Kwa Nini Watoto Waliokufa Wanaombewa Du’aa Katika Swalaah Ya Jenaza Na Hali Hawana Madhambi?


577

SWALI: Assalaam Alaykum, Tunavyoambiwa katika dini kuwa, watoto wadogo na wasiofikia baleigh akil, wakifariki huwa hawana hesabu yaani ni moja kwa moja peponi. Jee nini asili au mantiki ya kuwaombea dua kuepushwa na moto wakati ya sala ya maiti??

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kuwaombea du‘aa watoto wachanga katika Swalah ya Jeneza. Hilo ambalo ndugu yetu aliloandika si sawa kwani zipo Hadiyth nyingi kuhusu hukumu ya watoto wachanga watakaohukumiwa na Allaah Aliyetukuka. Ama suala la watoto wachanga wanachuoni waliotangulia na wa sasa wametofautiana, Allaah Awarehemu wote. Mas-ala yenyewe ni kuhusu watoto waliokufa wakiwa wachanga, ilhali wazazi wao ni makafiri: Je, hukumu yao ni gani? Na hivyo hivyo, wendawazimu, viziwi, vikongwe na wanaokufa katika Fitwrah (maumbile ya mwanaadam ya asili –Tawhiyd-), wakiwa hawajafikiwa na ujumbe, hukumu yao itakuwa ipi? Hadiyth nyingi zimepokewa katika mas-ala haya, lakini tuchukue mojawapo tu: Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kila kinachozaliwa kinazaliwa katika Fitwrah (maumbile ya mwanaadamu ya asli –Tawhiyd-), ni wazazi wake ndio wanaomfanya awe Myahudi, Mkristo au Majusi kama hayawani wanavyozaa hayawani – je waona yeyote anayezaliwa akiwa ameatilika (akiwa hana kiungo kimoja au kingine)?" Katika riwaya moja, walisema: "Ewe Mtume wa Allaah! Waonaje kuhusu wale wanaozaliwa wakiwa wachanga?" Akasema: "Allaah Anajua zaidi kwa kile ambacho wangekifanya" (al-Bukhaariy na Muslim). Mantiki hiyo ni kuwa Allaah Aliyetukuka Anajua zaidi kuwahusu wao hivyo inakuwa vyema kuwaombea kama tulivyofunzwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili waingie katika rehema ya Mola wao. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Ibrahim al-Dosari