Kuchukua Mkopo Kwa Ajili Ya Kumpeleka Mzazi Hajj Inafaa?


390

SWALI: INAFAA, KUJITOLEA KUMPELEKA MTU HAJJ KWA PESA ZA DENI, YANI (LOAN)? ANAWEZA KUCHUKUA MTU LOAN KUMPELEKA MTU HAJI, ALAFU AKALIPA LILE DENI KWA UTARATIBU, YANI KIDOGO KIDOGO? LENGO LA KUCHUKUA HIO LOAN NIKUA:- MTU HUNA UWEZO WA KUMPELEKA. IJAPOKUWA TUNAVYO JUA KATIKA NGUZO ZA KISLAMU NI KUA: i. SHAHADATU ANLAA-ILAHA-ILLAH LLAH, WAANNA-MUHAMMADAN-RASULULLAH, ii. WAIQAMI-SWALATY, iii. WAIITAI-ZAKATI, iv. WASWAUMU RAMADHANA, v. WAHIJJUL-BAITY MANISTATWAA-ILAYHI SSABIILA LAKINI STILL UNATAKA KUNAFANYA JAMBO HILI, UKIWA NA IMANI KUWA UTAKUWA NA UWEZO WA KUTEKELEZA JAMBO HILI, LAKINI KITARATIBU ( KIDOGO KIDOGO). UNAE MDHAMIRIA HIO SAFARI NI MTU MZIMA, KWAHIO KUNA HOFU YAKUA WAKATI UTAKAPO ZIPATA PESA HIZO KWA KUCHANGA MWENYE KUPELEKWA ANAWEZA KUWA HAYUPO TENA DUNIANI, AU WEWE MWENYEWE UNAWEZA KUWA HUPO DUNIANI PIA, AU UTAKUA UMESHIKIKA MA MAS’ULIA MENGINE. UNAHAMU YA KUMFANYIA JEMA LA DUA NA AKHERA HUYO MTU, YANI NIKAMA JAZAA YAKO KWA ALIYO KUFANYIA WEWE, IJAPOKUA ITAKUA NI JAZAA NDOGO SANA, KULINGANA NA YALE ALOKUFANYIA WEWE. YANI KWA KIFUPI, MTU HUYO NI MZAZI WAKO. TAFADHALI NDUGU ZANGU WAISLAMU NISAIDIENI KWA SWALA HILI! MIMI NDUGU YENU KATIKA ISLAM.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tumepokea Swali lako kuhusu maudhui ya Hajj. Swali hili lina mas-ala mawili muhimu ya kuzingatia: Kwanza: Kumpeleka mtu kufanya Hajj ikiwa mwenyewe hukufanya bado. Tafadhali soma Swali na Jibu katika kiungo kifuatacho ambalo limeulizwa www.alhidaaya.com na kujibiwa kwa ufafanuzi: Kuwagharimia Wazazi Kwenda Hajj Kabla Ya Kufanya Mwenyewe Pili: Kumpeleka mtu Hajj kwa pesa za mkopo: Fardhi ya kutekeleza Hijjah ni fardhi inayompsa mtu kutekeleza akiwa na uwezo kama Anvyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala): ((وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً ....)) ((Na kwa ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea)) [Al-'Imraan: 96-97]. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kutokana na Hadiyth iliyopokelewa kutoka na 'Umar bin Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu): ((Na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo)) (Muslim, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy] Ibara hii ya Aayah na Hadiyth yana maana ya kuwa kila Muislamu ni lazima ahiji mara moja katika maisha yake akiweza kufanya hivyo. Uwezo una tafswili nyingi na yaliyo muhimu ni: - Awe na afya nzuri ya kuweza kustahamili mazito ya safari. Kuwe na usalama njiani, kwenda na kurudi. Awe na uwezo wa kutoa gharama za safari na kuacha masurufu yote ya wale wanaomtegemea. Ikiwa sharti moja katika hayo imekosekana basi Hijjah haijamlazimu mtu huyo. Fardhi hii ni sawa tu na fardhi ya kutoa Zakaah kwani maskini hana waajib wa kutoa Zakaah pamoja na kuwa Zakaah ni nguzo ya Uislam, na hata mwenye uwezo pia kuna masharti yake mfano, awe na kiasi maalum cha mali na pia sharti ya mali yenyewe iwe imetimia kwa mwaka mzima bila ya kutumiwa. Muislamu anaposhindwa kutimiza sharti hizo, waajib wa kutekeleza fardhi hizo huwa umemuondokea. Na hata atakapofariki akiwa katika hali ya kukosa uwezo basi hana jukumu wala dhambi mbele ya Allaah. Ikiwa hali ni hiyo basi, kuchukua mkopo kwa ajili ya kutekeleza Hajj mwenyewe kwanza haifai, kwani ni jambo la kujikalifisha ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuondoshea: ((لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ)) ((Allaah Haikalifishi nafsi yeyote ila kwa kadiri ya iwezavyo. Faida ya iliyoyachuma ni yake, na khasara ya iliyoyachuma ni juu yake pia)) [Al-Baqarah: 286]. Seuze basi iwe ni kuchukua mkopo kwa ajili ya kumpelekea mtu? Hata kama ni kwa ajili ya mzazi ambaye hakuwahi kutekeleza Hijjah japo una khofu kwamba huenda akaondoka duniani bila ya kutekeleza. Mzazi ambaye hakujaaliwa kutekeleza Hijjah kwa kukosa uwezo wa fedha na siha, naye pia ataingia katika hukmu hiyo hiyo ya 'kutokuwa na uwezo'. Hakuna shaka kwamba kuwatendea wazazi wema ni amri kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), lakini mas-ala mengine kama hayo ya kutekeleza fardhi yana masharti yake. Hii ni Rahma ya Mola wetu kuwa Yeye Mwenyewe Aliyetuumba Ametambua kila hali ya mja Wake itakavyokuwa, ndio maana Akatuwekea takhfifu kama hizo ili tusipate mashaka ya kujikalifisha. Muislamu atakayejitia katika taklifu ya kufanya fardhi atakuwa katika shaka ya kukubaliwa matendo yake atakayoyafanya kwa kwenda kinyume na amri za Mola wake. Vile vile deni ni jambo zito katika Uislamu kwani ni haki ya mtu, hivyo ni jambo la kwanza la kutekelezwa kabla ya ibada yoyote. Muislam ambaye alisubiri kwanza alipe deni lake, kisha akafariki akiwa hakutimiza Hijjah, basi ataonana na Mola wake akiwa amekamilisha Uislamu wake kwa sababu Hijjah haikuwa ni waajib kwake. Lakini akitekeleza Hijjah kabla ya kulipa deni kisha akafariki, atakuwa katika hatari kwa sababu hata wanaofariki wakiwa Mashahidi wanasamehewa kila kitu isipokuwa deni. Sasa vipi basi iwe wengine? Hitmisho ni kwamba haikupasi kuchukua mkopo kwa ajili ya kutekeleza Hijjah ikiwa kwa ajili yako au ya mzazi wako. Inakupasa uridhike na amri za Mola wetu Mtukufu bila ya kujitia mashaka, na bila ya kuhisi kuwa umeshindwa kumtekelezea mzazi wako fardhi. Bali nia yako peke yake inatosheleza kulipwa thawabu kama tunavyopata mafunzo katika Hadiyth ifuatayo: إن الله كتب الحسنات والسيئات , ثم بين ذلك , فمن هم بحسنة فلم يعملها كتبها الله له عنده حسنة كاملة فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له عنده عشر حسنات , إلى سبعمائة ضعف , إلى أضعاف كثيرة , ومن هم بسيئة فلم يعملها , كتبها الله عنده حسنة كاملة , فإن هو هم بها فعملها كتبها الله له سيئة واحدة. متفق عليه ((Allah Ameandika mema na mabaya. Kisha Akayabainisha. Basi atakayetia nia kutenda jema kisha asilifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapofanya hima na akalitenda, ataandikiwa mema kumi hadi kuzidi mia saba na ziada nyingi. Na atakayetia nia kufanya kitendo kibaya kisha asikifanye, ataandikiwa jema moja kamili. Atakapokifanya ataandikiwa dhambi moja)) [Al-Bukhaariy ya Muslim]. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Swala ya Kuomba Mvua