Kujifuta Maji Baada Ya Kuoga Na Kuchukua Wudhuu, Inajuzu?


562

SWALI: A.W.W. Je nikishaoga bila kujikausha maji, nikatawadha halafu ndio nikajifuta mwili kwa taulo safi, itakuwa nimetengua udhu wangu? Au ni lazima nioge, nijikaushe kwanza kabla ya kutawadha? Ahsanteni na Mwenyezi Mungu awajaze kheri.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kuoga, kutawadha na kisha kukausha maji ya mwilini mwako. Hakika kila ‘Ibaadah katika Uislamu ina utaratibu na nidhamu yake. Na wudhuu pia una utaratibu wake na vitu ambavyo vinatengua wudhuu huo. Ikiwa hakuna kitu chochote cha kutengua wudhuu basi jambo hilo litakuwa ni sawa. Tukija moja kwa moja katika swali lako ni kuwa unaweza kuoga, kisha ukatawadha na mwisho ukafuta maji na wudhuu wako utakuwa ni sahihi kabisa. Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake Al-Mughniy, anasema: “Hakuna tatizo kukausha viungo kwa kutumia taulo baada ya kuoga au baada ya Wudhuu” Haya ndio yaliyopokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah). Imepokewa pia kuwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Hasan bin ‘Aliy, ‘Aliy bin Abi Twaalib, Anas na Maswahaba wengine kuwa walikuwa wakitumia taulo kujikausha baada ya wudhuu.” Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) anasema kuwa, “Hakuna makatazo yoyote ya mtu kujikausha baada ya wudhuu. Na endapo mtu atahoji vipi kuhusu Hadiyth ya mke wa Mtume, Maymuunah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa alimletea Mtume taulo ajikaushe baada ya wudhuu na Mtume akakataa na akayapangusa maji mwilini mwake kwa mkono wake, basi jibu ni kuwa Hadiyth hiyo ina tafsiri nyingi na si kukataa kwa Mtume ni sababu kuwa haifai, bali sababu zinaweza kuwa nyingi kama vile, taulo kuwa chafu, au hakutaka kulilowesha taulo kwa maji ya mwilini mwake, au sababu zingine mbalimbali. Na kule Mke wake kumpa taulo kunaonyesha pia ni kuwa ni ada yake kuletewa taulo kujikausha nayo na kama si hivyo Mke wake asingempelekea hiyo taulo kama jambo lenyewe halifai.” Majmu’ Fatawaa Ibn ‘Uthaymiyn (11/93) Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Mtu na tabia zake