Kutengukwa Na Wudhuu Katika Swalah Ya Jamaa


373

SWALI: Kama unasali jamaa kati kati ukatengukwa na udhu utahitajika kuondoka pale pale au usubiri umalize then utie udhu usali tena? ukizingatia jamii yetu wengi hatujui namna ya kupishana katika sala ukitokewa na udhuru.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Swalah hili ni muhimu na linahitaji kuonyeshwa kimatendo kwani huenda lisifahamike katika waraka. Hivyo, itabidi katika Misikiti watu wafundishwe ili kusiwe na utata aina yoyote baada ya hapo. Kwani hili ni tatizo kubwa katika jamii zetu kujua namna ya kutoka pindi mtu anapotengukwa na wudhuu. Lakini Insha’Allah tujaribu na tunamuomba Allah atupatie tawfiki katika hilo. Pindi wudhuu unapovunjika inakuwa huwezi tena kuendelea na Swalah na inabidi uondoke ili ukachukue wudhuu na urudi uanze Swalah ile kuanzia mwanzo. Wudhuu unapomtenguka mmoja wetu inabidi akate Swalah na aanze harakati za kutoka ili aende kuchukua wudhuu mpya. Hapo atasimama nyuma ya mtu wa upande wa kushoto au kuumeni katika wale waliokuwa naye msitari mmoja. Na anaweza kumuashiria yule aliye katika msitari wa nyuma ili ajongee katika nafasi yake. yeye naye atapiga hatua katika ile nafasi iliyoachwa wazi kwa yule wa nyuma kujongea mbele. Atasimama tena nyuma ya mtu wa msitari huu wa nyuma. Huyu wa msitari wa tatu atakuja kuziba ule mwanya na ataendelea hivyo mpaka afike sehemu ya kuchukua wudhuu. Akiona kuwa kutoka kwake kunaweza kuleta shida zaidi na vurugu kwa wengine au kuleta tashwishi ya kuwaondolea khushuu wengine, itakuwa ni afadhali abakie amekaa katika sehemu yake mpaka jamaa imalizike kisha atoke kwenda kuchukua wudhuu mpya kwa ajili ya kuanza Swalah upya. Lakini pia kuna ushahidi mwengine uuoneshao kuwa mtu anaweza kupita mbele ya safu nyuma ya Imaam na hatokuwa amewakata wenzake Swalah, kwani katika Sahihi Al Bukhariy, (( سترة الإمام سترة من خلفه)) البخاري ((Sutra ya Imaam ni Sutra ya walio nyuma yake)) Al-Bukhariy Na maadam Maamuma kizuizi chao ni kile kizuizi cha Imaam, basi haikatwi Swalah yao kwa kupita mtu mbele yaokama tunavyoona katika tukio la Ibn ‘Abbaas رضي الله عنهما: عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما قَالَ : أَقْبَلْتُ رَاكِباً عَلَى حِمَارٍ أَتَانٍ , وَأَنَا يَوْمَئِذٍ قَدْ نَاهَزْتُ الاحْتِلامَ , وَرَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يُصَلِّي بِالنَّاسِ بِمِنًى إلَى غَيْرِ جِدَارٍ، فمَرَرْتُ بَيْنَ يَدَيْ بَعْضِ الصَّفِّ فَنَزَلْتُ, فَأَرْسَلْتُ الأَتَانَ تَرْتَعُ، وَدَخَلْتُ فِي الصَّفِّ فَلَمْ يُنْكِرْ ذَلِكَ عَلَيَّ أَحَدٌ . Imetoka kwa Ibn ‘Abbaas رضي الله عنهما ambaye kasema: “Nilikuja siku moja huku nimepanda punda mwanamke na nilikuwa ndio kwanza nafikia umri wa kubaleghe, Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anaswalisha watu huko Minaa bila ya kuweko ukuta mbele yake. Nikapita baina ya baadhi ya safu, kisha nikateremka, nikampeleka punda (sehemu ya ) kumlisha, na nikaingia katika safu, wala hakuniambia mtu lolote kuhusu hivyo nilivyofanya” Al-Bukhariy Na katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Imaam Muslim من طريق عبيد الله بن عبد الله بن عتبة أن عبد الله بن عباس أخبره أنه أقبل يسير على حمار ورسول الله صلى الله عليه وسلم قائم يصلي بِمِنى في حجة الوداع، يُصلي بالناس. قال : فَسَارَ الحمار بين يدي بعض الصف، ثم نزل عنه ، فَصَفّ مع الناس. Na katika Hadithi iliyosimuliwa na Muslim kupitia kwa 'Ubaydullaah bin Abdullaah bin 'Utbah kwamba Abdullaah bin 'Abbaas kamjulisha kuwa alifika huku kapanda punda na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kasimama anaswalisha watu alipokuwa Minaa katika Hijjatul Widaa. Akasema: Akawa anapita na punda baina ya safu, kisha akateremka akaingia katika safu (kuswali) pamoja na watu” Hadithi hizi zinatujulisha kuwa mtu anaweza kupita mbele ya safu za Maamuma kama kuna haja ya kufanya hivyo, na bila ya kuwa na makatazo yoyote juu ya hilo. Pia kuna hadithi kama hizo iliyopo kwenye Sahih Muslim ambayo Ibn ‘Abbaas رضي الله عنهما anasimulia kuwa alikuwa na nduguye juu ya kipando na wakapita mbele ya safu na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hakuwaambia chochote. Pia tunaona katika hadithi hizi kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliswali bila ya kuweko na ukuta mbele yake, kwa hiyo Swalah ya Maamuma ni kumfuata Imaam hata kama Imaam hana sutra mbele yake, na haidhuru ikiwa mtu atapita baina ya safu, kwa maana kuwa huyo mtu haikati Swalah za wanaoswali. Vile vile ingawa katika hadithi nyingine ya sahihi inayosema kuwa miongoni mwa vitu vinavyoharibu Swalah ni kupita kwa punda ikiwa atapita mbele ya Imaam au mtu anayeswali pekee, lakini hapa haikuharibu Swalah kupita punda baina ya safu. Wa Allaahu A'alam






Vitambulisho: