Dhahabu Ya Kujipamba, Yatolewa Zakaah?


334

SWALI: Je dhahabu ya mwanamke ya kujipamba inatolewa zaka?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka siku ya Mwisho. Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu suala hili, a) Kikundi cha kwanza wamasema kuwa ni lazima itolewe kila mwaka ikiwa imefika nisabu, yaani gramu 82.5 ikiwa ni dhahabu, au gramu 577 ikiwa ni fedha. Haya ni kwa dalili ya kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: }}وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ{{ “Na wanaokusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumiii katika njia ya Allah, wabashirie habari ya adhabu iliyo chungu” (Suratu Tawba 9: aya ya 34), Na pia Hadiyth aliyoipokea ‘Amru bin Shu’ayb, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kuwa: Mwanamke mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na binti yake na kwa mkono wa binti yake alikuwa amevaa vikuku viwili vinene vya dhahabu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Je, umevitolea Zakaah?” Akajibu: “Laa”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Je, utafurahi kuwa Mwenyezi Mungu atazibadilisha viwe vikuku vya moto siku ya Qiyaama?” Yule mwanamke akavivua na kumpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku akisema: “Nimevitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Hadiyth ameipokea Imaam Ahmad, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy. b) Kikundi cha pili wakasema kuwa si lazima Zakaah itolewe kwani dhahabu hii inatumiwa kwa mavazi kama vile si lazima kutoa Zakaah kwa mavazi mengineo yanayotumiwa na mtu binafsi kama nguo anazozivaa mtu mwenyewe ao viatu vyake, n.k. Pia wakatoa dalili kuwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akilea mabinti mayatima wa kaka yake katika nyumba yake, na mabinti hao walikua wakivaa dhahabu na wala hakua akiwatolea Zakaah. Kauli yenye nguvu Wa Allaahu A’alam, ni kuwa Muislamu anatakiwa kuwa na hadhari hasa katika Ibaada, kwa hivyo ikiwa dhahabu hiyo imefika kiwango cha Niswaab itolewe Zakaah kila mwaka. Zakaah yake itakuwa 2.5% ya thamani ya dhahabu alionayo ikiwa imepita kiwango cha gramu 82.5. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




fasiri ya Tarjuma ya Qur'ani(juz Tabarak)