Ikiwa Mtachezeana Tu Na Kutokwa Manii Inapasa Kukoga Josho?


436

SWALI Assalamu aleikum, Ninaelewa unaweza au mnaweza kugusana tupu baina ya mke na mume na ikawa hamtokuwa wenye kuhitajika kukoga Janaba.Isipokuwa kama ntatokwa na shahawa. Swala langu lipo hapo najua vigumu kwa mwanamke kukumbana na umbile lauume au akawa mwenye kucheza nacho kiungo hicho bila kumtoka chochote. Kwa sisi inawezekana (wanaume) sasa tulijaalie suala hili kwa mwanamke ambae anajaribu kumridhisha mumewe, namzungumzia mwanamke hapa kwa sababu ana njia nyingi za kumridhisha mumewe kwa mfano: mkono, mguu kiuno au hata mdomo. Hivo wanaweza kuvitumia na khafla mume akajikuta tiari amekusha.Na mke akawa bado hajatokwa na chochote, Vipi hapa atahitajika kukonga na yeye. Ishaallah liwe lenye kufahamika suala hili.

JIBU: Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Allah Mtukufu kwa kutupatia fursa hii na neema kubwa ya kuwa Waislamu na tunatarajia kuwa Atatuweka katika hali hiyo mpaka tunapoaga dunia. Swalah na salamu zimfikie kipenzi chetu, Nabii Muhammad Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ahli zake, Maswahaba zake na watu wema mpaka Siku ya Kiyama. Shukrani kwa muulizaji, ndugu yetu mpendwa kwa swali lako Hili. Lakini kama tunavyoliona na kulisoma swali lenyewe halipo wazi na kufuma pale panapotaka kuulizwa. Ni nasaha zetu kwa waulizaji wapendwa wawe ni wenye kuuliza swali moja kwa moja badala ya kuzunguka sana na hivyo hata kueleweka vibaya na wenye kujibu au kutoeleweka kabisa. Ni muhimu ieleweke kuwa wanazuoni wote wa Salaf (waliopita) na khalaf (wa sasa) wameafikiana kuwa ni wajibu kujitwaharisha kwa kuoga kwa yeyote yule (mwanamme na mwanamke) anayetokwa na manii akiwa usingizini au akiwa macho au kwa kujamiiana na pia pale mwanamke anapopata ada yake au damu anayotokwa baada ya uzazi. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Umm Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) aliuliza: “Ewe Mtume wa Allah! Allah Haoni haya juu ya ukweli. Mwanamke anaona katika usingizi kama anavyoona mwanamme, je ni juu yake kuoga?” Akasema: “Ndio, anapoona maji” (Al-Bukhaariy na Muslim). Wametofautiana Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anuhum) kuhusu kuwajibika kuoga kwa kujimai. Miongoni mwao ni wale wenye rai kuwa zinapokutana ngozi mbili zilizotahiriwa basi inakuwa wajibu kwa wote wawili kukoga ikiwa wametokwa na manii au la. Hii ni rai ya Mafakihi wakubwa na hii ndiyo kauli ya jamhuur (wanachuoni wengi). Rai ya pili ni ile inayosema si wajibu kukoga ikiwa hawakushusha, na hii ni kauli ya baadhi ya watu wa Dhahiriy. Dalili zilizotolewa kwa wenye kuunga kauli ya kwanza ni kama zifuatazo: 1. Amepokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Anapokaa mmoja wenu baina ya viungo vinne vya mwili wake (yaani mkewe) na akafanya juhudi (jimai), basi inakuwa wajibu kuoga” (Ahmad na Muslim). 2. Amesema Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokaa baina ya sehemu zake nne na zikakutana ngozi mbili zilizotahiriwa imekuwa wajibu kwao kuoga”. 3. Anahadithia Abu Muusa al-Ash‘ariy (Radhiya Allaahu ‘anhu): Kulizuka tofauti baina ya kikundi cha Muhajirina na kipote cha Ma-Answari, na tofauti yao ilikuwa Ma-Answari wakisema: “Josho la janaba linakuwa wajibu tu pale wanapotokwa na manii”. Lakini Muhajirina wakasema: “Pindi mtu anapostarehe na mwanamke kuoga inakuwa wajibu (ikiwa atashusha au la)”. Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Sawa, mimi nitawatosheleza kwa hilo”. Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) “Nilisimama na nikaelekea kwa ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na kutaka ruhusa ambayo alinipatia”. Nikamwambia: “Ewe Mama wa Waumini! Nataka kukuuliza kuhusu jambo Fulani lakini naona haya kukuuliza”. Akasema: “Usione haya kuniuliza kuhusu jambo ambalo unaweza kumuuliza mamako aliyekuzaa, kwani mimi pia ni mama yako”. Kwa hili nikasema: “Ni kitu gani kinachofanya kuoga kunakuwa wajibu kwa mtu?” Akanijibu: “Umekuja kwa mtu mwenye ujuzi wa hilo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ‘Yeyote mwenye kukaa kwenye sehemu nne (za mwanamke) na sehemu za siri zikagusana baina yao, josho la janaba itakuwa ni wajibu’” (Muslim, Ahmad na Maalik kwa maneno tofauti kidogo). 4. Dalili ya kauli ya pili ni Hadiyth hii: Aliulizwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaambiwa: “Waonaje mtu anapostarehe na mkewe lakini hakushusha (hakutokwa na manii)?” Akajibu: “Atatawadha kama anavyotawadha mmoja wenu kwa ajili ya Swalah, nimemsikia hayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Imenukuliwa na Muhammad bin Ahmad al-Qurtubiy katika kitabu chake Bidaayatul Mujtahid, Mjalada wa kwanza). Wenye kauli ya kwanza wanafuata Hadiyth ya kwanza na nyenginezo ambao tumezitaja na kusema kuwa hukumu ya Hadiyth inayotumiwa na wenye kauli ya pili imefutwa. Na kutilia mkazo Hadiyth hiyo ya kwanza ni ile Hadiyth aliyopokea Ubayy bin Ka‘ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Hakika Mtume wa Allaah Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa ruhusa hiyo mwanzo wa Uislamu kisha akaamrisha kuoga (kwa wenye kujamiiana)” (Abu Dawuud). Na pia maelezo ya ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipomjibu Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuhusu hilo. Katika Hadiyth tulizozitaja hapo juu sehemu zilizotahiriwa ni utupu wa mwanamme na sehemu za siri za mwanamke. Hivyo, pindi utupu wa mwanaume unapoingia katika sehemu ya siri ya mwanamke, josho la janaba linakuwa wajibu kwa wote wawili. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema, “Na mkiwa na janaba basi ogeni” (5: 6). Kusherehesha kuhusu mas-ala haya, Ash-Shaafi‘iy amesema: “Katika lugha ya Kiarabu, janaba inamaanisha tendo aina yoyote ya kukutana kimwili baina ya mume na mke, bila kujali kama manii yametoka au la. Ikiwa mtu atasema, ‘Fulani na Fulani wana janaba kwa sababu ya kadha na kadha’, hii inamaanisha janaba kwa njia yoyote ya kujamiiana baina yao (mume na mke) hata ikiwa hakutakuwa na kushusha. Hakuna anaye kataa kuwa zinaa ambayo ina adhabu maalumu ni kukutana kimwili baina ya wawili hata ikiwa hakuna kutokwa kwa manii”. Na hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatueleza kinaganaga pale Aliposema: “… wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge. Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake – na msipate maji ukusudieni mchanga safi …” (4: 43). Na maana ya mmewagusa wanawake ni kukutana kimwili baina ya mume na mke kama anavyosema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) Kwa hivyo hapana shaka kuwa ni lazima kuwe na kuingiliana kwa sehemu za siri ili mtu iwe ni wajibu kuoga, lakini ikiwa ni kugusana kama alivyosema muulizaji kwa kucheza cheza au kupigana busu au kushikana shikana au jambo jengine lolote mbali na kuingiliana hakutakuwa na uwajibu kwa mke kukoga ikiwa hatotokwa chochote vilevile na mume kadhalika. Lakini ikiwa mwanaume kama ulivyosema atatokwa na maji ya uzazi basi itabidi akoge. Wanazuoni wote wamekubaliana (wameafikiana) katika hili. Na Allah Anajua zaidi.






Vitambulisho:




Mustafa Raad Al Azzawi - Quran Downloads