Je, Inafaa Kumuingilia Mke Baada Hedhi Lakini Kabla Ya Ghuslu?


755

SWALI Assalaam aleykum Je kuna makatazo yoyote ya kumuingilia mkeo baada ya kumaliza hedhi kabla hajaoga josho, hali yuko msafi ?

JIBU: BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad: Kuna ikhtilaaf ya maulamaa kuhusu jambo hili. Kuna waliosema kuwa haimpasi mume kumuingilia mkewe akimaliza hedhi hadi afanye ghuslu nao wamechukua kauli ya Allaah سبحانه وتعالى ((وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُواْ النِّسَاء فِي الْمَحِيضِ وَلاَ تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىَ يَطْهُرْنَ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ)) ((Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watoharike. Wakishatoharika basi waendeeni Alivyokuamrisheni Allaah . Hakika Allaah u Huwapenda wanaotubu na Huwapenda wanaojisafisha)) [Al-Baqarah 222] Hivyo wameona kuwa kujimai baada ya mwanamke kumaliza hedhi lakini kabla ya kufanya ghuslu ni dhambi na itabidi kuomba maghfira na tawbah. Kuna maulamaa walioona kwamba inafaa kujimai baada ya mwanamke atakapokuwa amesafika kutokana na damu ya hedhi yote na kumwagika kwake kumesimama kabisa, hapo anaruhusiwa kurudia kitendo cha jimai baada ya (1) kuosha sehemu inayotoka damu, (2) au kufanya wudhuu au (3) akakoga josho kamili (Ghuslu). Yoyote kati ya haya matatu atakayofanya itaruhusiwa kwao kurudia kitendo cha jimai kutokana na kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Qur'aan: ((فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ)) ((…Wakishatwahirika basi waendeeni Alivyokuamrisheni Allaah. Hakika Allaah Huwapenda wanaotubu na Huwapenda wanaojitakasa)) [Al-Baqarah 2:222] Huu ni msimamo wa Ibn Haazim, 'Atwaa, Qataadah, Al-Awzaa'iy na Daawuud Az-Zaahiriy na wa Mujaahid kama alivyosema Ibn Haazim, "Zote tatu hizi ni Twahara, kwa hiyo, iwapo mwanamke atafanya moja ya njia hizo zilizotajwa, basi atakuwa ni halali kwa mumewe" Kauli hiyo hiyo inatumika kumaanisha kuwa ni kuosha sehemu ya siri katika Aya iliyoteremshwa kuhusu watu wa Qubaa: ((فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُواْ وَاللّهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ)) ((…Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa. Na Allaah Anawapenda wanaojitakasa)) [At-Tawbah 9:108] Na wameona kwamba hakuna popote ima kwenye ayah au Sunnah panaposhurutisha mojawapo kati ya maana tatu hizo zilizotajwa. Na kwa hali hiyo, panabaki kufanya moja ya aina hizo kuwa ni rukhsa ingawa kufanya Ghuslu baada ya mwanamke kumaliza hedhi yake na kabla ya kujimai ndiyo bora zaidi. Na Allaah Anajua zaidi.






Vitambulisho: