JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Hakuna Swalah za Sunnah hasa za usiku isipokuwa ni Sunnah ya Tahajjud, nazo ni kuswali Rakaa mbili au nne, au sita, au nane na kumalizia na Rakaa tatu za Witr. Wala hakuna Swalah hasa ya usiku wa Alkhamiys kuamkia Ijumaa au siku yoyote katika wiki. Na kusoma Surah hizo au kutaja majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) pia hakuna dalili yoyote iliyokuja kutufundisha kuzisoma Surah hizo na majina kwa idadi yoyote. Uzushi mwingi wa ibada unazushwa na wengi wasiojua ambao hufuata bila ya kuchunguza kwanza wala kuwa na elimu sahihi. Mara nyingi ibada hizo hutaja idadi kubwa ya kusoma Surah au dhikr fulani kama kutaja majina ya Allah, au tasbiyh kama alivyouliza muulizaji wa Swali la pili. Uzushi unafika kusema 'soma Suratul-Baqarah mara tatu' au 'soma Surat Yaasiyn mara nne' au 'soma Qul-Huwa Allahu Ahad mara elfu'. Uko wapi huo muda wa mtu kukaa kusoma sura zote hizo? Hatuoni kuwa huku ni kujitia mashaka tu ya kufanya ibada ngumu kama hizi ambazo hazina thamani yoyote? Ibada zetu zilizothibiti ni nyepesi kabisa, lakini watu wamezifanya ni ngumu kwa kuzua uzushi mwingi kama huu. Nasiha yetu ni kwamba kabla ya kufanya ibada yoyote ni vizuri kuhakikisha kama ni sahihi. Kisha tumia wakati wako huo kufanya ibada ambazo hazina shaka kabisa na hakika zitakupatia thawabu. Kama hizi zifuatazo: 1. Kusoma Qur-aan na kujitahidi kukhitimisha kwa mwezi mara moja au zaidi ya hivyo. Kila herufi utakayosoma katika Qur-aan ni thawabu mara kumi. 2. Soma tafsiri ya Qur-aan upate kujua maana ya maneno ya Mola wako, nayo ina fadhila kubwa kufahamu Qur-aan. 3. Anza kuhifadhi Qur-aan ikusaidie katika Swalah yako, na pia kuhifadhi Qur-aan kuna fadhilia kubwa kwani siku ya Qiyaama utapandishwa daraja ya Pepo kwa kila Aayah uliyoihifadhi. 4. Fanya adhkaar zilizothibitika ambazo zote utazipata katika kitabu cha 'Hiswnul-Muslim' kinachopatikana katika kiungo kifuatacho humu AL HIDAAYA: Hiswnul Muslim – Kinga Na Nyiradi Za Qur-aan Na Sunnah 5. Sikiliza mawaidha ambayo ni njia bora kabisa ya kukuongezea elimu yako na pia kuzidisha imani yako ya dini. 6. Soma vitabu vya dini, kama vya Hadiyth za Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na vitabu vingi vya dini vimejaa. Hii ni kuongeza elimu ya dini yako ambayo pia ina fadhila kubwa. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuzindue na kila uzushi na yote yaliyo batili na Atuonyeshe yaliyo haki na Atuwezeshe kuyafuata. Na Allaah Anajua zaidi