Kufanya Wudhuu Katika Choo Kilichoko Ndani Ya Chumba Na Kusema BismiLlaahi Inafaa?


398

SWALI: Assalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Swali langu ni kuhusu ikiwa udhu unasihi ikiwa mtu ataufanya ndani ya chumba ambacho mna choo na bafu halafu kuna mfereji wa maji ambao unafanya ufanyaji wa udhu uwe sahali.Tena izingatiwe ya kwamba mtu hawezi kusema Bismillahi kwa sauti bali kwa kimoyo moyo kwa kuwa hapo ni chooni. Je udhu utasihi ukifanyiwa ndani ya chumba hicho. Tafadhali nijibuni kwa urefu na kwa haraka kwa kuwa siku hizi watu wengi wanaishi katika nyumba ambazo choo na bafu zipo mahali pamoja kwa hivyo wanaona ni sawa kutawadhia hapo.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu hukumu ya kusema BismiLLaah wakati wa kutawadha chooni. Hakika ni kuwa Uislamu ni njia kamili ya maisha ya mwana Aadam hivyo hakuna lililoachwa katika kila jambo. Kwenda haja pia ni jambo ambalo tumeelezewa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Miongoni mwa adabu za kuingia chooni ni: 1. Usiingie na kitu chenye jina la Allaah Aliyetukuka ila ukihofia kupotea au kuibwa. 2. Kujisitiri kutokana na watu. 3. Kuomba kinga kwa Allaah kutokana na mashaytwaan kabla ya kuingia chooni. Ni katika Sunnah kusema kabla ya kuingia: “Allaahumma inniy A'udhu bika minal Khubuthi wal Khaba'ith – Kwa jina la Allaah, Ee Allaah! Najikinga Kwako kutokana na majini wanaume na wanawake" (Ahmad, Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaa'iy na Ibn Maajah). 4. Asizungumze kabisa chochote, si adhkaar wala du’aa, hufai kurudisha salaam wala kuitikia Adhaan. Anaweza mtu kuzungumza tu kukiwa na haja na inapohitajika kuitika kwa jambo maalum. Tukirudi katika swali lako ni kuwa hakuna tatizo kwa Muislamu kutawadha chooni na kadhaalika hivyo vyoo vya ndani ya nyumba zijulikanazo kama 'self container'. Unaweka Niyyah yako moyoni kwa ajili ya kutawadha. Ama suala la kusema BismiLLaah kabla ya kutawadha, hili lina khilafu kutokana na Ahaadiyth zake zilivyochambuliwa na Wanachuoni wa Hadiyth. Wako wanaoona hazijathibiti na wako walioona ni nzuri na hivyo kufaa kutumika. Katika hao wanaoona kuwa hizo Ahaadiyth zina daraja nzuri, wako wanaosema ni lazima kusema BismiLLaah kabla ya kuchukua wudhuu na wengine wanaona ni jambo lenye kupendezwa. Ama wanaoona kuwa Hadiyth haijathibiti, wanaoona hakuna ulazima wa kusema BismiLLaah kabla ya wudhuu, isipokuwa miongoni mwao wako wanaoona si vibaya kusema kwa sababu wudhuu ni jambo zuri. ​Ama kusema BismiLLaah ndani ya choo, Wanachuoni wengi wameonelea ni jambo lisilopendeza. Hata hivyo kuna wachache walioona kusema BismiLLaah ni lazima kabla ya wudhuu na hivyo hiyo ni dharura kuisema hata mtu akiwa ndani ya choo wakati anachukua wudhuu. ​Wengine wanaonelea hakuna ubaya kuisema kimoyoni bila kutamka maneno. ​Kufupisha yote hayo, ni bora kutosema BismiLLaah chooni na itatosha kuchukua wudhuu wako. Na Allaah Anajua zaidi.






Vitambulisho:




Akram Alalaqmi