Hedhi Inayojitokeza Na Kupotea – Nini Hukmu Ya Swalah Na Kitendo Cha Ndoa?


538

SWALI: Assalaam alykum kwa mfano nilipata hedhi kisha nikakaa siku 40 ndipo nikapa hedhi nyengine na nikatumia siku 8 nikapata twahara na kukaa siku 8 za twohara na nikapata hedhi tena na kutumia siku 8 kisha nikaka siku 20 nikafanya tendo la ndoa mara baada ya tendo la ndoa niliona dalili za wazi za kupata hedhi bali hali hiyo ilidumu chini ya masaa 5 nilikaa kwa siku 3 bila ya kupata dalili yoyote ya hedhi na baada ya siku ya 3 ndio nikaanza kuhisi dalili za hedhi na hali hiyo iliendelea kwa siku kadhaa Swali je hizi hali zitahesabiwa zimo katika hukmu gani? Je hizi siku hedhi iliyokuja baada ya siku nane itakuwa na hukmu gani? Je hizi dalili zilizojitokeza kwa kipindi kisha ikapotea kwa muda wa siku 3 itakuwa na hukumu gani kisheria? Na kama nilijizuilia kuswali mara baada ya kuona dalili za wazi za hedhi ambazo baadae zilitoweka na paswa kukidhi swala hizo? Na kama katika kipindi hicho niliingiliana na mume wangu je nitakuwa nimefanya makosa?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu uliyeuliza swali hilo zuri na muhimu kuhusu damu ya ada iliyo na utata kama ulivyoeleza. Utata na kubadilika kwa ada ya mwezi kwa wanawake ni kitu cha kawaida kutegemea mazingira, vyakula, mitihani ya kilimwengu na mifadhaiko na kadhalika. Kwa hivyo, usitishike wala usiwe na wasiwasi kuhusu hilo kwani huwatokea wengi miongoni mwa dada zetu. Ama kuhusu hayo utayakuta yapo mambo ambayo tunafaa tuyaangalie ili tupate hukumu muafaka. Mambo yenyewe ni kama yafuatayo: Ikiwa unaweza kutofautisha baina ya damu yako ya hedhi na damu nyingineyo, utaangalia hii damu ikiwa rangi, harufu na twabia (maumbile) yake ni kama ya hedhi au ni tofauti. Ikiwa ni kama ya hedhi basi ujue hutoruhusika kuswali, kufunga na kujimai na mumeo kama ulivyokuwa kwani hakuna muda maalumu wa mwisho wa hedhi. Ukipata damu ni kinyume na kawaida ya hedhi yako, utaoga na kuswali kwani hiyo haitakuwa ni ada ya hedhi yako. Ikiwa huwezi kutofautisha baina ya hedhi na damu nyengineyo, na jambo hili linapatikana kwa wanawake wengi, utabaki katika hali ya hedhi. Hivyo, hutaswali, hutafunga wala kujamiiana na mumeo mpaka utwahirike kwani hakuna mipaka ya muda kwa damu ya hedhi ingawa baadhi ya Maulamaa wamewka kiwango cha juu kuwa ni siku 15. Ama ule umanjano na kufifia kwa rangi ni maji anayoona mwanamke kama usaha na umanjano wake umeiva. Mwanamke anapoona hii baada ya kukatika damu au baada ya kukauka, haichukuliwi kuwa ni hedhi, naye atakuwa twahara. Kwa hiyo, ataswali, atafunga na kuweza kujamiana na mumewe. Hiyo ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyesema: “Tulikuwa hatuchukulii fifia kwa rangi na umanjano chochote” (Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah). Kuhusu masuala yako yote yanaingia katika kanuni ya hayo maelezo yaliyopo juu. Inaonekana wewe unaweza kutofautisha baina ya hedhi na damu nyingineyo hivyo usiwe na tatizo katika kutekeleza wajibu wa Ibaadah zote. Ikiwa ulikuwa twahara ukakutana na mumeo katika tendo la ndoa baada yake ukapata hedhi tendo hilo halina neno kwani lilifanywa wakati wa twahara. Ama kule kupatwa na hedhi ikakauka kisha baada ya muda ikaja tena hiyo ni dalili kuwa muda wake ulikuwa haujamalizika kabisa kwa hivyo ikiwa umeswali katika hali hiyo Swalah yako itachukuliwa ni sahihi. Ama siku za hedhi zilizokuja baada ya siku nane ni kuwa ikiwa ina sifa za hedhi itakuwa ni hedhi na ikiwa haina sifa za damu ya hedhi itachukuliwa ni istihaadha. Mwenye istihaadha anafaa aswali na afunge kama kawaida kabisa. Ama dalili ambazo zimetokea, na si dalili tu bali ulipata hedhi kisha ikakatika na kurudi tena ni kuwa hedhi hiyo haikumalizika kwa hiyo siku baina yake zote zinahesabiwa kuwa ni hedhi. Na ikiwa uliona hedhi kisha ikatoweka na kurudi tena basi kama tulivyosema ni kuwa muda wote baina yake ni hedhi na ilikuwa hufai kuswali. Na lau uliacha kuswali na kumbe haikuwa hedhi itabidi siku hizo ambazo hukuswali uswali Swalah ya kukidhi. Na katika hali hiyo ikiwa uliingiliana na mumeo ukiwa na yakini kuwa uko bado katika hedhi basi utakuwa umefanya makosa na inabidi uombe msamaha kwa Mola wako Mlezi. Ama ikiwa uliona kuwa uko katika twahara na kumbe uko katika hedhi hutakuwa na makosa yoyote ya kujamiiana na mumeo.






Vitambulisho:




As-Samiry – Mtengeneza Ndama wa Sanamu.