Nguzo Ya Hajj Itekelezwe Mara Ngapi Kishari#039;ah?


461

SWALI: as.kum hijja mafrudh ni faradhi kwa mwenye uwezo jee hajj hasa ni mara ngapi mbona watu wanakwenda zaidi ya mara 1inakuaje?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Nguzo ya Hijjah imefaridhiwa kwa Waislamu katika Qur-aan kuitekeleza mara moja tu katika umri wao na hivyo atakapofanya mtu mara moja tu, atakuwa ameshakamilisha nguzo yake na kupata fadhila zake zote. Na juu ya hivyo nguzo hii haikufaridhiswa ila kwa mwenye uwezo tu. Anasema Allaah (SubhaanahuWa Ta'ala): ((وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً)) ((Na kwa ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea)) [Al-'Imraan: 96-97] Na Anasema Allaah (SubhaanahuWa Ta'ala): ((وَأَتِمُّواْ الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلّهِ)) ((Na timizeni Hijjah na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah)) [Al-Baqarah: 196] Ikiwa Hajj si lazima kwa asiye na uwezo ni dhahiri kuwa mwenye uwezo inamtosha kuitekeleza mara moja na kuhesabika kuwa katimiza fardhi yake kama tulivyoona katika Aayah juu. Hata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametekeleza nguzo hii mara moja katika maisha yake. Na alipofaridhisha nguzo hii katika Sunnah alikuja mtu kumuuliza kama inapasa kufanya Hajj kila mwaka, maelezo katika usimulizi ufuatao yanatupa majibu: عن أبي هريرة قال : خطبنا رسول الله صلى الله عليه وسلم فقال: ((أيها الناس قد فرض الله عليكم الحج فحجوا)) ، فقال رجل : "أكلَّ عام يا رسول الله ؟" فسكت حتى قالها ثلاثا ، فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم(( : لو قلت نعم لوجبت ولما استطعتم)) ، ثم قال : ((ذروني ما تركتكم فإنما هلك من كان قبلكم بكثرة سؤالهم واختلافهم على أنبيائهم فإذا أمرتكم بشيء فأتوا منه ما استطعتم وإذا نهيتكم عن شيء فدعو)) رواه مسلم Kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesema: “Alitukhutubia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Enyi watu Allaah Amekufaridhisheni Hajj hivyo mhiji)). Mtu mmoja akasema: Kila mwaka ewe Mjumbe wa Allaah? Akanyamaza kimya (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi yule mtu aliporudia mara tatu [swali lake] akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ningelisema ndio, ingeliwajibika, na wala msingeliweza)). Kisha akasema ((Niacheni kwa yale niliyokuachieni kwani watu wa kabla yenu waliangamia kwa maswali yao mengi na ikhitilaaf zao [kujadiliana sana kwao] na Mitume yao. Hivyo nnapokuamrisheni jambo lifanyeni muwezavyo na nnapokukatazeni jambo jiepusheni)) [Muslim] Vile vile: عن ابْنِ عَبَّاسٍ أَنَّ الأَقْرَعَ بْنَ حَابِسٍ سَأَلَ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ : يَا رَسُولَ اللَّهِ الْحَجُّ فِي كُلِّ سَنَةٍ أَوْ مَرَّةً وَاحِدَةً ؟ قَالَ : ((بَلْ مَرَّةً وَاحِدَةً ، فَمَنْ زَادَ فَهُوَ تَطَوُّعٌ)) رواه أَبُو دَاوُد وصححه الألباني Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Al-Aqra’ bin Haabis alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Ewe Mjumbe wa Allaah, je, Hijjah ni kila mwaka au mara moja tu? Akasema: ((Ni mara moja lakini mwenye kupenda kuzidisha ni tatwawwu’ [kujitolea na anapata ujira wake])) [Abu Daawuud na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh al-Albaaniy] Tunafahamu katika usimulizi huo ulio Swahiyh kwamba mwenye uwezo wa kufanya zaidi ya mara moja (Hajj au ‘Umrah) anaweza kufanya, kwani ni katika kutafuta fadhila zake nyingi na tukufu kama tulivyopata mafunzo katika simulizi mbali mbali, tunazinukuu baadhi yake: Kufanya ‘Umrah katika Ramadhaan ni sawa na Hajj: (( عمرة في رمضان تعدل حجة )) أخرجه البخاري و مسلم (('Umrah katika Ramadhaan ni sawa [kwa thawabu] na Hijjah)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Baina ya Hajj na Umra ni kufutiwa madhambi: ((العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما، والحج المبرور ليس له جزاء إلا الجنة)) البخاري ((‘Umrah hadi ‘Umrah [nyingine] ni kafara [kutufiwa dhambi] baina yake, na Hajjum-Mabruur haina jazaa isipokuwa ni Pepo)) [Al-Bukhaariy] Vile vile: عن إبن مسعود قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((تابعوا بين الحج والعمرة فإنهما ينفيان الفقر والذنوب كما ينفى الكير خبث الحديد والذهب والفضة وليس للحج المبرور ثواب دون الجنة)) سنن النسائي و أحمد والترمذي بإسناد حسن Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Fuatilieni Hajj na ‘Umrah kwani hizo (mbili) zinaondosha ufakiri na madhambi kama kinavyoondosha chombo cha kupulizia moto uchafu wa chuma na dhahabu na fedha, na Hajj Mabruur (Hajj iliyotakabaliwa) jazaa ya thawabu yake hakuna zaidi ya Pepo)) [Sunan An-Nasaaiy, Ahmad na At-Tirmidhiy ikiwa na isnaad Swahiyh] Miongoni mwa vitendo bora kabisa: عن أبي هريرة أن رسول الله صلى الله عليه وسلم سئل أي العمل أفضل ؟ فقال : ((إيمان بالله ورسوله)) قيل : ثم ماذا ؟ قال : ((الجهاد في سبيل الله)) قيل : ثم ماذا ؟ قال : ((حج مبرور)) رواه البخاري ومسلم Kutoka kwa Abu Hurayrah kwamba aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Kitendo gani bora kabisa? Akasema: ((Kumuamini Allaah na Mjumbe Wake)) Akulizwa: Kisha nini? Akasema: ((Jihaad katika njia ya Allaah)) Akaulizwa: Kisha nini? Akasema: ((Hajjum-mabruur [Hajj iliyotakabaliwa])) [Al-Bukhaariy na Muslim] Kufutiwa dhambi zote عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : سمعت النبي صلى الله عليه وسلم يقول : ((من حج لله فلم يرفث ولم يفسق رجع كيوم ولدته أمه)). رواه البخاري ومسلم Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayefanya Hajj asitoe maneno machafu wala asitende vitendo vichafu atarejea kama siku aliyozaliwa na mama yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Lakini ni vizuri Muislamu aliyekwishatimiza Hajj kuwafikiria ndugu zake waliokuwa bado hawakujaaliwa kutekeleza nguzo hii na badala ya kwenda yeye zaidi ya mara moja amsaidie ndugu yake ili aweze kutekeleza naye nguzo hii. Walio muhimu zaidi kusaidiwa kutekeleza nguzo hii na wazazi wawili kwani itakuwa ni katika kuwafanyia wema wazazi, ambayo ni moja ya amri tuliyoamrishwa na kusisitizwa sana. Juu ya hivyo itakuwa ni kupata radhi zao. Pia kutokana na zahma zinazozidi kila mwaka ya mamilioni ya watu kwenda Hijjah, kutokurudia Hijjah itapunguza zahma hizo na kuwapa fursa ndugu wengine ambao hawakutekeleza bado nguzo hii kwani kama tunavyojua kuwa Serikali na wasimamizi wa Hijjah wanatoa idadi fulani tu ya watu kila nchi kwenda kutekeleza nguzo hii na sasa hivi kwa miaka kadhaa wameanzisha utaratibu wa kutoruhusu aliyefanya Hajj asiende tena hadi baada ya miaka kadhaa ili wengine wapate nafasi. Hatuna uhakika kama utaratibu huo unafuatwa vizuri na nchi wanazotoka mahujaji au na hao watoaji visa. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho: