Swawm Katika Nchi Za Baridi Zenye Nyakati Fupi.


375

SWALI: Kulikuwa na suali linanikakanja nomba fatwa. Hivyo katika mijin ya baridi ambayo wakati mwengine mchana hufika saa sita za usiku na kunapambazuka saa tisa alfajiri huwa wanafungaje?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu mas-ala ya funga katika nchi ambazo ni za baridi ambazo masika yanabadilika na masaa ya mchana au usiku yanakuwa mengi kuliko nchi zetu za Afrika Mashariki. Ibadah zote katika Uislamu zina misingi, masharti na mpangilio maalumu. Kuhusu Swalah, Allah Aliyetukuka Anatueleza: “Kwa hakika Swalah kwa Waumini ni Faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi” (4: 103). Na umuhimu wa kutunza wakati umeelezewa na Mtume wa Allah (Swalla Llaahu ‘Alayhi wa Sallam) pale alipoulizwa: “Ni amali ipi aipendayo zaidi Allah?” Akasema: “Kuswali Swalah katika nyakati zake” (al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy). Nyakati za Swalah alifundishwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi wa Sallam) pale alipoamuriwa kuswali siku mbili na Jibril (‘Alayhis Salaam). Swalah ya Adhuhuri ni pale kivuli kikiwa ni sawa na kitu chenyewe na Swalah ya Alasiri kivuli kinakuwa mara mbili ya kitu chenyewe. Swalah ya Maghrib ni wakati jua linapozama na wakati wa Alfajiri ni baada ya asubuhi ya kweli na kabla ya kuchomoza jua. Ama kuhusu swali lako la funga, Allah Aliyetukuka Anatuelezea kuhusu nyakati za mtu kufunga na kufungua: “Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa Alfajiri katika weuzi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku” (2: 187). Hiki ni kipindi ambacho mtu aliyefunga hafai kula kabisa, kuanzia kabla ya Swalah ya Alfajiri kidogo mpaka jua linapozama wakati wa kufungua aliyefunga. Masaa ya funga yatatofautiana katika nchi ambazo zina masika tofauti – baridi na joto. Inafahamika kuwa katika nchi hizo ikiwa ni nyakati ya baridi basi usiku unakuwa mrefu kupita kiasi, hivyo mwenye kufunga atafunga masaa kidogo zaidi. Hata hivyo, wakati wa joto mchana unakuwa mrefu, na mfungaji anafunga masaa mengi kupita kiasi. Kwa hiyo katika nchi hizo nyakati zao za funga zitakuwa ni kulingana na machomozo ya jua na kukuchwa kwake vile inavyofanyika katika nchi za Afrika Mashariki. kama Hekima anaijua Mwenyewe Allah Aliyetukuka, lakini ni wazi kuwa Muislamu ambaye anaishi katika nchi hizi anakuwa ni mwenye kupata uzoefu wa kufunga masaa mengi na katika hali ya joto kali, hivyo kuweza kuwa na subira. Pia wakati mwengine anafunga kwa masaa machache lakini katika hali ya baridi kali ambayo hukwaruzwa matumbo yake, hivyo kuwa na subira vile vile. Tunamuomba Allah Aliyetukuka Atufanikishie mambo yetu na Atupatie tawfiki katika kutekeleza Ibadah Zake. Na Allah Anajua zaidi






Vitambulisho:




KUUMBWA NA KUKIRIMIWA KWA MWANADAMU