Kauli Za Wanachuoni Kuhusu Hadiyth Za Mama Wa Waumini Zinazohusiana na Swawm Za Siku 9 Dhul-Hijjah


240

SWALI:Kauli Za Wanachuoni Kuhusu Hadiyth Za Mama Wa Waumini Zinazohusiana na Swawm Za Siku 9 Dhul-Hijjah

JIBU: AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. Kuhusu Hadiyth hizo mbili; Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) anayosema hakumuona Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufunga masiku hayo yote, na Hadiyth inayosema kuwa mmoja wa wake za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikikusudiwa Mama wa Waumini Hafswah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kasimulia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga masiku hayo tisa, ‘Ulamaa wamefafanua kuhusu Hadiyth hizo mbili. Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ni sahihi kabisa, na Hadiyth Mama wa Waumini Hafswah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) pamoja na kuwa kuna baadhi ya ‘Ulamaa wameona ni sahihi, lakini wengi wameona ina udhaifu. ‘Ulamaa wanasema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asingefunga masiku hayo bila Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kufahamu, kwani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) katika masiku mawili ya kila siku tisa, kwa kuwa mke mwengine wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni Mama wa Waumini Sawdah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alimpa Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) siku ya zamu yake na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliridhia hilo na hivyo Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alikuwa na siku za ziada za zamu za kukaa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko Mama wa Waumini Hafswah na wake wengine. Kwa hali hiyo, Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) angelifahamu ikiwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anafunga masiku hayo. Hivyo, Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ni sahihi na yenye nguvu zaidi. Hata hivyo, pamoja na kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufunga masiku hayo tisa yote, haiashirii kuwa hakupendezewi kufunga masiku hayo japo si jambo lililosisitizwa. Isipokuwa tunajua kuwa, kutokana na Hadiyth ya Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) yenye kuonyesha kuwa kuna fadhila nyingi na kubwa za kufanya matendo mema katika masiku kumi ya Dhul-Hijjah. Hivyo, kufunga katika masiku hayo ni katika 'amali nzuri ambayo vilevile mtu anaweza kufanya na kuchuma malipo zaidi. Kwa ujumla, ukiweza kufunga ni jambo zuri na kuna malipo mengi, usipoweza si lazima isipokuwa ni vizuri usikose siku ya tisa ambayo fadhila zake kubwa ziko wazi katika Hadiyth ya kufunga Swawm ya 'Arafah. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Dini Kwanza.