JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atupatie tawfiki ya kuweza kutekeleza ‘Ibaadah Zake zote kwa kiasi tunachoweza na Atufishe tukiwa katika Imani na Uislamu, Aamiyn. Swali la mwanzo, jibu lake linapatikana katika kiungo kifuatacho: Zakaah Ikiwa Mtaji Unaongezeka Itolewa Vipi? Jibu kwa suala lililo juu yaonyesha limeleta utata kwa muulizaji, ambaye amelirudisha tena katika ukumbi. Mara nyingi wengi wetu hutumia mantiki katika mas-ala ya Kidini na mara nyingine mantiki na akili hii huwa haifanyi kazi na matokeo yake huleta natija mbaya. Kwa ajili hiyo ndiyo ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema: “Ikiwa Dini inakwenda kwa rai (mantiki) basi ingekuwa kupangusa khufu (soksi za ngozi [wakati wa wudhuu]) ni chini (kwenye uchafu) na siyo juu yake, lakini hivi ndivyo nilivyomuona Mtume akifanya [akipangusa juu na si chini]”. Tukirudi katika suala lako ni kuwa mwanzo hakuna mtu katika dunia hii ambaye pesa zake zinaongezeka kwa mamilioni kama ulivyo ashiria. Hawa wenye ziada ya aina hii ya pesa ni wale mabilionea ambao kwao pesa si chochote, na watu aina hiyo ni wachache. Sijui kama jambo hilo limetokea kwako au vipi? Au ni fikra tu ambayo imekupitia kuwa huenda likawa linatokea. Yaani kwako ulikuwa na 1000 kama katika mfano wetu wa awali ambacho ndicho kiwango cha chini cha kutolewa Zakaah na kabla ya mwezi kufika kwa Hawl pesa hizo zikawa mamilioni. Hili kwa uhakika si jambo jepesi kwa mtu kufikia hasa kwa hali hiyo ya mfano uliopigiwa. Hata kama hilo limetokea kweli basi mtu mwenyewe atabidi alipe Zakaah kwa pesa hizo zote (mamilioni aliyonayo). Hakika ni kuwa japokuwa pesa nyingi kati ya hizo hazikufikiwa na mwaka (Hawl) lakini kwa kuwa ziliingia hizo pesa kabla ya Hawl kufika itabidi azitolee Zakaah zote. Hakika ni kuwa Zakaah ni usaidizi kwa masikini, faradhi kwa matajiri, thawabu nyingi na ni nyongeza/ ziada kwa mtoaji. Kwa hivyo mtoaji mali yake inazidi badala ya kupungua anapotoa. Hivyo ni juu yetu sisi kutofikiria kuhusu kiwango tunachotoa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) katika kumridhisha Yeye kwani tufahamu hizo pesa ni amana tu tuliyopewa na Muumba wetu (Subhaanahu wa Ta‘ala). Lau Anataka basi badala ya kuongezeka kwa muda mfupi kutoka 1,000 hadi milioni moja au zaidi inawezekana Azipunguze kutoka 1,000 hadi –10,000. Kutoa hizo ni kweri kwako hapa duniani na ujira mkubwa utaupata Kesho Akhera. Hiyo ni katika fadhila ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), ukishukuru kwa kutekeleza jukumu hilo la kutoa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Atakuongezea na ukikanusha basi tambua kuwa adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) inaumiza na ni kali sana. Na Allaah Anajua zaidi