JIBU: Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. Shukrani kwa swali lako kuhusu utoaji wa Zakaah. Zakaah ni ‘Ibaadah na miongoni mwa nguzo ya Uislamu muhimu sana yenye faida kubwa sana kwa jamii yetu. Zakaah kama ‘Ibaadah nyingine yoyote ina masharti ambayo yanafaa yatekelezwe kabla ya mtu kupaswa kuitoa. Masharti muhimu ya kumpasa mtu kutoa Zakaah ni yafuatayo: 1. Kuwa na Niswaab (kiwango cha chini) ambapo Muislamu akiwa nacho inampasa yeye kutoa Zakaah. Na kiwango hicho ni mtu kuwa na akiba ya pesa zinazotosha kununua gramu 82 za dhahabu safi. 2. Akiba hiyo ipitiwe na mwaka katika kalenda ya Kiislamu bila ya kupungua kabisa. Ikiwa umetimiza masharti haya mawili basi inakupasa kutoa Zakaah. Sasa ni kutazama akiba yako kwa mfano mshahara wako ni yeni laki moja, lakini akiba yako mwisho wa mwezi ni ngapi? Ikusanye hiyo akiba kila mwezi mpaka ifike hiyo Niswaab. Tarehe akiba yako itakapofikia Niswaab ndio utaanza kuhesabu mwaka, ikiwa baada ya mwaka kiwango ni vile vile au kimepanda itabidi utoe Zakaah. Na ikiwa hutofikia Niswaab hakuna Zakaah kwako mpaka uifikie hiyo Niswaab. Ama duka nalo ni hivyo hivyo, utakusanya faida unayopata kama vile ulivyohesabu akiba yako ya mshahara. Utakuwa unaweka rekodi ya ununuzi na mauzo yako na ile faida uliyopata mwisho wa mwaka. Faida hiyo ni baada ya kutoa matumizi yako yote pamoja na bidhaa ulizonazo na thamani yake. Ikiwa imefikiwa na Niswaab pamoja na akiba ya mshahara wako utaanza kuhesabu mwaka wa Kiislamu. Ukifika mwaka huo nawe una kiwango hicho cha chini itabidi utoe Zakaah. La, sivyo basi utakuwa huna wajibu wa kutoa Zakaah japokuwa utawajibika kutoa Swadaqah. Na Allaah Anajua zaidi