JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako linalohusiana na najisi ya mkojo. Hakika swali hilo halina utata kabisa kwani tumebainishiwa na Uislamu kuhusu hilo na mengineyo. Ikiwa najisi ni mkojo wa mtoto ulioingia katika nguo utaiosha hiyo nguo yako kwa maji na ukiiosha kwa sabuni ni bora zaidi. Pindi harufu inapokuwa haipo tena tayari nguo hii itakuwa imetwaharika. Ikiwa hata mapovu ya sabuni hayajaisha lakini harufu imetoka, basi hakutakuwa na tatizo lolote unaweza kuitumia bila tatizo lolote. Na kama najisi hiyo iko sakafuni cha kufanya ni kuifuta kwa kitambaa baada ya kumwagia maji kwenye mkojo huo ulioko sakafuni au kwa kitambaa ulichokitia maji. Ukishafuta utakiosha kitambaa hicho na pindi harufu yake itakapoondoka kitambaa na sakafu vitakuwa twahara wala usiwe na wasiwasi. Kutwaharisha kitambaa si lazima kuwe na maji ya kuchuruzika. Na najisi ya mkojo haisafishwi kwa kutumia mchanga. Mchanga unatumiwa tu kuondoa najisi kwa kitu ambacho kimerambwa na mbwa, ila tu katika hali ya dharura ya kukosekana maji kabisa. Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi 003 Aina Za Najisi 009 Najisi Zinazosamehewa 010 Namna Ya Kuzitwaharisha Aina Mbalimbali Za Najisi Ambazo Matini Imekuja Kuzibainisha 011 Je, Ni Lazima (kutumia) Maji Katika Kuondosha Najisi? Au Inajuzu Kuondosha Kwa Vimiminika Vinginevyo Au Mada Nyinginezo? Na Allaah Anajua zaidi