama zipo sifa hizo basi ajiepushe na kuswali na kufunga. Ama kama sifa hizo hazikupatikana basi aendelee kuswali na kufunga, na haimpasi kukoga kila mara anapotaka kuswali bali awe anajisafisha tu vizuri kila anapokwenda kuswali. Tafadhali pia soma Jibu katika kiungo kifuatacho upate maelezo kuhusu tofauti baina ya damu ya hedhi na ya Istihaadhwa: Nimepata Hedhi Karibu Magharibi Je Nilipe Swawm? Wa Allaahu A'alam






Vitambulisho:




Hoja yenye kuzungumza.