JIBU: AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu damu ya nifasi. Hakika ni kuwa nifasi ni damu inayotoka katika tupu ya mbele ya mwanamke baada ya kuzaa, wala hapana mpaka wa uchache wake, kwani wakati wowote atakapoona mwenye nifasi twahara, ataoga na ataswali na hata kuingiliwa na mume wake. Kwa hiyo, muda wako mfupi inawezekana baada ya masaa ya kuzaa kwake ikiwa damu hiyo itakatika. Ama muda wake mrefu ni siku 40 kulingana na Jamhuri ya wanazuoni ingawa kuna waliosema siku 60. Amesema at-Tirmidhiy: “Wamekubaliana wanazuoni kuanzia kwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Tabiina na waliokuja baada yao kuwa mwenye nifasi anaacha Swalah kwa siku 40 ila akitwahirika kabla ya hapo. Ikiwa ni hivyo atajitwahirisha na kuswali (Sunan at-Tirmidhiy). Mj. 1, uk. 258). Pia ipo Hadiyth iliyopokewa kuwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) alisema: “Alikuwa mwanamke mwenye nifasi anakaa siku arobaini”. Na amesema nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) muda gani anakaa mwanamke pindi akizaa? Akasema: “Siku arobaini ila atakapoona twahara kabla ya hapo” (at-Tirmidhiy, na ameisahihisha al-Haakim). Ikiwa damu yenyewe itapita siku 40 basi hiyo itakuwa ni damu ya ugonjwa inafaa mwenye kuona hivyo baada ya muda huo aoge na ni lazima kwake kufunga na kuswali. Na Allaah Anajua zaidi