Msafiri Anatambulikanaje Ni Msafiri Ili Afupishe Swalah na Swawm


322

SWALI: Assalam aleikum warahmatullah,baada ya salam ya kheri na baraka,kwa kweli kazi zenu zinatusaidia sana na tutazidi tuwaombea dua Allah awajalie wepesi ndani yake na awalipe pepo amin,nilikua naomba nieleweshwe kwa kirefu ni safari ipi ambayo Allah katupungizia uzito wa ibada mfano kupunguza swalah,na kutokufunga swaum,yaani nilita nielewe kama ni kua safarini mpaka utakapo fika unapoelekea ao mpaka utakapo rudi nyumbani,nawatakia kila la kheri wassalam aleikum warahmatullah

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunashukuru kwa swali lako kuhusu Swalah ya Msafiri. Wanachuoni wametofautiana kuhusu umbali ambao mtu anaruhusiwa kufupisha Swalah. Baadhi yao wamesema kuwa mtu anafupisha Swalah baada ya umbali wa kilometa 81 na kilometa 83 au maili 48 kwa makisio ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema, “Kutoka Usfaan hadi Makkah, au kutoka atw-Twaaif hadi Makkah, au kutoka Jiddah hadi Makkah.” Lakini masafa hayo yatatofautiana kutokana na chombo anachotumia mtu kusafiria; inaweza kumchukua mtu masaa kufika kama anatumia ndege, na mwengine kumchukua siku mbili kama ilivyokuwa ikiwachukua Maswahaba kama inavyoonyesha mitazamo ya Ibn ‘Abbaas mwenyewe, Ibn ‘Umar na pia waliokuja baadaye kama Maimaam Maalik na Al-Layth na Ash-Shaafi’iy. Wengine wameonelea kuwa safari yoyote ile inayotambulikana na ada na jamii kuwa ni safari basi mtu atafupisha Swalah yake japo haijatimia kilometa 81, 82 au 83, au japo safari yenyewe ni fupi. Mtazamo huo wa pili ndio unaoelekea sahihi zaidi kwani una dalili zenye nguvu zaidi ingawa unaweza kuwa na ugumu kutekelezeka kwa baadhi ya watu, kwani kuna wengine wanaweza kuona umbali fulani kuwa ni safari na wengine wakaona si safari. Mtazamo huu dalili zake ni kuwa hakuna pahala Allaah wala Mtume Wake wameeleza kipimo cha safari. Pia Hadiyth ya Anas bin Maalik ambayo amesema: “Alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisafiri kwa umbali wa masafa ya maili tatu au farsakh tatu, alikuwa akiswali Rakaa mbili.” Muslim Pamoja na kuwa mtazamo wa pili ndio ulio sahihi zaidi, lakini wengi wameona mtazamo wa kwanza wa kusafiri kwa kuhesabu kilometa kuwa ni mwepesi zaidi kwao kuutekeleza. Ikiwa watu watakubaliana kuunganisha mitazamo yote hiyo miwili pamoja, basi hakutakuwa na tatizo na utata. Kilicho bora ni mtu kuwa katika mtazamo wa salama zaidi kwa Dini yake. Kwa vipimo hivyo, mtu anaweza kuswali Swalah ya safari, na pia anaruhusiwa kutokufunga. Na suala la kufunga ni rukhsa na pendekezo la kisheria kwa Msafiri japo baadhi ya Madh-hab yanaona kuwa si suala la khiyari bali ni waajib kwa Msafiri uacha kufunga, lakini mtu atatazama safari yenyewe na mazingira mazima ya safari yenyewe kama anaweza kufunga au la! Ila sheria imemruhusu kuacha kufunga anapokuwa safarini. Kinyume na Swalah ambayo msafiri hata akifika anapokwenda anaweza kuendelea kufupisha Swalah, kufunga, mtu anapofika kwenye mji anaoudhamiria, basi anaendelea kufunga kwani yale mashaka ya kufunga akiwa safarini hayatakuwepo tena. Suala la muda wa kufupisha Swalah ni suala lenye kutofautiana baina ya Wanachuoni. Wengi wakiwemo Maimaam wanne na wanachuoni wa karibuni kama Shaykh Ibn Baaz wameonelea ni siku nne mtu anaruhusiwa kufupisha Swalah na baada ya hapo ataswali kikamilifu, badala ya kuswali mbili mbili zile Swalah za Rakaa nne nne, atatakiwa aziswali nne kikamilifu. Hawa waliona hivyo, wamechukulia dalili yao kwa ufupishaji wa Swalah wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda Makkah kwa kufanya Hajj yake ya kuaga (ya mwisho kabla ya kufariki kwake), na alikaa siku ya nne ya tano ya sita na ya saba akifupisha Swalah zake na siku ya nane aliswali Swalah yake ya Alfajr sehemu iitwayo Al-Abtah. Wengine kama Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah na Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn na wengineo wameonelea kuwa mtu maadam atakuwa hajaweka niyah ya kukaa masiku maalum alipokwenda kwa shughuli zake, ziwe ni za kibiashara, matibabu, au hata jihaad n.k. basi anaweza kufupisha kwa muda atakaokuwepo hapo. Na dalili yao ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda Makkah katika kuukomboa mji huo mtakatifu, alifupisha Swalah kwa muda wa siku 19, na pia alipokuwa Taabuuk kupigana na wakristo alikaa kwa siku 20 na siku zote hizo akifupisha Swalah kwani alikuwa hajaweka niyah ya kukaa muda wote huo na pia alikuwa hajamaliza kilichompeleka huko. Wengineo wakaenda mbali na kuonelea kuwa mtu anaweza kufupisha Swalah muda wowote ule atakapokuwa ugenini japo ni miaka na miaka. Hao wamechukulia dalili yao kuwa Maswahaba kama Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alifupisha Swalah kwa muda wa miezi sita alipokwenda Azerbeijan. Hata hivyo, hali hiyo ya Swahaba Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ya kufupisha alipokwenda huko Azerbeijan si hali ya kupenda kwake au kimatembezi, bali alikwama kuingia huko Azerbeijan kutokana na barafu nyingi iliyokuwepo. Na hali hiyo ni kinyume na baadhi ya watu wanaochukulia dalili hiyo kwa kuhalalisha kufupisha kwao walipo ugenini kimatembezi, likizo, kimaisha au kiukimbizi na hali hawana malengo ya kurejea makwao. Hivyo, msimamo wa usalama zaidi ni ule wa siku nne ambao ndio msimamo unaomuweka Muislam pema na kutumbukia na mtazamo ambao unaweza kumkosesha kheri nyingi na pia fadhila mbalimbali kama za Swalah kamili na Swalah za Jama’ah. Kujibu kipengele chako cha mwisho, kuwa safari inahesabiwa atakapokwenda au hadi atakaporudi, jawabu ni kuwa huhesabiwa kuanzia anapokwenda hadi atakaporejea. Kwa ziada tu, mtu hufupisha Swalah anapokuwa ametoka nje ya mji wake au atakapofika masafa ya kuwa Msafiri. Na hawezi kuanza kufupisha Swalah akiwa bado yupo mjini kwake, na pia hawezi kufupisha Swalah baada ya kurejea kutoka safari japokuwa kuna Swalah imeingia hali ya kuwa yeye bado ni msafiri na hajaiswali hadi alipofika kwake. Kufunga pia kunaingia katika hali hiyo hiyo. Na wanachuoni na Maimaam wameonelea kuwa msafiri kama anaona safari anayosafiri haina mashaka na hakutakuwa kuna uzito wala ugumu kwake kufunga, basi ni bora kwake kufunga kwa sababu nyingi mbalimbali, kwani kuna ushahidi mbalimbali kuwa Mtume mwenyewe alifunga na hata Maswahaba walifunga wakiwa safarini, kufunga kunamfanya mtu aweze kuitekeleza fardhi ile klwa wakati wake kuliko kuja kuilipa baadaye na kuwa ngumu, na pia kufunga wakati watu wanafunga (Ramadhaan) ni wepesi kuliko mtu kuja kufunga peke yake, na pia, kutekeleza nguzo hiyo katika mwezi huo wenye Baraka kuna ubora kuliko kuitekeleza katika miezi mingine isiyo hiyo. Na hiyo ndio rai ya Wanachuoni wengi wa sasa na wa zamani kama Imaam Ash-Shaafi’iy. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Salah Al Hashem