Hajj Itasihi Akiwa Na Uhasama Na Wengine?


609

SWALI: ASALAMA ALAYKUM mimi suala langu kuwa hija yangu itaswihi ikiwa sisemeshani na familiya ya mume wangu, lkn mimi nipo tayari kwa kusemesha nao lkn wao hapo tayari tena hata kwa kuisogelea ile nyumba yao. Naomba nifahamishe uzuri kuhusu hili suala langu.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uhasama na jamaa za mumeo. Hakika ni kuwa uhasama ni sifa ambayo haifai kuwepo baina ya Waislamu licha jamaa wanaohusiana kwa kuoana. Ikiwa utahiji ukiwa na uhasama na jamaa za mumeo, Hija yako itaswihi bila ya wasiwasi wowote. Hata hivyo, ikiwa wewe ndiye uliyeanza uhasama thawabu za ‘amali zako nyingi zitapungua kwa ajili ya kuwa na sifa mbaya kama hiyo. Jambo ambalo unafaa ufanye ni kujaribu njia zote za kuweza kurudisha hali ya awali na kuondosha utesi na uhasama. Tufahamu kuwa Muislamu ni ndugu ya Muislamu, hivyo Waislamu hawafai kuhusudiana wala kuwa na uhasama. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wala si halali kwa Muislamu kumhama nduguye Muislamu zaidi ya siku tatu” (al-Bukhaariy na Muslim). Na pia amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hufunguliwa milango ya Pepo siku ya Jumatatu na Alkhamisi, akasemehewa kila mja asiyemshirikisha Allaah na chochote, ila mtu ambaye ana uhasama na nduguye. Husemwa: Waongozeni hawa wawili mpaka wapatane, Waongozeni hawa wawili mpaka wapatane” (Muslim). Wa kwanza ambaye anaondoka katika uhasama huo ni yule anayemsalimia mwenziwe. Ikiwa utakuwa umejaribu kuwatolea salamu wakakataa basi makosa yote yatawarudia wao nawe hutakuwa na makosa aina yoyote ile. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Ugonjwa wa Upotofu