JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Kuoga josho (ghuslu) la janaba ni waajib kwa Muislamu kwani ni amri kutoka kwa Muumba wetu Mtukufu Ambaye Hatoi sheria ya kumkaflisha mja ila iko katika uwezo wake kutekeleza. Juu ya hivyo sheria zake zote ni za kheri kwetu, zenye hikma na na manufaa yanaturudia sisi wenyewe. Anasema Subhaanahu wa Ta’ala katika sheria ya kufanya ghuslu: ((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُواْ بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَينِ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُواْ وَإِن كُنتُم مَّرْضَى أَوْ عَلَى سَفَرٍ أَوْ جَاء أَحَدٌ مَّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لاَمَسْتُمُ النِّسَاء فَلَمْ تَجِدُواْ مَاء فَتَيَمَّمُواْ صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُواْ بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ مَا يُرِيدُ اللّهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَكِن يُرِيدُ لِيُطَهَّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ)) ((Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Allaah kukutieni katika taabu; bali Anataka kukutakaseni na kutimiza neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru)) [Al-Maaidah: 6] Tunaona kutokana na Aayah hiyo kwamba ruhusa imetolewa ya kutokuoga kwa mtu mgonjwa ambaye anakhofia kuwa maji yatamdhuru, au aliyekuwa safarini na hakupata maji. Hapo ndipo anapopasa kujitia twahara kwa kutumia mchanga kutayamamu. Nasi hatuoni kuwa hilo ni tatizo kwani wangapi wanaoishi nchi za baridi na pengine kuna baridi zaidi ya nchi unayoishi wewe lakini hawaachi kutimiza waajib huo. Bila ya shaka kuna maji ya moto, hivyo hakuna sababu ya kukufanya ushindwe kuoga wakati wowote ule. Na tambua kwamba kujitia twahara katika hali ya shida ni alama ya Iymaan ya Muislamu. Hivyo inakupasa ujitie twahara vizuri ya ghuslu kama ipasavyo na kama ilivyoelezewa katika jibu lifuatalo na haipasi kufanya wudhuu pekee katika kujitia twahara ya janaba. Ghuslu - Vipi Kukoga Janabah, Nifaas Na Hedhi Na Allaah Anajua zaidi