Ghuslu - Vipi Kukoga Janabah, Nifaas Na Hedhi


650

SWALI: Naomba inshaallah unieleze kidogo namna ya wanawake wanavyotakiwa kuoga janaba baada ya maangiliano na mumewe. Kwa sababu jambo la kuingiliana baina ya mume na mke linafanyika kila bada siku chache tu, sasa kwa vile wanawake wanajisikia uzito kuosha nywele kila siku kichwa kizima, kwa sababu ni jambo la mara kwa mara bila shaka kuna tofauti na kuoga baada ya wanawake kupata period au baada kujifunguwa. Tulikuwa na shekh mmoja na kwake tulisoma hii habari namna ya kuoga wake zetu baada ya maangiliano,lakini sikumpata sawa sawa, kwa kumbu kumbu zangu alitusomesha kwamba just wanaweza kupaka kwenye kichwa, kwa kutia maji kwenye mikono halafu wakatiya vidole chini ya mizizi ya nywele, (hii ni baada ya maangiliano sio muogo wa baada ya period au kuzaa) na akanukuu kwa kuitaja ile aya inayosema, kwani dini hii ya Kislamu ni rahisi .

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kuna Mas-ala mawili hapa katika Swali hili nayo ni: 1) Ghuslu ya Janaba ni sawa na ya Haydh na Nifaas? 2) Vipi mwanamke afanye Ghuslu ya Janabah? Mas-ala ya kwanza: Ghuslu ya Janaba, ya Haydh na Nifaas yote ni moja tu nayo ni kuosha viungo vyote vya mwili kutokana na kauli ya Allaah سبحانه وتعالى : وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُواْ ((Na mkiwa na janaba basi ogeni)) [Al-Maidah :6] Vile vile: وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُواْ النِّسَاء فِي الْمَحِيضِ وَلاَ تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىَ يَطْهُرْنَ ((Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watwahirike))[Al-Baqarah: 222] Kutoharia ni maana pia kukoga Na dalili kwamba kujitia tohara ni kukoga imo katika aya hii: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَقْرَبُواْ الصَّلاَةَ وَأَنتُمْ سُكَارَى حَتَّىَ تَعْلَمُواْ مَا تَقُولُونَ وَلاَ جُنُبًا إِلاَّ عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىَ تَغْتَسِلُواْ ((Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue mnayo yasema, wala hali mna janaba – isipo kuwa mmo safarini – mpaka mkoge)) [An-Nisaa: 43] Kwa hiyo ni wazi kwamba kukoga (ghuslu) ni kuosha viungo vyote vya mwili. Taratibu ya Ghuslu: Kwanza kabisa ni kutia 'Nia' ambayo inawekwa moyoni wala haitajwi kwa kusema au sivyo itakuwa ni kitendo cha Bid'ah. Kisha ni kujisafisha vizuri na katika Haydh na Nifaas mwanamke ajisafishe na 'Misk' mwishowe baada ya kujimwagia maji ili atoe athari ya harufu ya damu chafu katika sehemu zake. Ghuslu ya Janaba kama alivyokuwa akifanya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Kuosha mikono mara tatu. Kuosha sehemu za siri Kufanya wudhuu kama wudhuu wa Swalah. Wakati mwingine Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akichelewesha kuosha miguu mpaka mwisho kama ilivyokuja katika hadiyth nyingine. Hakikisha maji yanaingia katika nywele kwa kugusisha utosi mara tatu. Jimwagie maji mwili mzima kwa kuanzia upande wa kulia, kisha wa kushoto, na kuosha chini ya kwapa, masikioni, pembeni mwa sehemu za siri, katika vidole vya mguu na sehemu zozote nyingine za mwili zilizokuwa wepesi kusugua. Hii kutokana na hadiyth kutoka kwa bibi 'Aishah رضي الله عنها عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم كان إذا اغتسل من الجنابة يبدأ فيغسل يديه، ثم يفرغ بيمينه على شماله فيغسل فرجه ثم يتوضأ وضوءه للصلاة ، ثم يأخذ الماء ويدخل أصابعه في أصول الشعر حتى إذا رأى أنه قد استبرأ حفن على رأسه ثلاث حثيات ، ثم أفاض على سائر جسده ، رواه البخاري ومسلم Kutoka kwa bibi 'Aishah رضي الله عنها kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akioga Ghuslu ya Janabah alianza kwa kuosha mikono, kisha akijimwagia maji kuanzia mkono wa kulia na kwenda mkono wa kushoto, na akiosha sehemu zake za siri, akifanya wudhuu wa Swalah, akijitia maji kichwani na kufikisha kwa vidole vyake katika mizizi ya nywele mpaka aone kuwa ngozi imeshika maji, kisha akijimwagia maji kichwani mara tatu na kisha mwili mzima. Al-Bukhari na Muslim وفي رواية لهما : ثم يخلل بيديه شعره ، حتى إذا ظن أنه قد أروى بشرته أفاض عليه الماء ثلاث مرات Na katika riwaya imesimuliwa: 'alikuwa akipitisha vidole vyake kwenye nywele zake mpaka anahakikisha kuwa maji yamegusa ngozi kisha akijimwagia maji mwili mzima mara tatu Ghuslu ya mwanamke pia huwa ni sawa na ya mwanamume isipokuwa kama mwanamke ana nywele zilizosukwa hana haja ya kuzifungua bali ni kujimwagia maji na kuhakikisha maji yanagusa ngozi. Lakini kama ana nywele nyingi sana na zimesukwa kwa kukazwa sana basi ni bora afungue ili kuondoa khofu ya kutokufika maji katika nywele zote na ngozi. أم سلمة رضي الله عنها ، أن امرأة قالت يا رسول الله ، إني امرأة أشد ضفر رأسي ، أفأنقضه للجنابة ؟ قال :( إنما يكفيك أن تحثي عليه ثلاث حثيات من ماء ثم تفضي على سائر جسدك ، فإذا أنت قد طهرت ))) رواه أحمد ومسلم والترمذي وقال : حسن صحيح Ummu Salamah amesema kwamba mwanamke alimwambia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Ewe Mtume صلى الله عليه وآله وسلم mimi ni mwanamke mwenye nywele nyingi nzito zilizosukwa, je, inanipasa nizifungue ili nioge (ghuslu) ya Janaabah? Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ((Hapana, inatosha kwako kujimwagia viganja vitatu vya maji kichwani mwako na kisha jimwagie maji mwili mzima na baada ya kufanya hivyo utakuwa umeshasafishika)) [Ahmad na Muslim na Tirmidhiy akasema ni Hadiyth Hasan Sahihi] سألت أسماء رضي الله عنها عن غسل الجنابة فقال: فقال (( تأخذ ماء فتطهر ، فتحسن الطهور ، أو تبلغ الطهور . ثم تصب على رأسها فتدلكه . حتى تبلغ شؤون رأسها . ثم تفيض عليها الماء)) . فقالت عائشة : نعم النساء نساء الأنصار ، لم يكن يمنعهن الحياء أن يتفقهن في الدين رواه الجماعة إلا الترمذي . Asmaa رضي الله عنها alimuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم vipi kuoga Janaabah. Akasema: ((Achukue maji na kujisafisha, kwa kufanya wudhuu, kisha ajimwagie maji kichwani na asugue mpaka ahakikishe kuwa yamefika katika mizizi ya nywele na kisha ajimwagie maji mwili mzima)) Akasema 'Aishah: Uzuri wa wanawake ni wanawake wa Ki-Ansaar haiwazuii hayaa kujifunza dini yao [Imesimuliwa na kundi isipokuwa At-Tirmidhy] Kwa hiyo ni dhahiri kutokana na Hadithi hizo kwamba mwanamke inapasa ahakikishe katika kuoga kwake maji yawe yanagusa ngozi ya kichwa chake, ikiwa ni kwa kujimwagia maji kichwani au kwa viganja vitatu vya maji vilivyojaa. Ama kupangusa tu kichwa (Wiping) bila ya maji kufikia ngozi haifai kwani hii si maana ya 'Ghuslu'. Sheikh 'Abdul-Aziz Bin Baaz رحمه الله alisema, "Wanawake wakumbushwe kuwa watapata thawabu kubwa na malipo mema ya milele kwa kuwa na subira ya kufuata sharia ya dini yao" Wa Allaahu A'alam






Vitambulisho:




Hedhi, inayofanana na hedhi na nifasi