Siku Ngapi Inahesabika Kuwa Ni Msafiri Hata Afupishe Swalaah?


408

SWALI: Asalam aleykum, swali langu ni hili, ni siku ngapi msafiri anaweza kuswali swalah za mkato?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu idadi ya siku zinazohesabika kuwa mtu bado ni msafiri. Kwa vile Uislamu ni njia pekee kamili na sahihi ya maisha, basi unawafikiria Waumini na hali zao katika mazingira tofauti. Na kwa vile safari zina mashaka, misukosuko na taabu, Uislamu umemsahilishia mambo msafiri upande wa Swalah. Hivyo ukiwa safarini swali rak’ah mbili badala ya nne katika Swalah ya Adhuhuri, Alasiri na ‘Ishaa. Ama Magharibi na Alfajiri hazipunguzwi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuambia: “Na mnaposafiri katika ardhi si vibaya kwenu kama mkifupisha Swalah” (an-Nisaa’ 4: 101). Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hii ni neema ya Allaah kwenu, basi ipokeeni kwa shukrani” (al-Bukhaariy na Muslim). Msafiri anaweza kufupisha Swalah njiani akiwa safarini hata muda ukiwa mwingi namna gani. Ama anapowasili katika mji aliokuwa anakwenda, ni muda gani ataruhusiwa kukusuru? Jawabu ni kuwa idadi ya siku ambazo msafiri anaruhusiwa kukusuru kuna tofauti baina ya wanachuoni kwani hakuna Hadiyth iliyo wazi ya kukata idadi za siku kuhusu suala hilo. Hadiyth nyingi zimeashiria idadi mbalimbali. Kuhusu suala hili zipo kauli kumi na moja, lakini zilizo mashuhuri ni nne, nasi ndio tutazitaja. Kauli hizo ni kama zifuatazo: 1. Akitia Niyah Ya Kuketi Zaidi Ya Siku Nne Hatokusuru: Hii ni kauli ya madhehebu ya Maalikiyah, Shaafi‘iya na Hanaabilah isipokuwa Maalikiyah na Shaafi‘iya wamesema siku bila ya kuhesabu ya kuingia na kutoka. Na Hanaabilah wameweka Swalah ishirini na moja. Dalili yao kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia Makkah asubuhi ya tarehe 4 Dhul Hijjah, akaketi ndani yake tarehe nne, tano, sita na saba. Na akaswali Swalah ya Asubuhi siku ya pili, kisha akatoka akaenda Minaa, naye alikuwa akikusuru katika siku hizo. Naye alikuwa amenuia kukaa (al-Bukhaariy na Muslim). Hata hivyo, huu sio muda wa juu wa kuketi, kwani imethubutu kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliketi zaidi ya siku hizo na alikuwa anakusuru. 2. Akinuia Kuketi Siku Kumi Na Tano Hatokusuru: Na hii ni kauli ya Abu Haniyfah, ath-Thawriy na al-Muzaniy. Miongoni mwa dalili zao ni Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuelekea Makkah kutoka Madiynah. Naye alikuwa akiswali rak’ah mbili mbili mpaka tuliporudi Madiynah. Aliulizwa: “Je, muliketi Madiynah?” Akajibu: “Tuliketi siku kumi” (al-Bukhaariy na Muslim). Hadiyth nyingine ni ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: Aliketi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Makkah mwaka uliotekwa siku kumi na tano akikusuru Swalah (Abu Daawuud na Ibn Maajah). Hadiyth hii kwa lafdhi yake hiyo ni dhaifu, iliyo sahihi kutoka kwake Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ni siku kumi na tisa (al-Bukhaariy). 3. Msafiri Anakusuru Daima Maadamu Hana Niyah Kuketi Hapo Milele: Haya ni madhehebu ya al-Hasan, Qataadah, Is-haaq na akaichagua kauli hii Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah. Dalili zao ni Hadiyth zifuatazo: Imepokewa na Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliyesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliketi siku kumi na tisa akikusuru Swalah. Nasi tunaposafiri tukaketi siku kumi na tisa hukusuru, na zikizidi tunakamilisha (al-Bukhaariy). Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliketi Taabuuk siku ishirini akikusuru Swalah (Ahmad na Abu Daawuud, na kusahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy). Wenye rai hii wanaona kuwa hakika ya msafiri haifungwi na muda maalumu kwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikusuru siku kumi na tisa na ishirini, kwa kuwa alikuwa msafiri. Kwa madhehebu wenye kauli hizi tatu za mwanzo ni kuwa msafiri akiketi kwenye mji wowote ule bila ya kuwa na Niyah ya kuketi na hajui ni lini ataondoka au lini haja yake itamalizika ndani yake basi atakusuru Swalah mpaka atakapoondoka. Hii ni kwa mujibu wa matendo yafutayo: ‘Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliketi Adhrabayjaan miezi sita theluji ikiwa imedumu kwao, naye alikuwa akiswali rak’ah mbili’ (Ahmad na al-Bayhaqiy). Na pia Abu Waa’il amesema: Tulikuwa pamoja na Masruuq miaka miwili katika mji wa Silsilah, akiwa anafanya kazi akatuswalisha rak’ah mbili mpaka tulipoondoka (Ibn Abi Shaybah na ‘Abdur-Razzaaq). 4. Msafiri Anakusuru Siku Ishirini Pamoja Na Masiku Yake, Kisha Anatimiza Baada Ya Hapo, Akiwa Amenuia Kuketi Au Hakunuia: Na hii ni madhehebu ya Ibn Hazm, na akafuatwa na ash-Shawkaaniy. Dalili zao ni zile dalili zilizotumia na kundi la tatu hapo juu. Wanasema maadamu hapana dalili zinazo onyesha kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikusuru zaidi ya siku ishirini, basi kiwango cha idadi ya kukusuru ni siku hizo tu. Muhtasari wa mambo ni kuwa ikiwa Muislamu aliyekwenda mji au nchi nyingine, amechukua maskani akatia fanicha na vyombo vingine vya nyumba na akaishi akiwa na utulivu kimaisha, huyu anakuwa ni mkaazi haruhusiwi kishari’ah kukusuru Swalah, si siku nne wala zaidi ya hizo. Ama yule ambaye atafika sehemu lakini asihisi uhuru na utulivu kama ilivyo katika sehemu yake ya maisha, na hajaamua wala kujua atakuwa hapo kwa muda gani, basi huyu atakuwa ni msafiri, anaruhusiwa kukusuru maadamu yu hali hiyo hata ikiwa ni zaidi ya siku ishirini. Lakini isiwe kama wale waliotoka Afrika na kukimbilia Ulaya, Marekani na hata baadhi ya nchi Arabuni wakifupisha Swalah maisha yao yote wakizaa vizazi kwa vizazi kwa kigezo cha kudai kuwa madhehebu yao inaruhusu! Hakuna Swalah ya safari kwa mkazi aliyestakiri sehemu na kuishi maisha yake yote hapo. Hakuna Mwanachuoni yeyote wa kuaminika aliyetowa Fatwa ya aina hiyo. Bali tunaona wengi wanaofanya hivyo ni wale wavivu na wasiotilia uzito mas-ala ya Swalah na Dini kwa ujumla. Bonyeza viungo vifuatavyo upate manuaa zaidi: Swalah Ya Safari Ya Mtu Anayeishi Katika Nchi Muda Mrefu Msafiri Anatambulikanaje Ni Msafiri Ili Afupishe Swalah na Swawm Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Wema wa Amani