Je, Usingizi Unavunja Wudhuu?


302

SWALI: Kama nitalala na udhuu, nimetawadha, nikiamka kuswali sala ya usiku lazima nitawadhe tena?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah. Maulamaa wamekhitilafiana kama usingizi unavunja wudhuu au hauvunji na rai zao ni kama zifuatazo: 1. Kwamba aina yoyote ya usingizi unavunja wudhuu ikiwa ni usingizi mwepesi au mnono au vyovyote atakavyokuwa amelala mtu. Hii ni rai ya Is-haaq Al-Muzani, Hasan Al-Baswriy na Ibn Al-Mundhir kutokana na Hadiyth ya Safwaan bin 'Assaal (Radhiya Allahu 'anhu) ambayo ametaja kuwa kulala ni mojawapo ya mambo yanayovunja wudhuu na haikuelezewa zaidi. كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَأْمُرُنَا إِذَا كُنَّا سَفَرًا أَنْ لا نَنْزِعَ خِفَافَنَا ثَلاثَةَ أَيَّامٍ وَلَيَالِيهِنَّ إِلا مِنْ جَنَابَةٍ ، وَلَكِنْ مِنْ غَائِطٍ وَبَوْلٍ وَنَوْمٍ ) رواه الترمذي وحسنه الألباني), فذكر النوم من نواقض الوضوء . Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamrisha tunapokuwa safarini, tusivuwe khufu zetu (viatu vya ngozi) kwa muda wa masiku matatu, isipokuwa katika hali ya janaabah, lakini sio katika hali ya kinyesi au mkojo au kulala)) [At-Tirmidhiy na amesema Shaykh Al-Abaaniy ni Hadiyth hasan]. 2. Kwamba usingizi hauvunji wudhuu katika hali zote kwa sababu ya Hadiyth ya Anas ibn Maalik: كانوا ينتظرون العِشاء على عهد رسول الله صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ حتى تخفِقَ رؤوسهم ثم يُصلُّون ولا يتوضؤون (رواه مسلم) وفي رواية البزَّار يضعون جنوبهم . Walikuwa wakisubiri Swalah ya 'Ishaa wakati wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi vichwa vyao viliinama (walisinzia), kisha wakaswali bila ya kufanya wudhuu. [Muslim] na katika riwaaya ya Al-Bazzaar: walilala kwa ubavu. Hii ni rai ya Abu Musa Al-Ash'ariyyi (Radhiya Allahu 'anhu) na Sa'iyd ibn Al-Musayyib. 3. Ikiwa mtu atalala akiwa ameketi kwa kuthibiti kikalio chake katika ardhi, basi usingizi huu hauvunji wudhuu, kwa hali yoyote aliyonayo. Hii ni rai ya Imaam Abu Hanifa na Ash-Shaafi'iy. 4. Usingizi unavunja wudhuu isipokuwa usingizi mwepesi kwa yule aliyeketi au kusimama. Hii ni rai ya Imaan Ahmad bin Hanbal [Al-Inswaaf 2/20 25] 5. Wengine wamesema usingizi mnono unavunja wudhuu kwa hali yoyote, si kama usingizi mdogo. Hii ni rai ya Imaam Maalik na imeripotiwa pia kuwa Imaam Ahmad kuwa ana rai hiyo. Tofauti ya usingizi mnono na usingizi mwepesi ni kuwa katika usingizi mnono mtu hawezi kutambua kama kavunja wudhuu au hakuvunja. Ama usingizi mwepesi mtu anaweza kuhisi anapovunja wudhuu kama kutokwa hewa. Rai hii imependekezwa na Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyah (Rahimahu Allah) na katika Maulamaa wetu wa hivi karibuni, ni rai iliyopendelewa na Shaykh Ibn Baaz, Shaykh Ibn 'Uthaymiyn na Maulamaa wa na ndio rai iliyo sahihi. Rai hii inakubaliana na dalili zote kwani Hadiyth ya Safwaan ibn 'Asaal inaonyesha kwamba usingizi unavunja wudhuu na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allahu 'anhu) inaonyesha kuwa wudhuu hauvunjuki. Hadiyth ya Anas ifasiriwe kwa kumaanisha kwamba ni usingizi mwepesi ambao mtu anaweza kuhisi kama kavunja wudhuu, na Hadiyth ya Safwaan ifasiriwe kwa maana ya usingizi mnono ambao mtu hawezi kuhisi anapovunja wudhuu. Hii inaungwa mkono na maneno ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): )) العين وِكَاء السَّهِ ، فإذا نامت العينان استطلق الوكاء)) أحمد وحسنه الألباني في صحيح الجامع ((Jicho ni uzi (kizingo, kishikizo cha msuli) unaofunga tundu la nyuma, basi macho yanapolala, uzi unalegea (unaachia))) [Ahmad na imepewa daraja ya Hasan na Shaykh Al-Abaaniy katika Swahiyhul-Jaami'] Ina maana kwamba kuwa macho ni uzi unaofunga tundu la haja kubwa, yaani unazuia yaliyo ndani yasitoke nje kwa sababu madam mtu yuko macho ataweza kuhisi kinachomtoka lakini akilala uzi hulegea. Kutokana na hali yako muulizaji, inayonyesha kuwa umelala usingizi mnono, hivyo bila shaka wudhuu wako utakuwa umevunjika na itakupasa unapoamka ufanye tena wudhuu. Kwa maelezo zaidi tafadhali ingia katika kiungo kifuatacho kujua mambo yanayovunja wudhuu na yasiyovunja; Je, Wudhuu Unavunjika Ikiwa Hukujifunika Vizuri? Na Allah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Yasser Al-Dosari