JIBU: AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kutumia toilet paper au karatasi, sheria iko wazi ikiwa maji yamekosekana kwani katika sheria ipo hali ya Istijmaar (kutumia mawe kujisafisha) na karatasi inachukua mahali pa mawe. Hata maji yakiwepo unaweza kujisafisha na karatasi kwanza kisha ukatumia maji ili usafi uwe mzuri zaidi, na hivyo ni bora zaidi. Lakini tena kwenye suala hilo la kutumia makaratasi, tunavyojua vyoo vilivyopo huko ni kweli hawaweki vyombo vya maji kwa ajili ya kujisafishia, lakini tunavyofahamu kuwa hakatazwi mtu kuingia na chupa yake au kikombe chake cha kutumia na kutupa ‘disposable cups’ na kutumia kwa haja yake. Kinachowazuia wengi kufanya hivyo, si makatazo, bali ni kuwaonea hayaa wazungu tu ndio kunawapelekea wengi kutafuta njia za mkato na hali hakuna dharura hiyo. Ama ikiwa hakuna maji kabisa sehemu hiyo, basi hukatazwi kutumia toilet paper. Na kama kuna maji lakini umekosa kabisa chombo cha kutumia kutekea maji na kujisafishia, basi unaweza kuzitumia hizo toilet paper na kuzichovya kwenye maji kisha ukajisafishia ili kupatikane usafi zaidi na kutakatike na kuhakikishike kuwa hakujabaki aina yoyote ya uchafu. Na Allaah Anajua zaidi