JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuunganisha Swalah kwa ajili ya hofu ya najasa. Mwanzo inafaa tuelewe Muislamu hawezi kuswali kabla ya wakati wake kuingia, kwani kuingia wakati ni sharti katika kutimia Swalah. Kwa ajili hiyo lau mtu ataswali kabla ya kuingia wakati kama vile kusema kuswali asubuhi Swalah za adh-Dhuhr na al-‘Aswr ni jambo ambalo halikubaliki kishari’ah. Kuhusu umuhimu wa kuswali kwa wakati wake Allaah Aliyetukuka Amesema: “Hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu” (an-Nisaa’ [4]: 103). Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana Waislamu waswali Swalah tano kwa wakati wake makhsusi uliowekwa.