Kuvaa Kofia Ndani Ya Swalaah Au Nje Ni Sunnah?


2778

SWALI: Assalamu aleikum warahmatullahi wabarakatu, ALLAH Awajaze kheri na malipo makubwa, nauliza kuvaa kofia katika swala au nje ya swala ni katika sunnah? Tafadhali tufafanulieni. Shukran.

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu kuvaa kofia katika Swalaah au nje ya Swalaah. Kuhusiana na uvaaji wa kofia, Imaam Ibn Qayyim al-Jawziyyah amesema yafuatayo katika kitabu chake Zaad al-Ma’aad kuhusiana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Alikuwa na kilemba ambacho alimpa ‘Aliy kama zawadi, lakini alikuwa akikivaa juu ya kofia. Pia aliwahi kuvaa ama kilemba au kofia peke yake. Alipovaa kilemba, hata hivyo alikuwa akiacha ncha ya kilemba hicho ikining’inia katikati ya mabega yake mawili kwa nyuma”. Abu Daawuud amesimulia Hadiyth kutoka kwa Umm Qays bint Mihsan (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Swahaba Waabisah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alivaa kofia. Na Ibn 'Asaakir anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mara nyingine akiitoa kofia yake na kuiweka mbele alipokuwa akiswali akiifanya ni sutrah (kizuizi) yake. Hivyo, tunaona kwa haya kuwa kofia ilikuwa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo haikusisitizwa sana kwani yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati mwengine alikuwa anaivaa na pia kuivua akiwa ndani ya Swalaah au nje yake. Kwa hiyo, ukiivaa unapata Sunnah na ukitoivaa huna makosa. Na Allaah Anajua zaidi










Khalifa Al Tunaiji