Kumpeleka Hajj Mzazi Kwa Pesa Za Hawara


405

SWALI: mimi nina mwanaume ambaye anapesa sana sasa nilitaka kumwambia anipe pesa nimpeleke mama yangu hajj ila nikasita nikaona bora niulize kwanza je inafaa? mana siendi mimi nampeleka mama yangu jekwa sababu ni mama inafaa ? mana sio muhusika wa yule bwana ntakaeenda ni mama yangu? naomba ufumbuzi wa swala hili ndugu zangu ili tuelimishane

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kabla ya kujibu Swali lenyewe khaswa, inapasa utambue kwamba kuwa na mahusiano na mwanamume asiye Mahram (maharimu) wako ni maasi na jambo ambalo halimpasi mwanamke Muislamu kufanya. Umeeleza katika swali lako kwa kauli: “mimi nna mwanamume anapesa sana….” Je dada yetu hutambui kama jambo hilo ni la aibu na ovu kabisa wewe kuwa na mahusiano na mwanamume asiyekuwa mume wako? Ingawa umefanya vizuri kutukabili kuuliza kabla ya kupokea hizo pesa, lakini hakika inasikitisha sana kuona dada zetu mko katika maasi kama hayo na hali ni wazi kabisa kuwa ni jambo la haraam. Je, unafahamu kuwa hizo pesa atakazokupa wewe kwa matumizi yoyote ya kwako itakuwa ni haraam? Chakula chako, mavazi yako na mengineyo yote yatakuwa ni haraam kwako kwani hilo ni chumo la haraam. Kisha unapopokea pesa kutoka kwa mwanaume uliye na mahusiano naye ya haraam, huoni kwamba unajiweka katika fungu la wanawake wanaojiuza miili yao? Umefikiria yote hayo? Umeyaridhia? Inapasa tutambue kwamba maamrisho ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Anaposema: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُواْ مِمَّا فِي الأَرْضِ حَلاَلاً طَيِّباً وَلاَ تَتَّبِعُواْ خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ)) (( إِنَّمَا يَأْمُرُكُمْ بِالسُّوءِ وَالْفَحْشَاء وَأَن تَقُولُواْ عَلَى اللّهِ مَا لاَ تَعْلَمُونَ)) ((Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halaal na vizuri, wala msifuate nyayo za Shaytwaan. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhaahiri)) ((Yeye anakuamrisheni maovu na machafu, na mumsingizie Allaah mambo msiyoyajua)) [al-Baqarah: 168-169] Halaal Inamaanisha: 1) Nyama iliyochinjwa kihalali 2) Rizki anayopata mtu kutoka njia ya halaal Twayyiban inaamanisha: Vyakula vilivyo vizuri vya siha, ladha, vilivyomea vizuri n.k. Tunaona kwamba Aayah ya pili yake inayotaja kuhusu su-u (maovu) wal-fahshaa (machafu) ina maana kila aina ya uovu na uchafu uliokatazwa katika dini yetu. Na ndio maana Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) Akaunganisha Aayah hiyo baada ya maamrisho Ya kula vya halaal na twayyib, kwani mtu anapokula vya haraam ikiwa ni chakula au pesa kuzitumia kwa mahitajio yoyote, humfanya mtu asiweze kumuabudu Mola wake ipasavyo kwa sababu Shaytwaan atakuwa anaandamana naye wakati wote na popote. Hivyo basi kwanza tahadhari na ukate kabisa mahusiano na huyo mwanamume haraka yasije kukupelekea katika moto wa jahannam. Ikiwa huyo mwanamume anakupenda kikweli naye ana uwezo kwanini basi asikuoe ukawa mke wake wa halaal? Huoni basi kuwa anataka kukuchezea tu kwa kutumia neema aliyojaaliwa na Mola wake katika maovu? Vile vile mwenye kula chumo la haraam asitegemee kabisa kutakabaliwa du’aa zake na Mola kwani hazikubaliki du’aa zake wala amali zake zozote azitendazo kutokana na chumo hilo la haraam kama tulivyopata mafunzo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): عن أبي هُرَيْرَةَ رَضي اللهُ عنه قال: قاَل رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم : ((إنَ الله تعالى طَيِّبٌ لا يَقْبَلُ إلا طَيِّباً، وإنَّ الله أَمَرَ المُؤمِنينَ بِمَا أَمَرَ بِهِ المُرْسَلينَ فقال تعالى: ((يا أَيُّها الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيَّباتِ واعمَلُوا صالحاً)) [المؤمنون: 51] وقال تعالى: ((يا أَيُّها الَّذِينَ آمَنُوا كلُوا مِنْ طَيِّباتِ ما رَزَقْناكُمْ)) [البقرة: 172] ثُمَّ ذَكَرَ الرَّجُلَ يُطِيلُ السَّفَرَ أشْعَثَ أَغْبَرَ يَمُدُّ يَدَيْهِ إلى السَّماءِ يا رَبُّ يا رَبُّ، ومَطْعَمُهُ حَرَامٌ، ومَشْربُهُ حَرَامٌ، وَمَلْبَسُهُ حَرَامٌ وغُذِّيَ بالحَرَامِ، فأَنَّى يُسْتَجَابُ لهُ!)). رَوَاهُ مُسْلِمٌ Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alisema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Allaah ni Mwema na Hakubali ila kilicho chema tu, Allaah Ameamrisha Waislamu kufanya yale aliyowaamrisha Mitume, na Yeye (Subhaanahu wa Ta’ala) Kasema: ((Enyi Mitume Kuleni katika vitu vyema na mfanye yaliyo sawa)) [al-Mu’minuun:51]. Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala): ((Enyi mlioamini kuleni katika vitu vyema ambavyo Tumekuruzukuni)) [al-Baqarah: 172] Kisha akataja (kisa cha yule) mtu aliyesafiri safari ndefu, kachafuka na kajaa mavumbi na huku anayanyua mikono yake mbinguni akisema “Ee Mola! Ee Mola! Nipe kadhaa, nikinge na kadhaa wakati chakula chake cha haraam, na kinywaji chake ni cha haraam, na kivazi chake ni cha haraam, na anashibishwa na haraam, je, vipi atajibiwa ([du’aa zake?])) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim] Tunshukuru kuwa umetukabili kutuuliza kabla ya kuamua kufanya jambo hilo, na hii ni dalili kwamba ni mtu mwenye kutaka kutambua haki ili ufuate. Hivyo tunatumai kuwa utapokea nasaha zetu za dhati kuhusu kujiepusha na huyo mwanamume na utajirudi haraka na kuachana naye na kufanya Tawbah ya kweli. Maelezo kuhusu Tawbah utayapata hapa: Tawbah Tukirudi katika swali lako utakuwa tayari umeshapata jibu kutokana na dalili zote tulizozinukuu hapo juu kwamba haipasi kabisa kupokea pesa za haraam na kuzifanyia jambo lolote la kheri hata kama kuwafanyia wazazi, ndugu au yeyote mwengine. Maelezo zaidi utapata katika Swali na Jibu kwenye kiungo kifuatacho: Kumlipia Gharama Za Hajj Mwanamke Aliyekuwa Na Mahusiano Naye Yasiyo Halali Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Khalifa Al Tunaiji