Swawm Ya Nabii Daawuud Ukianza Kufunga Lazima Uendelee Haifai Kuacha?


298

SWALI: Swawm ya Nabii Daawuud Asalam alay kum warahmatullahi wabarakatuh Mimi nataka kuwa nafunga swaumu kama ile ya nabiyyullahi iberaahiym na kula leo na funga kesho lakini mimi napenda kusafiri sana sasa inajuzu kwangu kufunga swaumu hiyo ama uki anza haijuzu kupumzika na hakuna udhuru wowote?

JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa nia yako njema ya kutaka kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka. Hakika hilo ni wazo zuri na nia nzuri kwa kila Muislamu kuwa nayo. Kwa hiyo, tunakuombea tawfiki wewe nasi pia tuweze kuihuisha Sunnah hiyo njema. Hakika ndugu yetu hiyo Sunnah uliyoitaja sio swawm ya Nabii Ibraahim (‘Alayhis Salaam) bali ni swawm ya Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam). Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) alikuwa na Sunnah nzuri sana katika mas-ala ya funga, kufunga siku moja na kuacha kufunga siku ya pili mpaka kitendo hicho kikapigiwa mfano na Mtume wetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Funga hiyo imeelezwa katika Hadiyth kadhaa, baadhi yake ni: · Amesimulia ‘Abdallaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Hakika wewe unafunga kila siku na kuswali usiku mzima?” Nikasema: “Ndio”. Akasema: “…Hapana swawm ya mwenye kufunga milele, swawm ya siku tatu kila mwezi ni kama swawm ya mwezi mzima”. Nikasema: “Mimi naweza kulivyo”. Akasema: “Hivyo, funga swawm ya Daawuud (‘Alayhis Salaam), yeye alikuwa akifunga siku na kula siku ya pili yake, na hakimbii anapokutana na adui” (al-Bukhaariy, Muslim, · Imepokewa kwa ‘Abdallaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Swawm inayopendwa na Allaah ni funga ya Daawuud, na Swalah inayopendwa na Allaah ni Swalah ya Daawuud. Alikuwa akilala nusu ya usiku, akiswali thuluthi yake na kulala sudusi (1/6). Alikuwa akila siku moja na kufunga siku ya moja” (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah). Hizi funga na Swalah zilizotajwa ni zile za Sunnah sio za faradhi. Ni vyema na vizuri kwa Muislamu anapoanza jambo jema (Sunnah yoyote) basi adumu nayo hata kama inaonekana ndogo na hilo ndilo jambo bora. Lakini kwa kuwa Uislamu ni Dini ya Maumbile, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametuwekea mfumo wa kutekeleza hayo. Katika Ibaadah za faradhi kama vile Funga, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametusahilishia kwa njia kuwa lau mtu atakuwa mgonjwa au katika safari anaweza kula siku katika Ramadhaan kisha kulipa baadaye. Sasa kwa kuwa wewe ni mtu wa safari unaweza kuwa unafunga wakati uko nyumbani au mjini kwako, na wakati ukiwa katika safari ukawa unakula. Lakini kwa neema ya Uislamu, ikiwa utashika Sunnah hii au nyingine yoyote na ukashindwa kuitekeleza kwa sababu ya udhuru basi Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anakuandikia thawabu ya aliyefunga ukiwa na ikhlaas na nia nzuri. Na Allah Anajua zaidi






Vitambulisho: