JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Ndugu yetu katika Uislamu ilikuwa vyema useme hivi: Mimi nimedanganya na ninapata posho kwa huko kudanganya kwangu nini hukumu ya hilo posho? Hukumu yake ni kuwa si halali yako. Ndugu yetu katika Uislamu, pia ilikuwa vyema useme hivi: ‘Nina dhahabu ambazo zimefikia kiwango cha kutolewa Zakaah na ninataka kutoa Zakaah. Je, inafaa niitolee hiyo dhahabu iliyofikia kiwango, Zakaah? Hukumu yake kama dhahabu imefikia kiwango unatakiwa utoe Zakaah na kama tulivyoeleza kuwa fedha unazozipata kwa kudanganya si halali yako hivyo toa hizo dhahabu kama ni Zakaah yako. Ndugu yetuu katika Uislamu, pia ilikuwa vyema useme hivi: ‘wakimbizi na wakaazi wa hapa nilipo hupewa posho kuendesha maisha yao ya kila siku na mimi kiuhakika sina haja ya hilo posho kwani nina uwezo mkubwa hata nikawa na dhahabu; hivyo basi hilo posho analostahiki kila mkaazi asiye na kazi, kwa kuwa silihitaji hili posho nataka nipeleke kwetu na niwape watu wengine kama swadaka.’ Wenye kupewa hilo posho hupewa kwa kuwa ni katika mipango ya hapo ulipo kuwa kila mkaazi wao asiyejiweza au asiye na kazi asaidiwe. Ama wewe unajiweza na unaweza kufanya kazi hivyo basi si halali kwako hilo posho wala si halali kuwapa wengine kisichokuwa halali kwako na ukategemea malipo kwa Mola. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi: Kutoa Sadaka Na Pesa Za Kusaidiwa Na Serikali Na Zile Za Chumo La Haraam Pesa Alizozichuma Kusema Uongo Azifanye Nini? Pesa Anazopata Kwa Kuongopa Serikalini Zinafaa Kutumika Kwa Matumizi yake na kufanyia Mambo Ya Kheri? Na Allaah Anajua zaidi