Swalaatul-Masbuwq - Anapokosa Rak’ah Katika Swalaah Ya Jamaa’ah Afanyeje? Anatakiwa Asome Suwratul Faatihah Na Suwrah Ndogo Katika Raka’ah Alizozikosa


266

SWALI:Swalaatul-Masbuwq - Anapokosa Rak’ah Katika Swalaah Ya Jamaa’ah Afanyeje? Anatakiwa Asome Suwratul Faatihah Na Suwrah Ndogo Katika Raka’ah Alizozikosa

JIBU: AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. Swalaatul Masbuwq au Swalaah ya aliyetanguliwa au aliyechelewa Rak'ah na Imaam, ni pindi pale mtu ameingia Msikitini akamkuta Imaam tayari kaishasw ali baadhi ya Rak'ah; aidha moja au mbili au zaidi. Dalili ya hilo ni Hadiyth iliyopokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: "Anayeidiriki Rak'ah katika Swalaah, basi kaidiriki Swalaah" [Al-Bukhaariy na Muslim]. Kuipata Swalaah ya Jamaa'ah kunahesibika pale tu unapoiwahi japo Rak'ah moja na Imaam, kwa maana unapowahi kurukuu pamoja na Imaam. Hii ndio rai yenye nguvu. Endapo utakosa Rak'ah na Imaam japo moja, ukamkuta yuko kwenye Tashahhud au baada ya hapo, utahesabika kuwa umeikosa Jamaa'ah. Hivyo, kuna umuhimu mkubwa wa Muislamu kuharakisha kuwahi Msikitini kabla ya wakati wa Swalaah kuanza au kabla ya kukimiwa ili aweze kuipata Jamaa'ah na Imaam. Jambo jingine muhimu la kukumbushana ambalo wengi wanalielewa kimakosa au wanaghafilika nalo, ni pale mtu anapoingia Msikitini akamkuta Imaam anasujudu au amekaa kikao cha Tahiyyaatu, baadhi ya watu husubiri na hawafungi Swalaah wakimngojea Imaam anyanyuke juu ndio wajiunge naye! Hili ni kosa na watu wanapaswa wajiepushe nalo. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth aliyosimulia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Pindi utakapokuja kwenye Swalaah, ukatukuta tunasujudu, basi nawe sujudu (lakini) haitohesabiwa (kama ni Rak'ah), na yeyote atakayeipata Rak'ah, basi ameipata Swalaah." [Abu Daawuwd] Na katika Hadiyth nyingine iliyosimuliwa na Mu'aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Anapokuja mmoja wenu Msikitini na Imaam yupo katika sehemu yoyote ya (Swalaah yake), basi afanye kama Imaam anavyofanya (amfuate)." [At-Tirmidhiy, na Shaykh Al-Albaaniy kasema ni sahihi] Tukirudi kwenye swali lako kuhusu Swalaatul Masbuwq, unasema umechelewa Swalaah ya Adhuhuri ukamkuta Imaam yuko Rak'ah ya pili na wewe imekupita Rak'ah ya kwanza, utakachofanya ni baada ya Imaam kutoa salaam zote mbili, wewe usitoe salaam bali utanyanyuka na utakamilisha ile Rak'ah uliyoikosa kwa kusoma Suwratul-Faatihah peke yake kwani hiyo kwako ni Rak'ah ya nne. Kuhusu Masbuwq kusoma Suwrah ndogo ni kama ifuatavyo: Mfano, umekosa Rak’ah mbili za mwanzo katika Swalaah ya Adhuhuri au Alasiri au ‘Ishaa, basi unaposwali na Imaam zile Rak'ah zake mbili za mwisho, kwako wewe hizo zinahesabika kuwa ni Rak’ah zako za mwanzo. Utakachotakiwa kufanya hapo nyuma ya Imaam, ni kusoma Suwratul-Faatihah na Suwrah ndogo pindi ikiwezekana yaani bila ya kumkhalifu Imaam kwa kuchelewa kurukuu naye pale anapokwenda kurukuu. Na zile Rak'ah mbili unazoziswali baada ya Imaam kutoa salaam, kwako ni zinahesabika kuwa ni Rak'ah ya tatu na ya nne. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Mohammed Al-Muhasny - Quran Downloads