Hukmu Ya Kujichora Mwili Tattoo – Swalaah Inakubaliwa? Afanyeje Baada ya Kutubu Nayo Haitoki?


995

SWALI: Asalam aleikum, kuweka tattoo imekubakiwa katika dini ya kislamu? swalah itakubaliwa? na kama unayo waeza fanyaje? Thank you Assalam alykum. Mimi nimejichora tattoo mwilini. Sasa nimetambua kuwa ni dhambi, na kuitoa haiwezekani tena. Je, nifanyeje sasa na vipi sala zangu zitakubaliwa? Asanteni

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kujichora tattoo mwilini mwako. Tufahamu kuwa Uislamu ni Dini ambayo inakwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu. Sheria inajua kuwa Muislamu kama mwanadamu anaweza kosea, anaweza sahau au kutojua na akaingia katika dhambi. Ikiwa mtu amefanya dhambi bila ya kujua kiuhakika basi Allaah Aliyetukuka Anamsamehe. Na ikiwa amefanya dhambi kwa kujua lakini anataka kurudi kwa Allaah Aliyetukuka, Allaah Anamsamehe madhambi yake ikiwa atatimiza masharti yafuatayo: Kujiondoa katika maasiya. Kujuta katika kufanya dhambi hilo. Aazimie kwa dhati kuwa hatorudia tena kosa hilo. Lau atatekeleza hayo masharti matatu basi atasamehewa madhambi aliyofanya kwani Allaah ni msamehevu sanakama Alivyosema: “Hakika toba inayo kubaliwa na Allaah ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Allaah Huwakubalia toba yao, na Allaah ni Mjuzi na ni Mwenye hekima” (an-Nisaa’ [4]: 17). Na Amesema tena: “Isipokuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Allaah Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allaah” (al-Furqaan [25]: 70 – 71). Kujichora tattoo ni haramu katika Uislamu, na inatakiwa mtu katika kutubia aondoe ovu. Ikiwa michoro haiwezi kuondoka kwa kuwa inapochorwa ni yenye kudumu daima dawamu, inayohitajiwa ni ile azma yake ya nguvu. Allaah Aliyetukuka Hatamuadhibu mtu kwa kushindwa huko baada ya kujaribu. Swalaah atakazo swali katika hali hiyo zitakuwa ni zenye kukubaliwa baada ya muhawala wake huko na kweli kujirekebisha katika hali aliyokuwa nayo. Na Allaah Anajua zaidi.






Vitambulisho: