Swawm Yake Inakubaliwa Ikiwa Hasemi Na Mume Wake?


418

SWALI: swali kuhusu funga yangu kama inakubaliwa kwa sababu mimi na mume wangu hatusemi wala hatuna masikizano muda wa miezi . nataka kujua kama funga yangu inakubaliwa tunaishi pamoja na anakula ndani ya nyumba lakini hasemi na mimi .nisha muelezea kuwa hi niramadhan tukae kwa amani ili tufunge mwezi mtukufu kwa salama lakini hakunisikiza . jazaka allah kher naomba nipate jibu hili kwa haraka sana mungu wazidishie ilmu yenu

JIBU: Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Tunasikitika kuona hali kama hii na ndugu Waislam kukaa mwezi katika hali ya uhasama khaswa kwa walio karibu zaidi kama hali hii ya mke na mume. Tunakupa nasaha kwako na mumeo mzingatie hatari ya hali yenu hiyo. NASAHA KWA MKE Hukueleza sababu ya mume wako kukukasirikia hadi asikusemeshe, bila shaka kuna sababu nzito ikiwa hali imefika hivyo. Inakupasa utimize haki za mumeo ipasavyo na uwe maridhia kwake ili upate radhi za Mola wako. Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesisitiza sana mke kumtii mume wake hadi kusema: ((لَوْ كُنْتُ آمِراً أَحَداً أَنْ يَسْجُدَ لأَِحَدٍ لأَمَرْتُ الْمَرْأَةَ أَنْ تَسْجُدَ لِزَوْجِهَا مِنْ عِظَمِ حَقَِّهِ عَلَيْهاَ)) ((Kama ningeliweza kumuamrisha mtu amsujudie binaadamu mwenzake, ningeliamrisha mwanamke amsujudie mume wake kwa jinsi haki ya mume ilivyo tukufu kwa mke wake)) [Tuhfat Al-Ahwadhiy 4.323 kutoka Tafsiyr ya Ibn Kathiyr] Kwa hivyo, ingawa umemuomba mpatane kwa ajili ya Ramadhaan, lakini ni vizuri kwanza kufanya yafuatayo ili kurudisha hali ya mumeo awe radhi na katika furaha Insha Allah: 1. Mtake msamaha mume wako kwa makosa yoyote uliyofanya, na kwa kumpa maneno mazuri hadi alainike na akubali msamaha wako na awe radhi na wewe. 2. Jitahidi sana kutokurudia makosa hayo tena. 3. Timiza mas-uliya (jukumu) yako ya nyumba kikamilifu yakiwa ni kutazama nyumba, kulea watoto kumhudumia mumeo n.k. 4. Zidisha mapenzi kwa mumeo kwa kumpa maneno mazuri daima, kujiweka katika hali ya kupendeza kila mara, kutabasamu naye na kumridhisha kwa lolote analotaka umfanyie. (Isipokuwa maasi ya Allah na Mtume Wake) (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 5. Tekeleza ibada yako inavyopasa na omba Du'aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Adumishe ndoa yako kwa salama, amani na mapenzi. NASAHA KWA MUME Tambua kuwa kila binaadamu ni mkosa, na mbora ni yule mwenye kukiri makosa yake na kutubu kama Alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((كل ابن آدم خطّاء وخير الخطّائين التوابون ) ) رواه الترمذي وحسنه الألباني ((Kila mwanadamu ni mkosa na mbora mwenye kukosa ni yule anayetubia)) [Imepokelewa na At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hassan Shaykh Al-Albaaniy] Ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ambaye ni Mola wa Mbingu na Ardhi, na Mola wa viumbe vyote, Mwenye Kutupa uhai na afya, Anayeturuzuku na juu ya hivyo tunamuasi, lakini Anatughufuria madhambi na makosa yetu, sasa kwa nini sisi binaadamu tuwe wagumu na tuone uzito kusamehe wenzetu? Hakika inakupasa uzingatie hili, uondoshe uzito katika moyo wako na umsamehe mwenzako anapokuomba msamaha. Ukhasama baina ya ndugu Waislamu ni jambo la hatari kwani Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhadharisha tusikae zaidi ya siku tatu katika uhasama, na hali yenu hiyo ni zaidi ya siku tatu bali ni mwezi mzima. عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا ، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلامِ .(( رواه البخاري ومسلم و في رواية أبو داود بإسناد على شرط البخاري ومسلم ((فَمَنْ هَجَرَ فَوْقَ ثَلاَثٍ فَمَاتَ دَخَلَ النَارَ )) Imetoka kwa Abu Ayyuub Al-Answariy (Radhiya Allahu 'anhu) ambaye alisema: Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam)) [Al-Bukhaariy na Muslim na katika Riwayaah ya Abu Daawuud ((Atakayemhama (mwenzake) zaidi ya siku tatu akafariki basi ataingia motoni)) Zaidi ya hivyo ni kuwa huo ni undugu wenu wa uhusiano ambao ndio zaidi uliokemewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Qur-aan na Sunnah. Kisha hatari zaidi ni kwamba amali (vitendo) zako huwa hazipokelewi hadi upatane na ndugu yako kama ilivyo katika dalili ifuatayo: عن أبي هريرة رضي الله عنه قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : (( تُعرض الأعمال في كل أثنين وخميس فيغفر الله لكل أمريء لايشرك بالله شيئاً، إلا إمرءاً بينه وبين أخيه شحناء فيقول : اتركوا هذين حتى يصطلحا)) رواه مسلم Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Amali njema (vitendo vyema) huoneshwa kila Jumatatu na Alkhamiys, kisha Allaah Humghufuria kila mtu asiyemshiriki kitu Allaah, isipokuwa mtu aliyekuwa baina yake na baina ya ndugu yake uhasama, Husema: Waacheni hawa wawili mpaka wapatane)) [Muslim] Hali hiyo ya uhasama inapasa kuzingatiwa zaidi hatari yake tukiwa katika mwezi huu mtukufu, ikiwa Hadiyth kama hizo zinatupa maonyo makali, vipi mtu anategemea kukubaliwa amali zake, na vipi hana khofu ya matokea yake? Hatari hiyo haitokuhusu wewe mke ambaye umejaribu kuzungumza na mume wako lakini hataki kusikia. Hatari itakuwa kwa mume kama Hadithi zinazoonyesha. Funga yako itakuwa ni sawa, lakini yake itakuwa na walakini kwa sababu ya kosa lake hilo. Inabidi nawe umtakie mema kwa kumlingania kwa kumuonyesha Hadithi hizi. Una wajibu wa kumuokoa na adhabu ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani akibakia hivyo mpaka anapoaga dunia mpaka atakuwa na tatizo kubwa. Hiyo hali munayokaa si nzuri kama mume na mke, hivyo tunaomba mukae chini ili muzungumze kama mume na mke na mufikie mufaka. Muumini khaswa ni yule mwenye kuamini maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yanapomfikia na kuingiwa na khofu na kutekeleza amri hizo bila ya kusita. Hivyo tunatumai ndugu yetu utazingatia na kujirudi, umsamehe mke wako ambaye yuko tayari kukuomba msamaha. Bila shaka shaytwaan amekuvaa na kukutia uzito huo, hivyo jitahidi kumuepuka shaytwaan uwe katika salama na Mola wako. Tunatumai kwa nasaha hizi, ndugu zetu wengine wote ambao wana uhasama na ndugu zao au wenzao wafuate nasaha hizi kwa moyo mkunjufu ili Swawm na amali zao zote za mwezi huu mtukufu zikubaliwe na wapate radhi za Mola wao. Kumbukeni kuwa mbora zaidi ni yule mwenye kuanza kutaka sulhu (kupatana) kama alivyosema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth hiyo ya juu tuliyoitaja. Na Allaah Anajua zaidi






Vitambulisho:




Hukumu za Swala